JINSI YA KUTATUA CHANGAMOTO YA SOKO KWENYE KILIMO CHA BIASHARA
Katika makala ya leo tunakwenda kuangalia changamoto ya masoko kwenye kilimo cha kibiashara. Kabla hatujaingia na kuangalia changamoto hii, tuangalizie kwanza kilimo kwa siku za hivi karibuni. Kwa sasa kilimo kimekuwa tu siyo kilimo, bali kimekuwa ujasiriamali na hata biashara kwa wengi ambao wanataka kujikwamua kiuchumi. Kadiri hali ya uchumi inavyokuwa ngumu, kukosekana kwa ajira na hata kutoridhishwa na kipato kwa wale walioajiriwa, watu wengi wamelazimika kuingia kwenye kilimo.
Kilimo kinaonesha dalili nzuri za kuweza kumtoa mtu yeyote anayekifanya
vizuri na kwa ubunifu. Hii ni kwa sababu bado uhitaji wa mazao ya kilimo
ni mkubwa ndani na nje ya nchi. Lakini pamoja na uwezo huu wa kilimo
kuwatoa watu kifedha, bado changamoto ni nyingi. Changamoto zinaanzia
kwenye upatikanaji wa shamba bora, upatikanaji wa maji ya umwagiliaji
kwa sababu mvua sio za uhakika. Upatikanaji wa mbegu bora pia ni
changamoto kubwa, wasaidizi kwenye shughuli hizi za kilimo nao wamekuwa
changamoto, siyo watu wote wapo tayari kujitoa.
Ukiweza kuvuka changamoto zote hizo, za kuanzia shamba mpaka kuvuna,
kuna changamoto kubwa inayokuwa mbele yako mkulima, changamoto hii ni
soko. Kumekuwa na watu wa katikati ya mkulima na mlaji, watu hawa
wanajulikana kama madalali. Hawa wamekuwa wakipata faida mara dufu
kuliko hata mkulima aliyeteseka shambani kwa muda mrefu. Je unawezaje
kutatua changamoto hii ya soko kwenye kilimo cha kibiashara?
Hapa tutakwenda kushirikishana mbinu za kufanya hivyo. Lakini kabla
hatujaingia kwenye ushauri wenyewe, tusome maoni ya mwenzetu
aliyetuandikia kuomba ushauri juu ya hili;
Nina malengo ya kulima kilimo cha biashara cha matikiti maji, lakini
changamoto kubwa ninayoiona ni soko, wakulima tunalanguliwa sana hasa
mashambani na ukizingatia mimi ni mkulima ninayetaka kuanza, naomba
msaada katika hili. Naishi dar maeneo ya kigamboni, Ahsante. David
Haule.
Kwa mwenzetu David pamoja na wengine wote ambao mnapitia changamoto ya
masoko kwenye kilimo, hapa kuna mambo muhimu sana kuzingatia ili
kuondokana na changamoto hii ya masoko.
KWANZA; Angalia aina ya kilimo unachofanya au kutaka kufanya.
Kumekuwa na wimbi la watu kukimbilia kilimo cha zao fulani, kwa sababu
tu kuna watu wachache waliofanya kilimo hiko na wakafanikiwa. Mfano
mzuri ni kilimo cha matikiti maji. Zao hili ndiyo limekuwa kimbilio kwa
kila anayefikiria kuingia kwenye kilimo. Hii ni kutokana na ufupi wa
msimu wake na usambazaji wake kuwa mkubwa.
Kuna sheria moja ya uchumi inasema kwamba kadiri kitu kinavyopatikana
kwa wingi, bei yake inakuwa ndogo. Na hili ndilo limekuwa linatokea kwa
wakulima wanaolima mazao yanayoliwa na wengi. Unapofika msimu wa mavuno,
bei inakwenda chini kwa sababu kila mtu anauza. Na hapa ndipo madalali
wanaponufaika sana kwa kununua kwa bei ya chini sana na kwenda kuuza kwa
bei ambayo wao watapata faida. Hawajali kama bei wanayonunua kwako
mkulima itarudisha gharama zao, wanachoangalia ni kama wao wanapata
faida.
Hatua ya kuchukua hapa ni epuka kulima mazao ambayo kila mtu anakimbilia
kulima, na ikiwa ndiyo chaguo lako basi una vitu viwili vya kufanya,
cha kwanza ni kulima tofauti na msimu, yaani ujipange ili unapovuna
upatikanaji usiwe mkubwa. Cha pili soma namba mbili hapo chini.
PILI; Hakikisha unatoa mazao bora sana.
