YAFAHAMUMAGONJWA HATARI YA NYANYA NA DAWA ZAKE

Pamoja na umuhimu wake, magonjwa ya nyanya yamekuwa ni kikwazo kikubwa sana katika uzalishaji na ubora wa matunda ya nyanya. Sasa ili mkulima aweze kupata faida na kuongeza pato lake ni vema kuzingatia udhibiti wa magonjwa ya nyanya tangu mwanzo zinapoonekana dalili.

Utangulizi
Nyanya ni zao la chakula na biashara. Kilimo cha zao hili hufanyika majira yote (masika na kiangazi), na faida hupatikana haraka na ni ya kuridhisha ikilinganishwa na mazao mengine. Pamoja na umuhimu wa zao hili, wadudu waharibifu na magonjwa huathiri uzalishaji na ubora wa matunda. Ili mkulima aweze kupata faida na kuongeza pato la kaya yake ni vema kuzingatia udhibiti wa magonjwa na wadudu wa zao hili. Katika makala hii tutaangalia namna ya kudhibiti baadhi ya magonjwa muhimu ya zao la Nyanya.

1. Ugonjwa wa Ukungu
(i) Bakajani tangulia au ukungu mapema: Early blight (Alternaria solani)
Dalili
Dalili za ukungu mapema hutokea kwenye matunda, shina, na majani ya nyanya. Majani huonesha madoa ya kahawia iliyokoza na yenye mfumo wa duara zenye kati moja. Madoa kwanza hujitokeza kwenye majani yaliyokomaa na kuendelea juu ya mmea. Majani yenye madoa huweza kufa kabla ya wakati wake na kusababisha kupukutika mapema kwa majani, matunda huungua kwa jua na kuwa na rangi isiyopendeza.
Madoa ya kwenye matunda hujitokeza kwa juu kwenye ncha ya shina. Kwa kawaida madoa huwa na rangi ya kahawia iliyokoza mpaka nyeusi, yaliyozama ndani, magumu na yenye duara za kipekee zenye mfumo wa kati moja. Kuoza kwa chini ya shina huweza kutokea kwenye miche michanga. Hali hii hujionyesha kwa kuzunguka shina sehemu ya chini. Miche iliyoathirika hudumaa na huweza kunyauka na kufa. Miche mikubwa iliyoathirika huwa na makovu ambayo kawaida huwa upande mmoja tu wa shina na hurefuka na kudidimia kwenye mashina na vikonyo.
Jani-la-nyanya-lenye-dalili-za-ukungu-tangulia
Dalili za ugonjwa wa ukungu tangulia

Dalili za ugonjwa wa ukungu mapema mara nyingi hudhaniwa kuwa ni ukungu chelewa, lakini kwenye ukungu chelewa makovu yamefifia, madogo na hayana alama za duara zilizonyanyuka.

Njia za kudhibiti
Ukungu mapema unaweza kubainika shambani kwa kutafuta madoa ya kahawia iliyokoza ya kiasi cha 1.2 sm kwa upana. Ni vigumu sana kuzuia ukungu mapema ukishaanza shambani. Njia muhimu ya kudhibiti ukungu mapema ni kuzuia kuingia kwake na kusambaa.

Mbinu bora za kilimo
•Zungusha mazao ya nyanya na nafaka ndogo ndogo, mahindi au jamii za kunde
•Panda aina zenye kustahimili ‘early blight’. (Km. Floradade, Hytec 36, Julius F1 na Zest F1)
•Tumia mbegu safi
•Limia na kufukia mabaki ya mazao baada ya mavuno na choma moto mazao yaliyoathirika na takataka zote za mazao
•Epuka kumwagilia kwa juu
•Ongezea mbolea ya samadi
•Tumia matandazo kuzuia kurukia kwa maji
•Hakikisha kupanda kwa nafasi sahihi na kufunga vijiti
•Toa majani ya chini yaliyoathirika ili kuboresha mzunguko wa hewa
•Epuka kutumia ardhi kwa angalau miaka 2 baada ya uzalishaji wa nyanya

