KANUNI BORA ZA UFUGAJI WA MBUZI WA MAZIWA Sehemu Ya 02
Siku ya jana tulianza somo letu la Kanuni za kuzingatia katika ugugaji wa mbuzi hivyo siku ya leo naomba tuendelee na mfululizo wa somo hilo.
Mambo muhimu ya kuzingatia kuhusu
ufugaji wa mbuzi wa maziwa
Kama nilivyokwishaeleza siku ya jana, maziwa ya mbuzi ni mazuri na yana madini muhimu
kwenye mwili hivyo basi kila mmoja anapaswa kujifunza kuyatumia.
Maziwa ni chakula muhimu chenye madini
muhimu mwilini na pia ndiyo njia mojawapo ambayo watu huambukizwa magonjwa
haswa kwa kupuuza mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa.
Lakini lazima ifahamike kwamba, ufugaji
wa mbuzi wa maziwa ni uwekezaji mzuri hasa kwa wakulima wenye mashamba madogo
na hata yule mkazi wa mjini ambaye anaweza kulitumia eneo lake la uwani kufuga.
Ifahamike pia kwamba, ukulima ni sawa
na biashara na biashara nzuri lazima iwe na mpangilio mzuri hasa kwa matumizi
ya pesa zinazoapatikana. Kabla ya kuanzisha mradi wa ufugaji wa mbuzi wa
maziwa, lazima uwe na mpango mzuri hata kama unaanza na mbuzi wawili, kwani kwa
kufanya hivyo utaweza kujua gharama zake na hiyo itakusaidia pia hata kuongeza
mbuzi wengine na kupanua mradi.
Mpango wako wa mradi ndio pia utatoa
taswira ya matumizi ya fedha kwa sababu kama hutakuwa na matumizi mazuri ya
pesa hizo huenda iwe vigumu kununua vitu muhimu ili kuendeleza biashara hiyo.
Kwa maana hivyo, hata baada ya
kuanzisha mradi huo, ni vyema ukumbuke kuweka rekodi ili kujua ikiwa unapata
faida au hasara na ili kuweza kubaini matatizo yanayoikumba biashara yako.
Ufugaji wa mbuzi wa maziwa ni mradi
unaoweza kuanzishwa katika vikundi, lakini pia unaweza kuanzishwa na mtu mmmoja
mmoja.
Wakulima hao ni lazima waunde vikundi
au vyama ambavyo watafaidika navyo na pia vitasaidia kupigania kupata bei nzuri
ya bidhaa zao pamoja uimarishaji wa sera za serikali ili kuwawezesha kufanya
biashara yao chini ya usaidizi mzuri kutoka kwa serikali.
Tanzania ni mojawapo ya nchi zilizo na
maofisa kilimo na mifugo (maofisa ugani) waliohitimu vizuri lakini wananchi
wengi huwa hawawatumii maofisa hawa ipasavo ambao kazi yao kuu ni kukuhudumia.
Ukitaka kufuga vizuri utafanikiwa ikiwa utatafuta msaada na ushauri kutoka kwa
maofisa hao wa serikali walio kwenye eneo lako.
Maswali ya msingi yanayoulizwa na watu
wengi:
Kwa wastani, mbuzi anaweza kutoa lita
800 kwa mwaka. Hata hivyo, kiasi hiki hutofautiana kutegemeana na aina ya
mbuzi, lakini hii inamaanisha kwamba, anaweza kutoa lita kuanzia lita 2 hadi 7
kwa siku. Hii inategemea aina ya mbuzi, namna ya utunzaji na chakula
unachomlisha. Kwa matumizi ya nyumbani tu, kiasi hicho ni kikubwa kwa siku.
Kumbuka kwamba, mbuzi anakamuliwa kwa
kipindi cha miezi 10 kwa mwaka na wanaachwa kwa miezi miwili ili kuwapa nafasi
ya kuzaa tena. Mbuzi hutoa maziwa mengi baada ya kuzaa (kitaalam wanasema
‘kidding’). Ukiwa na mbuzi mmoja au wawili, huwezi kukosa maziwa kwa mwaka
mzima.
