KANUNI BORA ZA UFUGAJI WA MBUZI WA MAZIWA.

Watu wengi hutegemea mifugo kwa riziki lakini hawafugi katika misingi inayotakiwa ili kupata tija zaidi. Ufugaji wa wanyama humpa mkulima nyama na maziwa kwa matumizi ya nyumbani na mapato kutokana na mauzo ya ziada.

Ama mifugo pia ni chanzo cha samadi. Bidhaa zingine za wanyama zinazoweza kuuzwa ili kupata pesa zinajumulisha ngozi, samadi ya kuongeza rutuba kwenye ardhi ya kupanda mimea na pia kutoa kawi ya biogas, pembe, kwato na midomo ya ndege ambavyo hutumika katika viwanda kuzalisha bidhaa zingine.

Zipo aina nyingi ya wanyama ambao mkulima anaweza kuwafuga kuanzia ng’ombe, mbuzi, kondoo, ngamia, sungura, nguruwe na vile vile ndege wa nyumbani kama kuku, bata bukini, bata mzinga, bata, hua (njiwa) na mbuni.

Siku hizi pia wapo wakulima wanaofunga kware na kanga.
Chaguo la mnyama wa kufuga hutegemea mambo mengi. Hata hivyo, wakulima wengi hufuga wanyama ambao wana ujuzi wa kuwasimamia na wanawapatia mapato mazuri.

Katika Makala haya tutajifunza namna ya ufugaji bora wa mbuzi wa maziwa ambapo tutaanza kuangalia jinsi ya kuanzisha mradi huo na mambo mengine ya awali.

Mbuzi mara nyingi wanafahamika kama “ng’ombe wa maskini” kwa sababu nyingi. Kwa yeyote anayetaka kufuga mbuzi kwa ajili ya maziwa, mbuzi anaweza kuwa rahisi kumhudumia kuliko ng’ombe.

Gharama za uanzishaji wa mradi wa mbuzi wa maziwa mmoja au hata watano ni ndogo ukilinganisha na kuanzisha mradi wa ng’ombe wa maziwa. Chakula na zana za kufanyia kazi pia ni za gharama nafuu.

Kufuga ng’ombe wa maziwa kunaweza kuwa changamoto kubwa kwa mtu anayeanza ufugaji, lakini kwa mbuzi ni sawa na kutafuta mnyama mwingine rafiki zaidi ya mbwa.

Mbuzi wa maziwa humpatia mkulima maziwa kwa ajili ya familia na kuuza ili kupata fedha. Samadi ya mbuzi hutumika kurutubisha ardhi na mbuzi wenyewe wanaweza kuuzwa pia.

Kipato cha ziada kinachotokana na mazao ya mbuzi kinawawezesha wafugaji kumudu gharama za matumizi zikiwemo kulipa gharama za nyumbani kama chakula na huduma nyingine; kulipia gharama za shule kwa watoto wao ama kuwekeza katika miradi mingine kama kilimo na biashara zingine.

Kwa miaka ya karibuni serikali imekuwa ikihimiza ukulima endelevu ambao unahusisha ufugaji wa kisasa wenye tija kwa kuangalia mifugo ambayo siyo tu itakuwa fahari ya mkulima, bali inaweza kumpatia manufaa kibiashara.

Taasisi mbalimbali zimekuwa zikijitokeza kuwasaidia wakulima kwa mafunzo na kuanzisha miradi ya ufugaji wa mbuzi wa maziwa na ingawa siyo wakulima wengi waliopata mafunzo hayo ama kuanzisha miradi hiyo, lakini kwa wale wachache ambao wameanzisha miradi ya mbuzi wa maziwa, wameona faida zake.

Linapokuja suala la kufuga mbuzi wa maziwa, wengi wanapata hofu na kujiuliza maswali mengi kwamba wanahitaji ardhi yenye ukubwa gani ili kuwafuga, watawalisha nini, na namna gani ya kuwahudumia.

Lakini KILIMO BORA ni mtandao ambao uko kwa ajili ya kuwaelimisha wakulima na wafugaji, pamoja na wananchi wengine wanaotaka kuanzisha miradi ya aina hiyo, na ujasiriamali mwingine na tutakwenda hatua kwa hatua ili kila mmoja aweze kuelewa.

Ufugaji wa mbuzi wa maziwa unaweza kufanywa mahali popote, iwe mjini ama kijijini, kwa sababu mbuzi hawa, tofauti na mbuzi wa kienyeji wanaofugwa zaidi kwa ajili ya nyama, wanaweza kufugwa kwa njia ya ‘Zero Grazing’, kwamba wanaweza kufungiwa kwenye banda maalum na kulishwa.

Kanuni za ufugaji bora wa mbuzi wa maziwa
Mbuzi wa maziwa wanaweza kufugwa kwa gharama nafuu na kuishi katika mazingira magumu kama ya maradhi na ukame ikilinganishwa na ng’ombe.

Kutokana na umbile lao dogo wanaweza kufugwa katika eneo dogo na pia wanaweza kuhudumiwa na familia yenye nguvu kazi na kipato kidogo. Uzao wa muda mfupi unamwezesha mfugaji kupata mbuzi wengi kwa kipindi kifupi.

Wanyama hao hufugwa kwa ajili ya nyama, maziwa, ngozi, na mazao mengine kwa matumizi ya familia na kuongeza kipato.