Watu wengi wanapokutana na changamoto hiyo hapo juu, pale madalali
wanapotaka kununua mazao yao kwa bei ya chini, hukataa na kuamua
kupeleka mazao yao sokoni wao wenyewe. Na hapa ndipo wanapokutana na
ukweli mchungu, wakifika sokoni, watu wanachagua ubora. Kwa zao kama
tikiti maji, watu wanaangalia mbegu na ukubwa wa tunda. Ukipeleka
matunda madogo utajikuta unapata hasara kubwa kuliko hata ungemuuzia
dalali shambani.
Hivyo hakikisha kwa kilimo chochote unachochagua kufanya, mazao unayotoa
ni bora sana. Unapokuwa na mazao bora, hata dalali akifika shambani,
hatakuwa na nguvu ya kukuburuza, na akitaka kufanya hivyo unaweza kuamua
kuyapeleka sokoni wewe mwenyewe. Kwa zao la tikiti, unapokuwa na
matunda makubwa, mnahesabiana na dalali na kuuziana kwa bei fulani kwa
kila tunda, lakini ukiwa na matunda madogo ananunua kama mzigo hivyo
anakadiria tu bei.
Kilimo chochote unachochagua kufanya, hakikisha unatoa mazao bora sana.
Weka juhudi kubwa, fuatilia kwa karibu kuhakikisha unatoa mazao ambayo
unaweza kuyauza popote pale.
TATU; Tafuta njia mbadala za kusambaza mazao yako.
Kama umechagua kufanya kilimo cha kibiashara, basi unahitaji kutafuta
njia mbadala ya kusambaza mazao yako. Unaweza kuyasambaza kwa kupeleka
sokoni na kuuza kwa jumla, au unaweza kuyasambaza kwa kuuza kwa
rejareja. Unachohitaji ni kuangalia wapi ambapo mazao yako yanaweza
kuhitajika kisha tengeneza mtandao wako wa masoko. Kwa mazao ya nafaka
unaweza kuuza moja kwa moja kwa walaji kama mahoteli, shule na hata
taasisi nyingine zinazotumia nafaka katika vyakula.
Ili kuweza kusambaza mazao yako mwenyewe, unahitaji kuwa na mazao bora, ambayo yatawafanya watu wayafurahie.
NNE; Ongeza thamani ya mazao yako.
Tatizo kubwa ambalo wakulima wengi wanapitia ni kukosa taarifa za
kutosha, na hivyo wenye taarifa wanazitumia kufaidika zaidi. Kwa mfano
mtu analima mpunga na kuuza ukiwa kama mpunga. Mtu mwingine anaununua na
kukoboa, anapata mchele na kuupanga katika viwango tofauti. Anatafuta
vifungashio na kufunga mchele huo na kuuza kwenye maeneo mbalimbali,
ikiwepo kusambaza nje ya nchi. Kwa mkulima wa kawaida anaweza kuona hili
ni jambo kubwa sana ambalo yeye hawezi kufanya. Lakini kwa kupata
taarifa sahihi mkulima yeyote anaweza kuongeza thamani kwenye mazao
yake.
Kwenye zao lolote unalolima, jiulize ni kwa namna gani unaweza kuongeza
thamani ili usiuze likiwa ghafi. Bei ya kitu ghafi na kilichoongezwa
thamani ni tofauti kubwa sana. Fikiria ni namba gani unaweza kuongeza
thamani kwenye zao unalolima.
TANO; Pata taarifa, jielimishe kuhusu kile unachozalisha na kilimo kwa ujumla.
Kuna taarifa nyingi sana kuhusu kilimo lakini wakulima wanazo chache
mno. Wakulima wengi wamekuwa wavivu kujifunza vitu vipya kuhusu kilimo.
Wengi wamekuwa wakilima kwa mazoea, wengine wamekuwa na imani zisizo
sahihi kwenye kilimo kuhusu matumizi ya mbegu za kisasa na mbolea za
viwandani. Jielimishe kuhusu kile kilimo unachofanya, jua wengine
wanaolima na wakafanikiwa ni mbinu gani wanatumia. Jua mbegu bora zaidi
ni zipi na zinahitaji mazingira gani.
Unapoamua kufanya kilimo sehemu yako ya kujiingizia kipato, chukulia ile
ndiyo kazi yako, na mara zote angalia fursa ya kujifunza kupitia kilimo
unachofanya. Unapolima na kupata mazao ambayo siyo viwango
ulivyotarajia, jiulize ni wapi ulikosea na wakati mwingine usirudie kosa
hili.
Kilimo siyo rahisi hata kidogo, unahitaji kuweka juhudi kubwa kwenye
kulima, kujifunza na hata kusambaza mazao yako. unahitaji kuweka juhudi
kubwa ili kuweza kufikia malengo yako ya kifedha kupitia kilimo. Jambo
zuri ni kwamba inawezekana, kwa sababu wapo wengi walioweza.
JINSI YA KUTATUA CHANGAMOTO YA SOKO KWENYE KILIMO CHA BIASHARA
Reviewed by BENSON
on
March 09, 2018
Rating:
No comments