NAMNA BORA YA KUTHIBITI MAGONJWA YA PILIPILI HOHO

Pilipili hoho yenye dalili za ugonjwa wa chule
Magonjwa ya pilipili hoho ni moja ya sababu kuu zinazoweza kusababisha hasara kubwa sana katika kilimo cha pilipili hoho. Hasara ya mpaka asilimia mia inaweza kutokea kama hatua za kuyadhibiti magonjwa ya pilipili hoho hazitachukuliwa mapema.  Kuna magonjwa ambayo huweza kusababishwa na vimelea vya magonjwa na Hitilafu (kama kuoza kitako) ambazo si magonjwa ya pilipili hoho bali hutokea tu kutokana na sababu kama vile upungufu wa virutubisho.
Hivyo ili mkulima aweze kuchukua hatua stahiki katika kukabiliana na magonjwa ni muhimu ajue ni magonjwa yepi yanasumbua sana zao hili la pilipili hoho. Yafuatayo ni magonjwa ya pilipili hoho na njia za jinsi ya kuyadhibiti;

(a) Batobato
Huu ni ugonjwa unaosababishwa na virusi unaoenezwa kwa urahisi na wadudu wanaokula kwa kufyonza utomvu wa mmea kama vile vidukari na nzi weupe.
Mmea wa pilipili hoho wenye dalili za batobato
Mmea wa pilipili hoho wenye dalili za batobato 

Dalili

Dalili za ugonjwa huu ni pamoja na kudumaa na kukunjamana kwa majani. Vilevile majani hubadilika rangi taratibu kutoka kijani, kijani kilichofifia mpaka rangi ya njano katika michirizi.

 

Udhibiti

Ugonjwa huu huweza kudhibitiwa kwa kupanda aina ya pilipili hoho zinazostahimili ugonjwa kama vile Yolo wonder na kung’oa miche inayoonyesha dalili za ugonjwa. Vilevile kufanya mzunguko wa mazao na kutumia dawa za kudhibiti wadudu wanaoeneza virusi vya ugonjwa husaidia kudhibiti ugonjwa huu. Hakikisha bustani yako ipo mbali na shamba la tumbaku au matango. Teketeza masalia yote ya mazao baada ya kuvuna.

 

(b) Chule (Anthracnose)

Huu ni ugonjwa wa ukungu unaoanzia kwenye mbegu husababishwao na fangasi (Colletotrichum spp). Ugonjwa huu huweza kushambulia zao la pilipili hoho katika hatua zote za ukuaji hata baada ya kuvuna na mara nyingi hutokea wakati bustani inapokua katika hali ya unyevu mwingi.
Pilipili hoho yenye dalili za ugonjwa wa chule
Pilipili hoho yenye dalili za ugonjwa wa chule

 

Dalili

Ugonjwa huu husababisha madoa yaliyo bonyea yenye maji ambayo baadae hutanuka na kuwa meusi yenye viduara vya kahawia.

 

Udhibiti

Hakikisha unatumia mbegu safi zisizo na maambukizi ya ugonjwa na kufanya mzunguko wa mazao. Pandikiza miche isiyo na ugonjwa shambani kwa nafasi inayopendekezwa, kuepuka msongamano na pia usimwagie maji majani ya mimea kuepuka kuongeza hali ya unyevu bustanini. Fanya mzunguko wa mazao ukiepuka mazao ya pilipili, maharage na nyanya ambayo pia hushambuliwa na ugonjwa huu. Tumia dawa za ukungu zenye viambato vya Chlorothalonil, Mancozeb na Carbendazim. Mfano wa dawa za ukungu zinazopatikana Tanzania zenye viambato hivi ni pamoja na Dithane – M45(Mancozeb), Agrothalonil 720SC (Chlorothalonil) na Elcazim 50SC (Carbendazim).

 

(c) Bakadoa (Bacterial Leaf spot)

Ugonjwa huu husababishwa na vimelea vya magonjwa aina ya bakteria (Xanthomonas campestris pv. Vesicatoria) na kuenea kwa njia ya mbegu, mvua na umande. Huweza kushambulia zao la pilipili hoho katika hatua zote za ukuaji ukishambulia majani, shina na matunda.
Dalili za ugonjwa wa baka doa katika majani na matunda ya pilipili hoho
Dalili za ugonjwa wa baka doa katika majani na matunda ya pilipili hoho

 

Dalili

Majani huanza kuwa na madoa madogo ya rangi ya njano yasiyo na umbo maalum yenye maji maji na kingo nyeupe nyembamba ambayo hubadilika taratibu na kuwa ya kahawi katikati. Ukiyatazama madoa kwa juu ya jani   huonekana yaebonyea wakati kwa chini yaeinuka. Hatua ya mwisho wa ugonjwa kwenye majani ni kupukutika kwa majani. Madoa yanapokuwa mengi majani huweza kupukutika wakati yakiwa bado na ukijani. Madoa ya kwenye matunda huonekana madogo ya duara na yaliyodidimia yenye rangi ya kahawia hadi nyeusi.

