KILIMO BORA CHA BAMIA sehemu ya 02
MATUNZO YA SHAMBA BAADA YA KUPANDA
Matunzo
ya shamba ni muhimu sana kwa sababu huamua kiasi cha mavuno unayoweza
kupata kutoka shambani. Shamba ambalo halipati matunzo mazuri hata kama
mbegu bora inayozaa sana itatumika mavuno bado yatakuwa hafifu. Matunzo
ya shamba hujumuisha;
Umwagiliaji
i. Njia za umwagiliaji
Kuna
njia tofauti za umwagiliaji ambazo zinaweza kutumika katika umwagiliaji
wa bustani ya bamia kama vile umwagiliaji wa njia ya matone (drip
irrigation), wa njia ya mifereji na umwagiliaji wa kutumia cane. Kwa
kilimo cha kiangazi au pale mvua zinapokuwa hafifu ni muhimu kufanya
umwagiliaji wa bustani yako ili kuepuka kunyauka kwa mazao shambani
kutokana na upotevu mkubwa wa maji. Wakati wa kumwagilia hakikisha
haumwagii maji katika majani bali katika shimo chini ya kichaka cha mche
(canopy).
ii. Ratiba ya umwagiliaji
Unaweza
kumwagilia bustani ya bamia kila baada siku mbili hadi tatu kutegemeana
na hali ya hewa na udongo. Cha msingi usiache udongo ukauke bali mwagia
maji angalau asilimia hamsini ya unyevu wa udongo unapokuwa umepotea.
Mambo ya kuzingatia
Ni
vyema umwagiliaji wa bustani uzingatie hatua za ukuaji wa mimea
bustanini, hali ya hewa na uwezo wa udongo kutunza maji. Mahitaji ya
maji kwa zao la bamia huongezeka wakati wa kutoa maua na kutengeneza
matunda. Vilevile katika maeneo yenye hali ya joto na udongo wa kichanga
maji hupotea kwa urahisi. Hakikisha maji hayatuami katika shamba lako
kuepuka kuoza kwa mizizi na udongo haukauki.
Kupunguzia
Ng’olea
miche katika shamba wakati wa kufanya palizi ya kwanza wiki nne tangu
kupanda ikiwa na urefu wa sm 10 hadi 15. Bakiza mmea mmoja wenye afya
katika kila shimo. Mimea iliyong’olewa kutoka katika shimo moja inaweza
kupandikizwa katika shimo lingine ambalo mbegu hazikuota.
Kuweka Mbolea
Weka
mbolea ya kukuzia aina ya Urea wiki sita tangu kupanda kwa kiwango cha
nusu kizibo cha soda kuzunguka shina sm 5 kutoka shina lilipo na kurudia
kuweka tena kila baada ya wiki mbili hadi mwisho wa kuvuna. Mmea
unapokuwa mkubwa wenye majani mengi usiweke mbolea ya kukuzia hadi bamia
zitakapo toka vinginevyo mmea unaweza kuwa na majani mengi na kuzaa
bamia chache. Mfuko mmoja wa Urea wa kilo 50 unatosha kutumika katika
eneo la ekari moja.
Kupiga Dawa
i. Dawa za ukungu
Uchaguzi
wa dawa za ukungu hufuatana na magonjwa yanayoshambulia zao husika
hivyo ni vema kujua magonjwa yanayoshambulia zao la bamia kabla ya
kuchagua dawa za kutumia kama kinga au tiba pale magonjwa
yanapojitokeza. Unaweza kuanza kupiga dawa ya ukungu wiki moja hadi
mbili tangu miche kuota na kurudia kila baada ya wiki moja hadi mbili
kutegemeana na maelekezo ya dawa husika.
ii. Dawa za kuua wadudu
Nyunyizia
dawa ya kuua wadudu baada ya kuona wadudu waharibifu katika shamba lako
ili kuweza kuchagua dawa sahihi ya kudhibiti aina ya wadudu waliovamia
bustani yako.
Kupalilia
Palizi
ifanyike kuanzia wiki ya nne tangu kupanda na kurudia kila baada wiki
mbii hadi tatu. Hakikisha hakuna magugu bustanini katika kipindi cha
kutoka maua na kutengenezwa kwa matunda. Unaweza kupalilia kwa kutumia
mikono, jembe dogo la mkono au dawa za viuagugu zinazopatikana katika
maduka ya pembejeo za kilimo. Fuata ushauri wa wataalamu walio katika
eneo lako na maelezo ya dawa kama yalivyo kwenye lebo ya chupa.
Kuweka Matandazo
Matandazo
husaidia kudhibiti magugu, kuifadhi unyevu na kuongeza rutuba katika
udongo. Kwa matokeo mazuri katika udhibiti wa magugu inashauriwa kuweka
matandazo kwa kuyatandaza katika udongo katika kina cha sm 10 mpaka 15
maeneo yote ya tuta kuzunguka mashimo ya miche. Matandazo ya asili kama
mabua ya nafaka, pumba za mpunga, maganda ya karanga na maranda ya mbao
yanaweza kuwekwa kabla ya kupandikiza baada ya kuchimba mashimo ya
kupandia au baada ya kupandikiza. Matandazo ya plastiki huwekwa mapema
kabla ya kupandikiza baada ya kuandaa matuta.
