KILIMO BORA CHA BAMIA SEHEMU YA 01
Bamia ni zao la mbogamboga linalotambulika kitaalamu kama Abelmoschus esculentus
lenye asili ya Ethipia na Afrika ya magharibi. Kwa sasa zao hili
linalimwa katika nchi nyingi hasa sehemu za joto. Baadhi ya maeneo
yanayolima zao la bamia kwa Tanzania ni pamoja na mikoa ya Morogoro,
Dodoma, Tabora, Pwani na Mbeya.
Matumizi ya Bamia
Zao
hili hulimwa kwa ajili ya matunda yake ambayo hutumika kama mboga au
kiungo katika mapishi mbalimbali majumbani. Vilevile katika nchi
zilizoendelea nyuzi nyuzi zinazotokana na zao hili hutumika katika
utengenezaji wa karatasi.
Aina za mbegu
Kuna
aina tofauti za mbegu za bamia zinazo patikana Tanzania kama vile
Clemson Spineless, Emerald Green, White Velvet, Perkins Mammoth na Dwarf
Prolific. Mbegu ambazo hutumika na wengi ni
- Clemson spineless. Mbegu hii inatabia ya kukua urefu wa mita 1 hadi 1.5 na kuzaa bamia za kijani zenye urefu karibu sm 15. Huchukua siku 55 hadi 58 kuanza kuvuna.
- Emerald green. Mbegu hii ina tabia ya kukua hadi urefu wa m 1.5 na kuzaa bamia za kijani zenye urefu wa sm 18 hadi 20. Huchukua siku 58 hadi 60 kuanza kuvuna.
- White velvet. Mbegu hii inatabia ya kukua urefu wa m 1.5 hadi 1.8 na kuzaa bamia ndefu, nyembamba, zilizochongoka na zenye urefu wa sm 15 hadi 18.
UCHAGUZI WA ENEO
Ni
muhimu kuchagua eneo linalofaa kwa kilimo cha bamia kabla ya kuanza
uzalishaji. Ni vyema eneo litakalotumika katika kilimo cha bamia liwe na
urahisi wa upatikanaji maji kurahisisha umwagiliaji kwa kilimo cha
umwagiliaji. Vilevile shamba liwe lenye kufikika kwa urahisi ili kufanya
wepesi katika kuhudumia shamba na usafirishaji wa mazao kwenda sokoni
au kufikiwa kwa urahisi na wanunuzi wanaofuata mazao shambani.
Zao
la bamia hushambuliwa sana na minyoo fundo (nematodes). Hivyo usichague
eneo ambalo limetoka kutumika katika kilimo cha mazao yanayoweza
kushambuliwa na minyoo fundo kama vile viazi vitamu, nyanya, bilinganya
na pilipili hoho. Kwa tahadhari unaweza kulima zao hili katika eneo
ambalo limetoka kutumika kwa kilimo cha mazao ya nafaka kama vile
mahindi na mtama kwa kuwa mazao haya hayashambuliwi na minyoo fundo.
MAHITAJI YA KIIKOLOJIA
Hali ya Hewa na Mwinuko
Bamia
ni zao linalopendelea hali ya joto hivyo hustawi katika maeneo yenye
hali joto kuanzia nyuzi joto za sentigredi 21 hadi 35. Ustawi mzuri
zaidi huonekana katika maeneo yenye joto la nyuzi za sentigredi 21 mpaka
30. Hali joto zaidi ya nyuzi za sentigredi 42 huweza kusababisha
kudondoka kwa maua. Bamia hustawi vizuri katika maeneo ya mwinuko
tofauti hadi mita 1000 kutoka usawa wa bahari yenye mvua za wastani.
Udongo
Zao
la bamia hustawi katika udongo wa aina nyingi wenye rutuba, kina, uwezo
wa kuifadhi maji vizuri na usiotuamisha maji. Hata hivyo zao hili
hufanya vizuri zaidi linapolimwa katika udongo wa tifutifu yenye
kichanga wenye rutuba ya kutosha na tindikali kuanzia Ph 5.8 hadi 6.5.
Mbegu za bamia hushindwa kuota kabisa pale joto la udongo linapokuwa
chini ya nyuzi za sentigredi 16.
KUANDAA SHAMBA
Muda wa Kuandaa
Shamba
la bamia liandaliwe mapema mwezi mmoja kabla ya kupanda ili kuruhusu
magugu na mabaki ya mazao kuoza vizuri. Kwa kilimo cha kutegemea mvua ni
vyema maandalizi yaanze mapema kabla ya kuanza kwa mvua za masika.
Inashauriwa kuanza maandalizi mapema mwezi Januari. Kwa kilimo cha
umwagiliaji unaweza kuanza maandalizi muda wowote kulingana na mahitaji
na soko unalolilenga.
Namna ya Kuandaa
Shamba huandaliwa kwa kufyeka nyasi, kung’oa visiki na kulima kabla ya kupima na kuweka matuta.