Dawa (chemical control)
‘Early blight’ inaweza kudhibitiwa kwa kutumia dawa za ukungu Boscalid ( Endura Captan, Captan 4F, Captan 50), dawa za ukungu zenye shaba (Champ Dry Prill, Champ Formula 2, Copper-Count-N, Kocide 101, Kocide DF, Kocide 4.5LF, Kocide 3000, Nordox Tri Basic), Chlorothalonil na Chlorothalonil Mixtures (Bravo 720/Echo, Bravo Ultrex/Echo 90DF, Bravo Weather Stik, Echo Zn, Ridomil Gold/Bravo), EBDC, Copper FBDC na EBDC/Zaxamide (Cuaprofix Disperss M2, Dithane/Gavel, Maneb 75, Manex, Mankocide, Manzate F1, Penncozeb 80W, Penncozeb 75DF), Famoxadone+Cymoxanil (Tanos, Fenamidone, Reason 500SC, Penthiopyrad, Fontelis, Pyrimethanil, Scala), Strobilurin na Strobilurin Mixtures (Cabrio, Flint, Quadris)

Kibaiolojia (Biological control)
Kuna mazao mengi yatokanayo na mimea ambayo husemekana kuwa na sifa za sumu kwa aina nyingi za ukungu. Haya ni mazao asilia ambayo hupoteza nguvu zake haraka juu ya majani na kwenye udongo. Juu ya hivyo, taarifa kidogo sana zinajulikana kuhusu viwango vyao vya matumizi, athari zao juu ya viumbe marafiki, na binadamu.

(ii) Bakajani Chelewa au Ukungu chelewa: Late blight (Phytophthora infestans)
Dalili
Dalili za ukungu chelewa hujitokeza kwenye matunda, majani, shina na matawi. Kwenye majani madoa ya kijani kibichi/kahawia hujitokeza upande wa juu wa majani, na pembezoni mwa majani huwa kijani kibichi na huwa kama iliyotota, kwa kawaida madoa hutanuka ghafla hadi majani yote yanapokufa. Nyakati za hewa ya unyevu, ukungu mweupe/kijivujivu hujitokeza kwenye kingo za madoa katika sehemu za chini za majani. Wakati wa joto, sehemu zilizoathirika huonesha kukauka. Madoa ya kahawia na yaliyorefuka hujitokeza kwenye mashina.
Kwenye matunda, madoa ya kijivujivu/kijani yaliyotota hujitokeza kwenye nusu ya tunda upande wa juu. Madoa haya baadae husambaa na kugeuka kahawia, yaliyokunjamana na magumu. Wakati wa hali ya unyevu ukungu mweupe hujitokeza kwenye sehemu za matunda yaliyoathirika. Dalili za ukungu chelewa mara nyingi hudhaniwa ni ukungu mapema (Alternaria solani), lakini dalili za ukungu mapema mara nyingi huwa za duara zaidi, kubwa, na zilizokoza na za duara zenye kati moja. Ukungu chelewa hauna duara hizi.
Matunda-ya-nyanya-yaliyoathiriwa-na-ukungu-chelewa
Ukungu chelewa kwenye nyanya

Njia za kudhibiti
Nyanya zilizoambukizwa huweza kushambuliwa kwa haraka na kuteketezwa na ukungu chelewa. Kuzuia ugonjwa huu ni shida sana ukishajiimarisha shambani. Njia muhimu sana ya kuzuia ukungu chelewa ni kuhakikisha haijajiimarisha na kusambaa. Hii inaweza kufanyika kwa kutumia mbinu zifuatazo:

Mbinu bora za kilimo
•Crop rotation: Zungusha mazao mengine kwa miaka 3 hadi 4
•Tumia aina zenye kustahamili ugonjwa huu (km. Meru, Tengeru 97 na Shengena)
•Tumia mbegu safi
•Ondoa mabaki ya mazao na choma moto mimea iliyoathirika na mabaki ya mimea
•Tumia moto au mvuke kuua vimelea katika maeneo yaliyoathirika
•Weka matandazo ya nyasi kuzuia kurukia kwa maji
•Tumia zana safi baina ya mashamba
•Hakikisha maji hayatuami na kuwe na mzunguko mzuri wa hewa
•Toa majani ya chini yaliyoathirika kusaidia mzunguko mzuri wa hewa
•Hakikisha kupanda kwa nafasi inayotakiwa

