JINSI YA KUANDAA KITALU CHA MBOGAMBOGA
Kitalu ni nini?
Kitalu ni sehemu ambayo miche huoteshwa na kutunzwa kabla ya kupandikiza bustanini / shambani.
Ni muhimu kujua jinsi ya kuandaa na kutunza kitalu cha miche ya mboga mboga kwa sababu mazao mengi ya mbogamboga huhitaji kuanzia kitaluni ili yaweze kufanya vizuri shambani / bustanini.
Baadhi ya mazao ya mbogamboga yanayo hitaji kuanzia kitaluni ni kama vile nyanya, pilipili hoho, vitunguu, kabichi, nanasi, matango, n.k.
Tumeshajifunza namna ya kufanya kilimo cha mazao mbalimbali ya bustani lakini hatukuwahi kueleza namna ya kuandaa na kutunza kitalu cha miche inayopandikizwa bustanini, leo nimekuletea makala hii ambayo naamini itakuwezesha kujua nini cha kufanya ili ukuze miche bora utakayopandikiza kwenye shamba lako.
Aina za Vitalu vya miche ya Mbogamboga
Kuna aina tofauti za vitalu ambavyo vinaweza kutumika kukuzia miche ya mboga. Njia inayotumika na wakulima wengi wa Tanzania ni ile ya (1) kutumia udongo wa asili, yaani kuandaa tuta / jaruba la kitalu karibu na shamba / bustani. Vilevile kuna kitalu ambacho huanzia katika (2) tuta la mchanga (ulioletwa) au matrei ya plastiki na baadae miche kuhamishiwa katika viriba vyenye udongo wenye rutuba au matuta. Kitalu cha kwenye viriba hutumika sana katika kuzalisha miche ya mbogamboga kwa ajili ya kuuza.
Faida za kukuza miche Kitaluni
Kitalu ni muhimu katika kilimo cha mboga mboga kwa sababu zifuatazo;
- Ni rahisi kutunza na kuiangalia miche michanga kwa uangalifu zaidi inapokuwa kitaluni kuliko inapokuwa shambani.
- Kupanda mbegu kwenye kitalu humpatia mkulima nafasi ya kuchagua miche mizuri yenye afya kwa ajili ya bustani yake kuliko pale anapopanda mbegu moja kwa moja shambani.
- Kitalu husaidia kuepuka matatizo kama vile ya mbegu kushindwa kuota ambayo husababisha shamba kuwa na mashimo tupu yasiyo na mimea.
- Kitalu hutumia sehemu ndogo kutunza miche ambayo huweza kupandikizwa katika eneo kubwa.
UCHAGUZI WA ENEO LA KITALU
Ni muhimu kuchagua eneo sahihi kwa ajili ya kuandaa kitalu cha mboga ili kurahisisha matunzo ya miche katika kitalu. Eneo kwa ajili ya kuandaa kitalu inashauriwa liwe na tabia zifuatazo:
- Eneo liwe na urahisi wa kupata maji ili kurahisisha umwagiliaji wa miche kitaluni.
- Eneo lisiwe tambarare sana au lenye mwinuko mkali.
- Eneo liwe na udongo mzuri wenye rutuba na usiotuamisha maji.
- Eneo liwe na mwanga wa jua wa kutosha.
- Eneo lisiwe na historia ya mashambulizi ya magonjwa na wadudu wanaoshambulia miche michanga au wanyama waharibifu kama vile panya tumbili n.k.
- Eneo lisiwe mbali sana na shamba kurahisisha uhamishaji wa miche kutoka kitaluni kwenda shambani wakati wa kupandikiza.
JINSI YA KUANDAA KITALU
Zifuatazo ni hatua za Kuandaa Kitalu cha miche ya mbogamboga
- Kusafisha eneo na kukatua
Safisha eneo la kuandalia kitalu kwa kufyeka vichaka na kuondoa magugu kisha katua udongo wa kutosha mita za mraba 10.
- Kuchoma udongo
Choma udongo wa kitalu kwa muda wa dakika 40 hadi saa moja katika pipa la bati au nyunyizia dawa katika udongo kuua vimelea na wadudu walio katika udongo. Vilevile unaweza kuchoma udongo kwa kutumia plastiki maalum jeusi (plastic mulch) au kuchoma nyasi juu ya udongo wa kitalu.
- Urutubishaji wa udongo
Rutubisha udongo kwa kuchanganya na samadi iliyoiva vizuri kiasi cha debe mbili. Ukikosa mbolea ya samadi unaweza kutumia mbolea ya kupandia aina ya DAP kwa kuweka gramu 200 ambazo unaweza kukadilia kwa kuweka maganda nane ya kiberiti yaliyo jaa mbolea. Inapendekezwa zaidi kutumia mbolea za asili kama samadi katika kitalu kuliko mbolea za viwandani. Vilevile kuharakisha ukuaji unaweza kuyunyizia mbolea ya maji aina ya booster siku kumi na nne tangu mbegu kuota.