 

Udhibiti

Unaweza kuzuia ugonjwa huu kwa kupanda mbegu zilizothibitishwa na wataalam na kunyunyizia dawa zenye viambato vya Mancozeb au copper. Kwa ufanisi zaidi unaweza kuzichanganya dawa hizi katika dumu la kunyunyizia dawa kabla ya kunyunyizia mimea bustanini. Mfano wa dawa zinazopatikana Tanzania zenye viambato hivi ni pamoja na Dithane M45 (Mancozeb) na Kocide 101 (copper hydroxide). Hakikisha bustani inakuwa katika hali ya usafi wakati wote na teketeza masalia yote ya mazao baada ya kuvuna. Usimwagie maji juu ya mmea wakati wa kumwagilia.

 

(d) Bakajani (Phytophthora blight)

Huu ni ugonjwa wa ukungu unaosababishwa na Phytophthora capsici na kuenezwa na maji kwa njia ya umwagiliaji mbaya au mvua.Ugonjwa huu unaweza kuathiri sehemu zote za mmea kuanzia mizizi, shina, majani hadi matunda.
Dalili za ugonjwa wa bakajani katika majani ya pilipili hoho
Dalili za ugonjwa wa bakajani katika majani ya pilipili hoho
Dalili za ugonjwa wa bakajani kwenye tunda la pilipili hoho
Dalili za ugonjwa wa bakajani kwenye tunda la pilipili hoho

 

Dalili

Miche michanga yenye ugonjwa huu huweza kunyauka na kufa ikiwa bado kitaluni au baada ya kupandikiza shambani. Mimea mikubwa huonyesha dalili za ugonjwa huu kwa kuoza mizizi, kukauka kwa shina hasa karibu na udongo, kuoza kwa matunda na kutokea kwa mabaka kama ya kuungua kwenye majani.

 

Udhibiti

Unaweza kudhibiti ugonjwa huu kwa kutumia mbegu bora zinazostahimili ugonjwa zilizothibitishwa na wataalam, kulima kwa mzunguko wa mazao na epuka kupanda pilipili hoho kwenye sehemu inayotuamisha maji. Tumia dawa za ukungu zenye viambato vya Metalaxyl, Chlorothalonil au Mancozeb.  Mfano wa dawa zinazopatikana Tanzania zenye viambato hivi ni pamoja na Dithane M45 (Mancozeb), Fangonil (Chlorothalonil), na Ridomil (Metalaxyl & Mancozeb).

 

(e) Mnyauko fusari (Fusarium wilt)

Huu ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea vya fangasi (Fusarium oxysporum f. pv. Lycopersici) vinavyoishi kwenye udongo ambavyo hushambulia mirija ya mmea ya kupitisha maji na chakula. Ugonjwa huu hutokea sana katika maeneo yenye udongo unaotuamisha maji kama vile maeneo yenye udongo wa mfinyanzi mzito. Vilevile katika maeneo ambayo udongo wake hauifadhi maji vizuri kama udongo wa kichanga ugonjwa huu huwa ni tatizo. Zana za kilimo zisizosafishwa na masalia ya mazao yenye ugonjwa huweza kueneza ugonjwa huu.

 

Dalili

Majani ya mmea hubadilika rangi na kuwa ya njano kabla ya mmea wote kunyauka na kufa. Shina la mmea likipasuliwa ndani huonekana rangi ya kahawia.

 

Udhibiti

Unaweza kudhibiti ugonjwa huu kwa kutumia mbegu safi na bora zilizothibitishwa na wataalam, kuteketeza masalia ya mazao na kufanya mzunguko wa mazao.Usipande pilipili hoho katika shamba lenye historia ya kuwa na ugonjwa huu. Vilevile choma kitalu kabla ya kusia mbegu kuua vimelea vilivyo kwenye udongo na weka mbolea ya samadi katika shamba lenye udongo unaotuamisha maji. Nyunyizia dawa za ukungu zenye viambato vya Carbendazim na Iprodione kabla ya kuanza dalili za ugonjwa. Nyunyizia Carbendazim wakati miche ikiwa bado michanga, wakati wa kutoka maua na wakati wa kutengenezwa kwa matunda. Baadhi ya dawa zinazopatikana Tanzania zenye viambato hivi ni pamoja na Elcazim 50SC (Carbendazim) na Eprodane 500SC (Iprodione).

 

(f) Mnyauko bakteria

Ugonjwa huu husababishwa na vimelea vya bakteria (Pseudomonas solanacearum)vinavyoishi kwenye udongo ambavyo hushambulia mirija ya mmea ya kupitishia maji na chakula. Ugonjwa huu hupendelea maeneo yenye hali ya mvua nyingi na joto ambapo huweza kusababisha hasara kubwa kwa mimea karibu yote kunyauka shambani.

 

Dalili

Mmea wote hunyauka ghafla bila ya majani kubadilika rangi kuwa njano. Mmea hunyauka ukiwa na ukijani wake. Ukikata kipande cha shina la mmea na kukidumbukiza katika glasi yenye maji safi michirizi ya bakteria kama vile ya maziwa huonekana ikichuruzika kutoka katika kipande cha shina.