Dawa (Chemical control)
Ukungu chelewa unaweza kudhibitiwa kwa kutumia dawa za ukungu za aina ya mrututu (Champ Dry Prill, Champ Formula 2, Copper-Count-N, Kocide 101, kocide DF, Kocide 4.5LF, Kocide 3000, Kocide 6000), Cholorothalolin na Cholorothalonil Mixtures (Bravo 720/Echo 720, Bravo Ultrex/Echo 90DF, Bravo Weather Stik, Echo Zn, Ridomil gold/Bravo), EBDC, Copper EBDC/ Zoxamide (Cuprofix MZ Disperss, Dithane, Gavel, Maneb 75 DF, Manex, Mankocide, Manzate F1, Penncozeb 80W, Penncozeb 75DF), Famoxadone + Cymoxanil (Tanos, Fenamidone, eason 500SC) Strobilurin na Strobilurin Mixtures ( Cabrio Flint Quadris).
Kibaiolojia (Biological control)
Mpaka hivi sasa hakuna dawa ya kibaiolojia inayo weza kudhibiti/kuzuia ukungu chelewa.

2. Bakadoa: Bacterial spot >Madoa ya majani kutokana na bakteria< (Xanthomonas spp.)
Dalili
Dalili bayana zaidi huonekana kwenye majani, ndio maana ya hilo jina ‘Madoa ya majani kutokana na bakteria’. Makovu madogo ya rangi ya manjano-kijani hujitokeza kwenye majani machanga na matokeo yake ni majani yaliyopindapinda, yaliyokoza, yaliyotota na yenye kuonesha ishara kama yenye mafuta kwenye majani yaliyokomaa.
Makovu hukua haraka na yanaweza kufikia ukubwa wa 0.25-0.5 sm, huwa na rangi ya kahawia/nyekundu. Umbo la makovu kwa kawaida huwa na pembe kwa vile hufuata umbile la mishipa midogo ya majani. Makovu mara nyingi hutokea kwenye ncha na pembezoni mwa jani ambamo unyevu huhifadhiwa. Katika hali ya ujoto/ukavu, majani huonekana yamechanika chanika kutokana na maeneo ya pembezoni mwa majani na kati ya makovu hukauka na kukatika. Ukubwa wa makovu huongezeka kutokana na muda ambao majani yanakuwa na maji. 

nyanya-iliyoathiriwa-na-ugonjwa-wa-bakadoa
Athari za ugonjwa wa bakadoa

Kwenye matunda, madoa huanza kwa kuwa na rangi ya kijani kibichi na kuonyesha sehemu kama zilizotota maji. Kwa kawaida hufikia ukubwa wa 0.5 sm. Madoa haya hatimaye huwa yenye mnyanyuko, rangi ya kahawia na yenye kukwaruza kwenye tunda la nyanya. Madoa haya kawaida hufanya njia za kupenya aina nyengine za ukungu na bakteria wavamizi na kusababisha kuoza kwa matunda.

Njia za kudhibiti
Madoa ya majani yanayosababishwa na bakteria yakishaingia tu shambani au kwenye jengo la kuoteshea mimea ni vigumu kuyadhibiti. Mbinu zifuatazo zinaweza kuchukuliwa kudhibiti ugonjwa huu:

Mbinu bora za kilimo
•Mbegu zisizo na vimelea vya magonjwa
•Miche isiyo na magonjwa
•Mzunguko wa mazao
•Epuka maeneo yaliyopandwa nyanya kwa muda wa mwaka mmoja
•Tumia miche iliyopasishwa
•Ondosha shambani na choma moto mabaki ya mimea iliyoathirika na masalio
•Safisha na kuua vimelea vya magonjwa katika vitalu kabla ya kusia mbegu

Matumizi ya kemikali
Madoa yanayosababishwa na bakteria yanaweza kudhibitiwa kwa kutumia kemikali zifuatazo; Acibenzolar (Actigard 50WG) Copper fungicides (Champ Dry prill, Champ Formula 2, Copper-Count-N, Cuprofix MZ Disperss, Kocide, Kocide DF, Nordox, Tofix Dispress Basic Copper) Copper/ EBDC/Zoxamide Mixtures, Cuprof ix Dispress MZ, Gavel, Mankocide) Famoxadone/Cymoxanil (Tanos) na Streptomycin (Agri-strep).