Ladha ya maziwa ya mbuzi ikoje? Ni
matamu kuliko ya ng’ombe?
Kama nilivyoeleza hapo awali, maziwa ya
mbuzi yana ladha nzuri ingawa katika mazingira mengi, ni wachache ambao
wanaweza kutofautisha. Maziwa ya mbuzi ni meupe sana.
Mbuzi pia wanatofautiana kutokana na
aina, ambapo mbuzi aina ya Nubian maziwa yao yana mafuta mengi
kuliko mbuzi aina ya Saanen kama ilivyo kwa ng’ombe aina ya
Jerseys na Holsteins. Lakini kuna mambo mengine yanayochangia maziwa kuwa na
mafuta mengi au kutokuwa na mafuta, kama uachishaji wa unyonyeshaji na
ulishaji.
Inagharimu kiasi gani kufuga mbuzi wa
maziwa?
Hii inatofautiana kila mwaka na kila
mahali, kutegemeana na mazingira ya upatikanaji wa chakula, na aina ya chakula
unachomlisha mbuzi huyo. Katika mazingira ya kijijini ambako unaweza
kumfungulia mbuzi akajichungia mwenyewe, gharama ni ndogo sana, pengine ni dawa
za chanjo. Mbuzi anahitaji chakula kuanzia nusu tani hadi tani mbili kwa mwaka,
kutegemeana na aina ya mbuzi, kiwango cha ubora wa chakula chenyewe, na
mazingira mengine kwa ujumla.
Mbuzi pia anahitaji chakula cha
nyongeza kama mahindi au mchanganyiko wa mahindi na ngano, pumba za nafaka na
nafaka nyinginezo. Kwa kawaida, inategemea na nini kinacholimwa kwenye eneo
husika au kinachopatikana. Mbuzi jike anahitaji chakula cha ziada ili kutoa
maziwa mengi.
Upatikanaji wa vyakula hivyo ndio
utakaoonyesha ni gharama kiasi gani unazotumia kumlisha mbuzi huyo. Suala la
gharama za tiba nalo ni muhimu.
Gharama nyingine za kuangalia ni zile
za kuanzia kama banda la mbuzi, uzio, vifaa vya kulishia na kunyweshea,
uhifadhi wa nyasi, na vifaa vya kukamulia.
Angalia, usitumie gharama kubwa, bali
unaweza kuanza na vile vinavyopatikana katika mazingira uliyopo. Usiwaze
kujenga banda la gharama wakati unaweza kutumia miti ya kawaida tu. Usinunue
chakula kama nyasi zinapatikana kwa wingi.
Sina nafasi ya kutosha, je, bado naweza
kufuga mbuzi kadhaa?
Mbuzi ni wanyama wanaofaa kufugwa
katika eneo dogo nyumbani. Mbuzi wanahitaji eneo lenye ukubwa wa futi 12 x 20
kwa kila mmoja kama unatumia mfumo wa Zero Grazing, na katika mazingira ambayo
mbuzi wanakwenda kuchunga wenyewe, wanahitaji eneo dogo. Banda linapaswa kuwa
kavu kwa sababu mbuzi siyo kama ng’ombe, hawawezi kulala kwenye tope.
Mbuzi wanaweza kuwa wanyama rafiki?
Ndiyo. Ni wanyama welevu na wenye
kujenga urafiki. Kama kuna mbuzi mkorofi, basi ujue hakutunzwa vizuri ama
alikuwa akinyanyaswa. Lakini kumbuka kwamba mbuzi ni mifugo, siyo kama mbwa.
Hupaswi kuwafunga Kamba muda wote, bali wanapokwenda kuchunga hasa kama katika
mazingira uliyopo wanaweza kuharibu mali zilizopo kwa kuwa wanapenda kucheza na
huvutiwa na vitu vingine. Jihadhari, usiegeshe gari lako jirani na banda la
mbuzi, kwa sababu wanaweza kuliharibu kwani wanaweza kupanda juu n ahata kuvunja
vioo.