Hata hivyo, ufugaji bora wa mbuzi wa maziwa lazima uzingatie kanuni zifuatazo:-
1) Wafugwe kwenye banda au zizi bora
2) Wachaguliwe kutokana na sifa za koo/aina na lengo la uzalishaji (nyama, maziwa au vyote kwa pamoja)
3) Wapatiwe lishe sahihi kulingana na umri na mahitaji ya mwili
4) Kuzingatia mbinu za kudhibiti magonjwa kama inavyoshauriwa na wataam wa mifugo
5) Kuweka na kutunza kumbukumbu sahihi za uzalishaji
6) Kuzalisha nyama au maziwa yenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko
Ziko faida nyingi za ufugaji wa mbuzi wa maziwa na miongoni mwazo ni:

Lishe bora
Maziwa ya mbuzi ni mazuri kwa afya na yana ladha nzuri mno kuliko ya ng’ombe! Pia maziwa hayo yana protini nyingi kuliko maziwa ya ng’ombe. Ni mazuri kwa lishe, rahisi kunywewa na yana viinilishe vingi kwa sababu yana madini mengi ya kalsiumu, fosforasi na klorine kuliko maziwa ya ng’ombe.

Kwa kuwa makala haya hayajalenga kueleza umuhimu wa madini hayo katika mwili wa binadamu, hatutaweza kujadili bali tutajadili katika makala nyingine, hata hivyo, ieleweke kwamba, maziwa ya mbuzi yana uwezo mkubwa wa kuongeza kinga katika mwili (immune) kwa watoto na hata watu wazima.

Wapo watu hawawezi kunywa maziwa ya ng’ombe kwa sababu wana mzio (allergy), lakini hakuna anayeweza kushindwa kunywa maziwa ya mbuzi.

Kama unafuga ng’ombe wa maziwa na mbuzi wa maziwa, nakushauri maziwa ya mbuzi uyatumie nyumbani halafu ya ng’ombe ndiyo uyauze. Lakini kama unao mbuzi wengi ama wanazalisha maziwa ya ziada, bado unaweza kuyauza ambapo bei yake ni zaidi ya mara mbili kwa ile ya maziwa ya ng’ombe.

Nyama ya mbuzi ni tamu sana na inaliwa na watu wengi. Lakini mbali ya maziwa na nyama, wafugaji wengi wa mbuzi wa maziwa wana faida kubwa ya kutengeneza mtindi pamoja na siagi, mazao ambayo yana soko kubwa. Kimsingi, maziwa ya mbuzi yana mafuta mengi hivyo ni rahisi kupata siagi nyingi zaidi.

Kiuchumi
Mbuzi wana gharama ndogo sana ya chakula kulinganisha na ng’ombe. Ng’ombe mmoja anaweza kula chakula kinachowatosha mbuzi watatu mpaka sita kwa siku, kutegemeana na aina (breed) na mahitaji ya mbuzi husika.

Mbuzi wanaweza kula nyasi, magamba ya miti na kadhalika, vyakula vingine ambavyo ng’ombe hawezi kula. Mbuzi wanazaa mara mbili kwa mwaka wakati ng’ombe anazaa mara moja. Ukipata bahati ya mbuzi wanaozaa mapacha, unaweza kuongeza mifugo ndani ya muda mfupi.

Kwa kawaida, mbuzi hubeba mimba kwa muda wa wiki 20 au miezi mitano (siku 150) na hunyonyesha kwa miezi miwili. Kumbuka pia mbuzi pia ni wastaarabu kuliko ng’ombe.

Ukiwa mfugaji wa maziwa huna haja ya kuhofia kuhusu uchakataji wa maziwa yako ili utoe siagi, jibini na samli, kwa sababu soko la uhakika la maziwa lipo, tena kubwa hapa Tanzania.

Nchini Kenya, kwa mfano, wakati lita moja ya maziwa ya ng’ombe inauzwa kwa KShs. 40 (takriban Shs. 800 ya Tanzania), maziwa ya mbuzi yanauzwa katika KShs. 80 na 100 (TShs. 1,600 na 2,000) kwa lita.

Kuhusu kiasi cha maziwa unayopata kila siku, mbuzi hawako nyuma sana ya ng’ombe. Wakati ambapo ng’ombe aliyetunzwa vizuri anaweza kutoa mpaka lita 15 au 20 kwa siku, mbuzi wa maziwa wa uzao bora anaweza kutoa mpaka lita 7 kwa siku na katika nchi ambayo mbuzi wa kienyeji wanaweza kutoa lita 2 kwa siku, hii ni faida kubwa kuwa na mbuzi wa maziwa.

Kwa maana nyingine, kuwa na mbuzi watatu ni sawa na kuwa na ng’ombe mmoja, jambo ambalo ni la faida pia, kwa sababu ikitokea ugonjwa ng’ombe huyo mmoja anaweza kufa, lakini mbuzi watatu hawawezi kufa wote, unaweza kuwaokoa wengine, hivyo kuendelea kuwa na maziwa.
Kwa upande mwingine, mbuzi wanahitaji usimamizi mdogo kuliko ng’ombe.


ITAENDELEA……………
KANUNI BORA ZA UFUGAJI WA MBUZI WA MAZIWA. KANUNI BORA ZA UFUGAJI WA MBUZI WA MAZIWA. Reviewed by BENSON on September 21, 2017 Rating: 5

No comments