Kibaiolojia (Biological control)
Virusi vinavyoshambulia bakteria hudhibiti magonjwa haya, lakini ni lazima viwekwe shambani wakati wa jioni angalau mara mbili kwa wiki. Bakteria wa jamii ya Xanthomonas ambao hawasababishi magonjwa hutoa udhibiti wa kiasi wa madoa yanayosababishwa na bakteria.

3. Mnyauko bakteria: Bacterial wilt 
(Ralstonia solanacearum, Pseudomonas solanacearum)
Dalili
Dalili za awali ni kunyauka kwa majani ya kwenye ncha. Baada ya siku mbili dalili hii huwa ni ya kudumu, na mti wote hunyauka na kufa kutokana na kuendelea kwa ugonjwa. Matawi yote hunyauka kwa wakati mmoja. Shina la mti ulionyauka likikatwa shehemu ya kati huwa na rangi nyeusi na huonekana kama iliyotota maji. Shina linapokamuliwa, hutoa maji ya utelezi kijivujivu unaotiririka. 
Hatua zinazofuata za ugonjwa huu ni kuoza kwa sehemu ya kati ya shina na hii husababisha uwazi katika sehemu hiyo. Mzizi ulioathirika huoza na kuwa na rangi ya kahawia mpaka nyeusi. 
Mmea-umenyauka-kwa-sababu-ya-ugonjwa-wa-mnyauko-bakteria

Mnyauko wa bakteria hausasababishi madoa kwenye matunda. Mmea hunyauka ukiwa na rangi ya kijani, (majani hayawi ya njano au kuwa na madoa) na inaweza kutokea ghafla. Katika hali ya ugonjwa kusambaa taratibu, mti hutoa mizizi mingi juu ya shina na mmea hudumaa. Kuanguka kabisa kwa mmea hutokea wakati nyuzi joto zinapofikia 320C au juu ya hapo.

Njia za kudhibiti
Mnyauko unaosababishwa na bakteria unaweza kutambuliwa shambani kwa kukata sehemu ya chini ya shina urefu wa 2-3 sm na kuisimamisha kwenye glasi ya maji. Ikiwa ugonjwa upo, basi michirizi ya bakteria kama nyuzi hutoka kwenye kipande hicho cha shina sekunde chache tu baada ya kukisimamisha kwenye maji.

Mbinu bora za kilimo
•Mzunguko wa mazao na yale ambayo hayaathiriki
•Usipande nyanya katika udongo ambao ugonjwa huu uliwahi kuwemo
•Tumia aina za mbegu zenye kustahimili/zisizopata ugonjwa wa mnyauko bakteria. (Kama vile Fortune Maker, Kenton na Taiwan F1)
•Toa na angamiza mimea iliyonyauka kutoka shambani kupunguza usambaaji wa maradhi
•Ruhusu mafuriko yenye kuenea
•Ongezea mbolea ya samadi
•Panda katika msimu ambao si rafiki kwa ugonjwa huu
•Zuia minyoo fundo (root-knot nematodes) kwani husaidia uingiaji wa ugonjwa
•Changanya na mazao jamii ya kunde
•Epuka kutumia ardhi kwa miaka 3-4 baada ya uzalishaji wa nyanya

Dawa (Chemical control)
Mnyauko wa Bacteria unaweza kudhibitiwa kwa kutumia Chlorothalonil (Bravo 720/Ensign, Bravo Ultrex, Bravo Weather Stik, Echo 720, Echo 90DF, Echo Zn, Ridomil/Bravo). Juu ya hivyo, tahadhari inapaswa ichukuliwe kuepuka usugu wa vimelea vya ugonjwa, hivyo mbinu ya matumizi ya kemikali katika kuzuia ugonjwa inabidi ichanganye na mbinu nyinginezo.