Vipi kuhusu maradhi?
Mbuzi mara nyingi ni wastahimilivu wa
mazingira na magonjwa na wana matatizo machache ikiwa watatunzwa vizuri.
Kwa kawaida wana wadudu tumboni, hasa minyoo (na hawawezi kuishi bila kuwa
nao), lakini mtaalam wa mifugo anaweza kusaidia kuwatibu minyoo hiyo kwa
kuanzisha program ya kuondoa minyoo.
Ugonjwa wa Mastitis (kuvimba kwa
kiwele) mara nyingi huwakumba mbuzi wengi, lakini huo unaweza kudhibitiwa
katika suala la ukamuaji.
Kwa ujumla, kama unataka kufuga
kibiashara au una mbuzi wengi ndipo utamhitaji ofisa ugani wa mifugo, lakini
kama unao wachache, ni rahisi kuwamiliki na kukabiliana na changamoto ndogo
ndogo.
Vipi kuhusu majukumu?
Mbuzi wanatakiwa kulishwa na kunyweshwa
maji kila siku. Kama wanakamuliwa, unapaswa kuwakamua kila baada ya saa
12 – lakini hiyo haimaanishi kila mshale unapogonga, na inaweza kuwa
saa 1 asubuhi na saa 1 usiku au mchana na usiku mnene.
Unatakiwa kusafisha vizimba vyao na
kuweka matandazo mahali wanapolala.
Mbuzi wanatakiwa kupunguzwa pembe zao mapema kwa
sababu mbalimbali, mojawapo ikiwemo kuogopa wasije wakaumizana wanapocheza ama
kupigana. Pia wanatakiwa kupunguzwa kwato kila mara, kwa sababu kwao za mbuzi
wanaofugwa bandani tu hukua haraka kuliko za mbuzi wazururaji. Punguza kwato
mara moja kwa mwezi.
Nimeambiwa nyama ya mbuzi ni tamu sana,
je ni kweli?
Nyama ya mbuzi (chevon au cabrito kwa
Kiingereza) inafanana kidogo na nyama ya kondoo. Watu wengi wanaipenda kwa
sababu ni tamu, lakini kwa sababu mbuzi jike anatakiwa azae ilia toe maziwa, wengi
wanategemea kwamba atazaa dume ambaye baada ya muda ataliwa.
Ninapaswa kuwa na beberu ninapoanza
ufugaji?
Hapana, hususan kama ni mfugaji mdogo
wa mbuzi. Inaweza kuongeza gharama za uchumi bure. Ukishajifunza kuhusu aina za
mbuzi, nasaba haiwezi kuwa na umuhimu sana, kwa sababu unaweza kuamua kutumia
mabeberu kadhaa tofauti. Unaweza kukodisha bebeeru au unaweza kutumia mabwana
mifugo kupandikiza mbuzi wako.
Kuna jambo la ziada ninalopaswa kujua?
Ndiyo! Uamuzi wa kununua mbuzi
haupaswi kufanywa kwa ghafla bila uhakika. Mbuzi atachukua muda wako na
kiasi cha fedha. Atarejesha faida ikiwa utamtunza vyema. Kuna mambo mengi ya
kujifunza. Hata wataalam na wazoefu wa kufuga nao hujifunza kila siku. Mbali ya
hayo, huhitaji kuwa mtaalam ndipo uanze ufugaji wa mbuzi wa maziwa. Kwa ujumla,
hakuna njia ya uhakika ya kupata elimu na uzoefu bila mwenyewe kuanza ufugaji.
Ni wajibu wako wewe kuingia kwenye ujasiriamali huo.
KANUNI BORA ZA UFUGAJI WA MBUZI WA MAZIWA Sehemu Ya 02
Reviewed by BENSON
on
September 22, 2017
Rating:
No comments