(i) Kulima
Shamba hulimwa kwa kutumia jembe la mkono, jembe la kukokotwa na wanyama, power tillers
au matrekta. Matumizi ya jembe la kukokotwa na wanyama, power tillers
na matrekta hurahisisha shughuli ya kulima na kuifanya iwe na ufanisi
kwani hukatua udongo vizuri na kuufanya uwe tifutifu. Unapotumia jembe
la mkono katika kulima hakikisha unakatua udongo katika kina cha kutosha
sm 20 mpaka sm 30 na kulainisha mabonge. Udongo uliokatuliwa vizuri
hupitisha hewa inayohitajika na mmea, hurahisisha ukuaji wa mizizi na
kuifadhi maji vizuri.
(ii) Kupima shamba (field layout)
Ni
muhimu kuanza kupima shamba kabla ya kuanza kuandaa matuta ili kupata
matuta yaliyo katika mpangilio mzuri na mistari ya mimea shambani
iliyonyooka vizuri. Kabla ya kupima matuta ni muhimu pia kujua nafasi ya
kupandia utakayo tumia ili kupata ukubwa sahihi wa kila tuta.
Kwa
mfano kwa nafasi ya kupandia ya sm 60 × sm 40 kwa matuta makubwa
unaweza kutengeneza kila tuta katika upana wa sm 1.2 na urefu wowote.
Acha nafasi ya m 1 kuzunguka shamba na njia kila baada ya tuta upana wa
sm 50. Tumia Tape measure au kamba yenye vipimo kupima shamba
huku ukiweka alama za matuta na njia kwa kuchomeka mambo (pegs) katika
kila kona ya tuta na kuzungushia kamba.
(iii) Kuweka matuta
Inashauliwa
kupanda bamia katika matuta ili kusaidia mizizi kukua vizuri na udongo
kuhifadhi maji. Wakati wa kiangazi, tengeneza matuta yaliyodidimia
kidogo ili kufanya maji yaweze kukaa kwenye udongo na wakati wa masika
matuta yainuliwe kidogo toka kwenye usawa wa ardhi ili kuzuia maji
yasituame. Matuta yanaweza kuwa makubwa au madogo kulingana na matakwa
ya mkulima. Matuta makubwa hupandwa mistari miwili na matuta madogo
hupandwa mstari mmoja. Tengeneza matuta kwa kufuata alama zilizowekwa
wakati wa kupima shamba.
UPANDAJI WA BAMIA
Zao
la bamia huweza kupandwa moja kwa moja shambani au kwa kuanzia
kitaluni. Hata hivyo wakulima wengi hupendelea zaidi kupanda zao hili
moja kwa moja shambani pasipo kupitia kitaluni. Katika eneo lenye udongo
mzito wenye asili ya mfinyanzi mbegu hupata shida kuota hivyo ni muhimu
kuanzia kitaluni ili kuweza kupata miche mingi shambani. Kwa kuanzia
kitaluni hakikisha unafuata taratibu zote za uandaaji na matunzo ya
kitalu cha mbogamboga na pandikiza miche pindi inapokua na majani halisi
matatu hadi manne.
Maandalizi ya Mbegu
Mbegu
za bamia ni ngumu kidogo katika kuota hivyo ni vyema ziandaliwe ili
kurahisisha uotaji wake. Mbegu za bamia huandaliwa kwa kuziloweka katika
maji ya vuguvugu kwa muda wa masaa ishirini na nne ili kuchochea
uotaji. Mbegu za bamia huchukua muda wa siku 5 hadi 10 kuota.
Kutegemeana na nafasi ya kupandia na uotaji wa mbegu kiasi cha kilo moja
na nusu hadi kilo mbili na nusu za mbegu kinaweza kutosha kupanda
katika eneo la ekari moja.
Nafasi ya Kupandia
Bamia
huweza kupandwa katika nafasi tofauti kuanzia sm 60 hadi 80 kati ya
mstari na mstari na sm 30 hadi 50 kutoka shimo hadi shimo.Hakikisha
unafuata maelekezo ya mbegu husika juu ya nafasi pendekezwa.
Hatua za Upandaji
Unaweza kufuata hatua zifuatazo katika upanzi wa mbegu za bamia shambani:
- Mwagia maji mengi shambani masaa kumi na mbili kabla ya kupanda mbegu ili kulainisha udongo na kurahisisha upanzi.
- Chimba mashimo ya kupandia yenye kina cha sm 2 hadi 3 katika nafasi iliyopendekezwa kwa mbegu itakayotumika mistari miwili miwili kila tuta kwa kutumia kamba iliyowekwa vipimo.
- Weka viganja viwili vya mkono vya samadi iliyoiva katika shimo la kupandia kisha changanya na udongo kupata mchanganyiko mzuri. Kwa mbolea ya kupandia kama DAP weka nusu kizibo cha soda katika kila shimo la kupandia kisha fukia mbolea kwa tabaka dogo la udongo kabla ya kupanda mbegu. Kiasi cha kilo hamsini za mbolea ya DAP kinatosha kutumika katika eneo la ekari moja.
- Panda mbegu mbili katika kila shimo, fukia kwa udongo mwepesi, shindilia na kisha mwagia maji.
KILIMO BORA CHA BAMIA SEHEMU YA 01
Reviewed by BENSON
on
March 03, 2018
Rating:
No comments