 

Udhibiti

Ni vigumu kuudhibiti ugonjwa huu unapoingia shambani hivyo ni vyema kuhakikisha hautengenezi mazingira rafiki yanayoweza kupelekea kutokea kwa ugonjwa. Njia kama kuchoma udongo wa kitalu kabla ya kusia mbegu, kuweka matandazo, kuosha zana za kilimo na kupumzisha shamba lenye ugonjwa kwa mwaka mmoja au miwili huweza kusaidia kudhibiti ugonjwa huu.

 

(g) Ubwili unga (Powderly mildew)

Huu ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea vya fangasi (Laveillula taurica) vinavyo shambulia mazao ya aina nyingi. Ugonjwa huu hupendelea hali ya hewa ya joto ambapo huweza kuonekana hata pale ambapo shamba linapokuwa katika hali ya ukavu. 
Jani la pilipili hoho lenye dalili za ugonjwa wa ubwili unga
Jani la pilipili hoho lenye dalili za ugonjwa wa ubwili unga

 

Dalili

Unga unga wa rangi ya kijivu cheupe huonekana chini na juu ya majani ya mmea ambapo majani yaliyokomaa huanza kushambuliwa na kufuatia majani machanga. Majani hubadilika rangi taratibu kuwa ya njano na mwishowe hufa na kupukutika.

 

Udhibiti

Njia nzuri ya kudhibiti ugonjwa huu ni kuzuia maambukizi, kuenea kwa ugonjwa na kuhakikisha bustani inapata matunzo yanayostahili. Tumia dawa za ukungu zenye viambato vya Sulphur, Tebuconazole, Hexaconazole, Triadimenol, Triadimefon, copper, Bitertanol au Azoxystrobin. Mfano wa dawa zinazopatikana Tanzania zenye viambato hivi ni pamoja na Funguran (Copper hydroxide), Bayfidan 250EC (Triadimenol), Salfarm 80 WP (Sulphur), Baycor 500SC (Bitertanol), Folicure EC 250 (Tebuconazole) na Estrobin 250 SC (Azoxystrobin). Vilevile dawa za asili zinazotokana na mafuta ya kitunguu saumu au muarobaini huweza kutumika.

 

(h) Kuanguka kwa miche (damping off)

Huu ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea vya fangasi (Rhizoctonia solani na Phytium spps) ambao hushambulia miche ikiwa bado michanga.

 

Dalili

Mbegu zenye ugonjwa hushindwa kuota na miche michanga hudumaa na kuanguka. Sehemu ya chini ya shina la mche huwa nyembamba na laini ukilinganisha na sehemu za juu.

 

Udhibiti

Njia sahihi ya kuudhibiti ugonjwa huu ni kuzuia maambukizi kwa kutumia mbegu bora na kuhakikisha miche michanga inakuwa katika mazingira rafiki. Vile-vile unaweza kuchoma nyasi juu ya kitalu kabla ya kusia mbegu au unaweza kunyunyizia dawa zenye kiambato cha Propamocarb hydrochloride katika udongo wa kitalu kabla ya kusia mbegu au shambani kabla ya kupandikiza. Mfano wa dawa zinazopatikana Tanzania zenye kiambato hiki ni pamoja na Dorado 722SL na Elpride 722SL.

HITILAFU
Kuoza kitako (Blossom end rot).
Hii ni hitilafu inayotokana na upungufu wa virutubisho vya chokaa (calcium) kwenye mmea ambapo huathiri matunda ya mmea. Kuoza kitako kunasababishwa na kiwango kidogo cha maji katika udongo na utaratibu mbaya wa umwagiliaji.
Tunda la pilipili hoho lilioza kitako
Tunda la pilipili hoho lilioza kitako

 

Dalili

Dalili za tatizo hili huonekana zaidi kwenye matunda ambapo sehemu ya chini ya tunda hubadilika rangi na kuwa ya kahawia kabla ya kuoza.

 

Udhibiti

Mwagilia bustani kiwango cha kutosha cha maji na hakikisha unakuwa na ratiba moja maalum ya umwagiliaji bila ya kubadili badili. Usiache udongo ukakauka kabisa kabla ya kumwagilia. Punguza matumizi ya mbolea za Naitrojeni bustanini hasa baada ya maua kutoka. Tumia CAN kama mbolea ya kukuzia miche bustanini na punguza majani katika mche wenye majani mengi kwa kupogolea (pruning).
Hitilafu zingine zinazoweza kuathiri zao la pilipili hoho ni pamoja na kuungua kwa matundakunakotokana na mionzi ya jua na kupasuka kwa matunda.
NAMNA BORA YA KUTHIBITI MAGONJWA YA PILIPILI HOHO NAMNA BORA YA KUTHIBITI MAGONJWA YA PILIPILI HOHO Reviewed by BENSON on April 26, 2018 Rating: 5

No comments