Kibaiolojia (Biological control)
Kuzuia kunyauka kunakosababishwa na bakteria kunajumuisha matumizi ya ardhi zenye kuzuia ugonjwa na ardhi zenye vimelea wapinzani (km. Candida ethanolica, Pythium oligandrum).

4. Makovu bakteria (Bacterial canker)
Ugonjwa huenezwa na vimelea vya bacteria vinavyoishi kwenye mbegu na hewani. Hutokea zaidi wakati wa masika. Majani hukauka nchani na makovu yaliyodidimia hutokea kwenye shina. Matunda huwa na makovu yenye rangi ya kahawia sehemu ya katikati.
Njia za kudhibiti
· Tumia mbegu bora na safi
· Teketeza masalia ya mazao
· Tumia mzunguko wa mazao

5. Mnyauko Fusari: Fusium wilt
(Fusarium oxysporum)
Dalili
Dalili zinajumuisha majani ya chini kuwa na rangi ya njano. Majani yaliyoathirika hukatika kwa urahisi kutoka kwenye shina na wakati mwingine hukauka kabla ya kubainika mnyauko. Tawi moja au mawili huonesha ishara. Majani machanga ya upande mmoja wa tawi huonesha dalili za kuathirika wakati upande wa pili hauneshi dalili zozote. Matawi na vipande vya matawi vikikatwa katikati huonesha rangi ya kahawia katika sehemu za kusafirishia maji.

Majani-ya-nyanya-yaliyogeuka-rangi-kutokana-na-mnyauko-fusari
6. Mnyauko Vetisili: Verticillium wilt 
(Verticillium spp.)
Dalili
Dalili hujitokeza kwenye majani yaliyokomaa na baadaye kwenye majani machanga. Majani yaliyoathirika hugeuka manjano, hukatika kwa urahisi kutoka kwenye tawi na wakati mwingine hukauka kabla kunyauka hakujajionesha. Ncha za matawi hunyauka wakati wa mchana. Wakati kupukutika kwa majani kukiendelea, majani ya juu hujikunja kwa kuelekea juu lakini hubaki hai.
Nyanya-zilivyokauka-kutokana-na-mnyauko-vetisili
Mnyauko vetisili kwenye nyanya

Njia za kudhibiti
Vyote, mnyauko ‘Fusari’ na ‘Vetisili’ hubaki kwenye udongo kwa miaka mingi. Njia za kudhibiti magonjwa haya hujumuisha yafuatayo:
Mbinu bora za kilimo
•Crop rotation: Mzunguko mrefu wa mazao (miaka 4-5) na mazao yanayostahimili magonjwa haya
•Tumia mbegu safi na zenye afya
•Lima kwa kuchimba zaidi
•Pandisha PH kwa kutumia chokaa au samadi katika ardhi zenye kiwango kikubwa cha tindikali
•Usipande nyanya katika ardhi ambayo mnyauko kutokana na Ukungu ulikuwepo
•Tumia mbegu zinazostahimili mnyauko unaotokana na Ukungu (km. Diego, Duke, Floridade, Fanny, Fortune Maker, Napoli, Radja, Roma VF, Roma VFN na Tengeru 97)
•Ondoa na teketeza mimea iliyoathirika, kuzuia usambaaji wa maradhi
•Mwagilia
•Dhibiti minyoo fundo, kwani hawa wanarahisisha na kuruhusu uingiaji wa maradhi haya ya kunyauka

Dawa (chemical control)
Mnyauko Fusari unaweza kudhibitiwa kwa kutumia Methyl bromide, Methyl bromide/Chloropicrin. Thiophanate-methyl, Streptomyces griseoviridis and Iprodione. Mnyauko Vetisili unaweza kudhibitiwa kwa kutumia Methyl bromide/Chrolopicrin.
Kibaiolojia (Biological control)
Dawa itokanayo na ukungu Mycostop husaidia kudhibiti mnyauko unaosababishwa ‘Fusarium’.