- Kutengeneza Tuta
Tengeneza tuta la upana wa mita 1, urefu wa mita 10 hadi 12 lililoinuliwa katika kimo cha sentimita 15 na kulisawazisha vizuri. Hakikisha upana wa tuta ni mita 1 na si vinginevyo ili kurahisisha uhudumiaji.
- Kupanda / Kusia Mbegu Kitaluni
Kuna njia mbili za kusia mbegu kitaluni, nazo ni kama zifuatazo:
(i) Kupanda kwa mstari
Kupanda mbegu kwa mstari chora vifereji vyenye kina cha sm 2 mpaka 3 juu ya tuta kwa kutumia kijiti au kidole cha mkono kukata urefu wa tuta kwa nafasi ya sm 10 au sm 15 kutoka kifereji hadi kifereji kisha sia mbegu kwa kuzisambaza katika vifereji na fukia kwa udongo mwepesi.
(ii) Kupanda kwa kutawanya
Njia hii hutumika hasa kwa mbegu ambazo ni ndogo sana kama vile mbegu za mchicha ambapo mbegu huchanganywa na mchanga katika uwiano wa 1:4 kabla ya kutawanya katika tuta. Kwa mfano kikombe kimoja cha mbegu kitachanganywa na vikombe vinne vya mchanga. Kipimo chochote utakachotumia hakikisha kinafuta uwiano huu ili kuwa na mchanganyiko mzuri wa mbegu katika tuta.
- Kuweka matandazo (Mulching)
Baada ya kutengeneza tuta na kusia mbegu weka matandazo ya nyasi kwa kuyatandaza katika tuta kisha mwagilia maji ya kutosha.
Zingatia: Idadi ya vitalu itategemea idadi ya miche unayotaka kuwa kutokana na ukubwa wa eneo unalotaka kupandikiza.
NAMNA YA KUTUNZA KITALU
Baada ya kuandaa kitalu hakikisha unakitunza vizuri ili kuweza kupata miche bora ya kupandikiza shambani. Matunzo ya kitalu hujumuisha mambo yafuatayo;
- Kujengea kichanja/Kivuli (Shading)
- Umwagiliaji
- Kupiga dawa za wadudu na magonjwa
- Kupunguzia miche na
- Kuitayarishaji miche kabla ya kuipandikiza.
(a) Kujengea kichanja / Kivuli
Mbegu zitakapoota ondoa matandazo na tengeneza kichanja chenye kimo cha mita 1 kutoka ardhini kilichotandazwa nyasi au makuti kufunika kitalu. Kichanja hiki hutengenezwa ili kuipa kivuli miche ambayo bado ni michanga isije kuungua na mionzi ya jua na kushindwa kukua vizuri. Vilevile kichanja husaidia kupunguza kasi ya matone ya mvua kubwa ili miche isijeruhiwe.
(b) Umwagiliaji
Mwagilia maji kitaluni kila siku asubuhi na jioni hadi wakati wa kutayarisha miche. Ni vyema kuzingatia uwezo wa udongo kutunza maji ili kuepuka kuzidi kwa kiwango cha maji kunakoweza kupelekea kudumaa kwa miche kitaluni na kuchelewesha upandikizaji.
(c) Kupunguzia miche
Punguza miche kitaluni ili kuondoa msongamano wa miche na kubaki na miche itakayoweza kukua vizuri kwa nafasi. Hili ni muhimu hasa kwa miche yenye majani mapana kama vile miche ya nyanya na kabichi. Miche ya kabichi hupunguziwa siku nne hadi wiki moja tangu mbegu kuota wakati miche ya jamii ya nyanyahupunguziwa baada ya wiki moja tangu kuota kwa mbegu. Miche iliyopunguzwa katika tuta moja inaweza kuhamishiwa katika tuta lingine.
(d) Kupiga dawa za Wadudu na Magonjwa
Unaweza kuanza kunyunyizia dawa za ukungu na kuua wadudu wiki moja hadi mbili tangu miche kuota. Chagua dawa kulingana na wadudu waharibifu na magonjwa yanayo shambulia zao husika. Hakikisha unafuata maelekezo ya dawa husika.
(e) Kuitayarisha miche (Acclimatization)
Miche hutayarishwa ili isipate tabu kuzoea hali ngumu ya shambani na hivyo kupona haraka inapopandikizwa. Utayarishaji wa miche hufanywa kwa kupunguza matandazo ya nyasi katika kichanja polepole kuanzia wiki mbili kabla ya kupandikiza. Ondoa kivuli chote na punguza kiwango cha maji ya kumwagilia wiki moja kabla ya kupandikiza ili kuiwezesha miche kuzoea hali ya ukame.
Zingatia: Usichelewe kupandikiza miche kwa sababu miche mikubwa ni vigumu kuihamisha na mizizi yake ni mirefu hivyo inaweza kukatika kwa urahisi. Pandikiza miche ikiwa na mizizi iliyozungukwa na udongo
JINSI YA KUANDAA KITALU CHA MBOGAMBOGA
Reviewed by BENSON
on
April 27, 2018
Rating:
No comments