KUVUNA
Kiwango cha mavuno
Kiwango
cha mavuno ya bamia kwa ekari moja hutegemeana na matunzo ya shamba,
uwezo wa kuzaa wa mbegu iliyotumika na idadi ya mimea katika shamba.
Mbegu za aina tofauti zina uwezo tofauti wa kuzaa na hivyo mavuno huwa
tofauti. Vilevile mashamba tofauti yaliyopandwa mbegu ya aina moja na
kupata matunzo ya viwango tofauti huwa na kiwango tofauti cha mavuno.
Kwa bustani ya bamia iliyopandwa mbegu bora na kutunzwa vizuri huweza
kutoa mavuno wastani wa tani 5 hadi 8 kwa ekari.
Muda wa Kuvuna
Bamia
huchukua siku 50 hadi 60 kuanza kuvuna. Huwa tayari kuvunwa siku tano
tangu kutoka kwa maua zikiwa bado changa na zenye urefu wa sm 5 hadi 10
kutegemeana na aina ya mbegu. Hivyo basi inashauriwa kuvuna bamia kila
baada ya siku tatu tangu mvuno wa kwanza wakati wa asubuhi. Uvunaji wa
bamia unaweza kuendelea kwa muda wa siku 30 hadi 40 tangu mvuno wa
kwanza.
Namna ya uvunaji
Mambo ya kuzingatia
Usiache
bamia zikomae kabla ya kuvuna kwa sababu bamia zilizokomaa huwa ngumu
na zenye nyuzi nyuzi na hivyo hazina soko kwa matumizi ya
nyumbani.Vilevile kuacha bamia zikomae katika mmea husababisha mmea
kuacha kuzaa mapema na hivyo mavuno huwa madogo. Tumia kisu au mkasi
wakati wa kuvuna ili kuepuka kuathiri shina na kusumbua mizizi ya mmea.
Vilevile usivune bamia zinazoonyesha dalili ya kuoza au kuathiriwa na
wadudu. Kwa baadhi ya watu bamia huweza kusababisha muwasho wa ngozi
hivyo hakikisha unavaa suruali ndefu na shati la mikono mirefu wakati wa
kuvuna.
Hatua za uvunaji
Hatua zifuatazo zinaweza kutumika katika uvunaji;
- Andaa vifaa na vyombo vya kuvunia kama vile kisu, mkasi na ndoo au chombo chochote cha plastiki kwa kuvisafisha kwa maji safi na sabuni.
- Andaa sehemu utakayokuwa unaweka bamia wakati wa kuvuna iliyo kivulini karibu na shamba na utandike turubai.
- Wakati wa kuvuna kata kikonyo cha bamia karibu na tawi linaloshikilia tunda kisha weka tunda kwenye ndoo. Hakikisha unavuna bamia na kikonyo chake ili zisiharibike kwa urahisi.
- Ndoo inapojaa bamia beba ukazitandaze katika turubai lililo tandikwa karibu na bustani ili zipate hewa na zipoe kutoka katika joto la shamba (field heat) kabla ya kuzipakia.
- Safisha vizuri vyombo vya kuvunia kwa maji safi na sabuni kila baada ya kumaliza siku ya kuvuna ili kuzuia vimelea vya magonjwa.
MATUNZO BAADA YA KUVUNA
Kupakia
Baada
ya kuvuna pakia bamia kwenye matenga au makreti yaliyo tengenezwa kwa
mbao au plastiki yenye matundu yanayo pitisha hewa vizuri. Hakikisha
upakiaji unafanyika kivulini ili bamia zisiunguzwe na jua.
Bamia huweza kuifadhiwa katika chumba maalum cha kuifadhia (cold room) katika nyuzi joto za sentigredi 7˚C hadi 10˚C na unyevu hewa 95% na kukaa bila kuharibika kwa muda wa siku saba hadi kumi. Vilevile unaweza kuifadhi bamia katika chumba chochote kisafi kikubwa chenye nafasi na kisicho na joto jingi chenye madirisha yanayo pitisha hewa vizuri, feni au Air conditioner kwa kupanga matenga kwa nafasi bila kuyarundika sehemu moja.
Mambo ya kuzingatia
Bamia
huweza kuharibika kwa haraka baada ya kuvunwa hivyo ni muhimu
kuhakikisha haziifadhiwi kwa muda mrefu na zinafika sokoni mapema baada
ya kuvunwa. Jambo hili litawezekana kwa urahisi ikiwa mkulima
atahakikisha soko linakuwa tayari kabla ya kuanza uvunaji.
Somo letu la bamia limeishia hapa, jiandae kwa somo li
KILIMO BORA CHA BAMIA sehemu ya 02
Reviewed by BENSON
on
March 04, 2018
Rating:
Enter your comment...naombeni hii kwenye email yangu mceddie09@gmail.com
ReplyDelete