7. Rasta: Yellow leaf curl
Ugonjwa huu husababishwa na virusi na huenezwa na nzi wadogo weupe. Hutokea zaidi wakati wa kiangazi. Mimea hudumaa na majani yaliyoshambuliwa huwa na rangi ya manjano na pengine rangi ya zambarau. Nyanya hupasuka.
 Jinsi ya kudhibiti
· Nyunyiza dawa za sumu za kuua wadudu (Selecron, Dursburn, Actelic)
· Ng’oa mimea yenye ugonjwa
· Tumia mzunguko wa mazao
· Weka shamba katika hali ya usafi

8. Batobato: Tomato mosaic virus (ToMV)
Ugonjwa husababishwa na virusi na hueezwa na mbegu na kugusana. Majani huwa na mchanganyiko wa rangi hasa kijani kibichi na kijani kilichofifia (majano). Majani hujikunja na manjani machanga huwa na maumbile yasiyo kawaida. Ukifikisha jani huwa linavinjikavunjika.

Majani-ya-nyanya-yalivyojikunja-kutokana-na-ugonjwa-wa-batobato
Ugonjwa wa batobato 

Jinsi ya kudhibiti
· Tumia mbegu bora na safi
· Ng’oa mimea iliyoshambuliwa
· Teketeza masalia ya mazao
· Weka shamba katika hali ya usafi

9. Virusi mosaic vya tumbaku, matango na Virus jani vya nyanya
Dalili
Dalili zinajumuisha rangi rangi, kuwa manjano, vichungu, mabaka, rangi za kahawia, kudumaa, kukunjika kwa majani, nafasi fupi baina ya vifundo, majani membamba. Mazao duni, kuchelewa kuiva kwa matunda, rangi isiyo sawasawa ya matunda ni matokeo ya mashambulizi. Dalili zinategemea sana umri wa mmea ulioshambuliwa, hali ya mazingira, aina au jamii ya virusi na jamii ya virusi vyote vilivyopo. Aina ya nyanya pia inachangia aina za dalili zinazojitokeza.

Njia za kudhibiti
‘Tobacco mosaic virus’ na ‘tomato leaf curl virus’ huendelea kuwepo sana na husambaa kirahisi na kwa haraka, wakati ‘cucumber mosaic virus’ haiendelei kuwepo sana na usambaaji wake ni mdogo kuliko ‘tobacco mosaic virus’. Virusi husambazwa kutoka mimea iliyoathirika na kwenda kwenye mimea yenye afya kupitia kufyonza kwa nzi weupe na ‘thrips’.

Mbinu bora za kilimo
•Panda aina asilia zenye kuzuia.
•Hifadhi miche isigusane na wadudu kwa kutumia chandarua.
•Epuka kupandikiza kwenye ardhi zenye mimea iliyoathirika.
•Ng’oa mimea iliyoathirika na choma moto mabaki ya mazao.
•Fanya mzunguko wa mazao na mimea yenye kustahimili.
•Epuka kuvuta sigara wakati wa kuhudumia nyanya.
•Safisha mikono na zana kwa kutumia dawa za kuua vimelea vya magonjwa.
•Epuka kwenda kwenye mashamba safi baada ya kutoka kwenye mashamba yaliyoathirika.
•Virusi husitishwa kasi ya mashambulizi yake kwa wafanyakazi shambani kutia mikono yao ndani ya maziwa kabla ya kupanda.

Dawa (Chemical control)
Mpaka hivi sasa hakuna kemikali inayozuia mimea isipate mashambulizi ya virusi. Dawa za kuulia wadudu zinadhibiti wadudu lakini thrips ni taabu kuwadhibiti.

Kibaiolojia (Biological control)
Mpaka hivi sasa hakuna viumbe vinavyoweza kudhibiti virusi kwenye sehemu za mimea. Viumbe vya kudhibiti nzi weupe na vidukari kanda mbili vinafanyiwa uchunguzi.

10. Ugonjwa wa ukoma wa nyanya
Huu ni ugonjwa wa virus unao enezwa na nzi mweupe. Inzi hawa hushambulia zaidi nyanya wakati wa kiangazi, hasa kipindi cha joto kali.
 Dalili
• Majani machanga hujikunja na baadaye majani yote.
• Kupungua kwa utoaji maua na matunda na hata yakitokea matunda huwa ni madogo.
• Mmea kudumaa na kutozaa kabisa.

Njia za kudhibiti
Mbinu madhubuti ni kupunguza kuenea kwa ugonjwa huu kwenye shamba kwa kudhibiti kuzaana na kuenea kwa mdudu (inzi mweupe) kama tulivyo ona katika kupambana na mdudu huyo, yaani:
• Kuondoa mimea michache iliyo shikwa na ugonjwa maana wadudu hawa wanachukua ugonjwa huu kutoka mimea hii.
• Kutumia mbegu zilizo hakikishwa kuwa zinaweza kuvumilia ugonjwa huu na kutoa mavuno mazuri.
• Usilime nyanya karibu na eneo lililo na mazao kama bamia, mipapai maana mimea hii huhifadhi inzi mweupe
• Kuua inzi weupe wanaofyonza nyanya na kusambaza virusi kwa kutumia madawa. Tumia madawa kama vile Selecron, Decis, Karate n.k.
• Epuka kuchanganya zao la nyanya na mazao mengine yanayohifadhi hawa nzi kama vile mipapai na bamia.
• Ng’oa na kuchoma moto mimea yote iliyougua ugonjwa huu.

11. Ugonjwa wa mmea wa nyanya kuoza sehemu ya shina inayogusa udongo na mmea kunyauka kama vile umekosa maji
• Wadudu wanaosabisha ugonjwa huu hupatikana ardhini.
• Hakuna dawa ya kutibu ugonjwa huu baada ya dalili kujitokeza.
• Kupiga madawa za viwandani ardhini kabla ya kupanda nyanya husaidia kupungu wadudu wa ugonjwa.
• Epuka kupanda nyanya au mazao jamii ya nyanya katika eneo moja kwa muda mrefu mfulilizo. Baadhi ya mazao yanayohusiana na nyanya ni bilinganya, pilipili, ngogwe, mnavu, n.k.

12. Ugonjwa wa miche michanga ya nyanya kuoza sehemu ya shina inayogusa udongo na kufa ghafla
Ugonjwa huu hushambulia miche kitaluni na husabishwa na wadudu waishio ardhini. Mara baada ya dalili, ugonjwa huu hauna dawa ila unaweza kukingwa kwa kutumia njia zifuatazo:
• Choma moto udongo wa kutengezea kitalu kabla ya kupanda mbegu zako. Kutumia mboji husaidia kukinga miche dhidi ya ugonjwa huu.
• Epuka kumwagilia maji kupita kiasi na kutumia kuvuli kizito.

13. Matunda ya nyanya kuoza kitako
Huu ni ugonjwa unaosababishwa na:
• Umwagiliaji wa nyanya bustanini usio na mpangilio maalumu. Mfano, kumwagilia mimea maji mengi kasha kuiacha bila maji kwa siku kadhaa.
• Upungufu wa virutubisho aina ya chokaa. Dalili zake ni matunda ya nyanya kuoza sehemu ya kitako na kuonyesha rangi nyeusi.

Njia za kudhibiti
Kuzuia ugonjwa huu, zingatia kuwa na utaratibu mzuri wa kumwagilia maji ambao haubadiliki ovyo kiratiba na kiasi cha maji yanayowekwa. Rutubisha mimea kwa madini ya chokaa kwa kutumia mbolea aina ya CAN zenye madini haya.
Haya ni baadhi tu magonjwa ambayo kwa kiasi kikubwa yanahatarisha mavuno ya nyanya, je kuna ugonjwa mwingine umekutana nao shambani kwako na hatuja ueleza hapa? je unafahamu njia nyingine ya kudhibiti ugonjwa wowote uliotajwa hapa? Tafadhali tufahamishe kwa kuweka comment yako hapa chini.

YAFAHAMUMAGONJWA HATARI YA NYANYA NA DAWA ZAKE YAFAHAMUMAGONJWA HATARI YA NYANYA NA DAWA ZAKE Reviewed by BENSON on March 10, 2018 Rating: 5

No comments