JINSI YA KUTENGENEZA CHAKULA CHA NGURUWE

A.    Utangulizi
Chakula bora kwa Nguruwe ni moja  ya suala muhimu sana kwenye dhana nzima ya ufugaji wa Nguruwe wenye tija na faida kwa mfugaji. Chakula cha Nguruwe kinagharimu kama asilimia sabini ya garama zote za ufugaji wa nguruwe. Kati ya matatizo mengi yanayosababisha tija na ufanisi duni wa uzalishaji wa Nguruwe yanatokana na lishe duni. Lakini kama wakipatiwa lishe bora, tija na ufanisi wa uzalishaji utakuwa mkubwa hivyo kuongeza faida kwa mfugaji.

B.       Baadhi ya faida za kulisha lishe bora kwa nguruwe
1.   Lishe bora huharakisha ukuaji wa haraka wa Nguruwe nahivyo kupata uzito unaohitajika kwa kipindi kifupi.
2.   Lishe bora hupunguza gharama za ufugaji na hivyo kuongeza faida kwa mfugaji kwa sababu nguruwe atahitaji kiasi kidogo tu cha chakula na atachukua muda mfupi kupata uzito mkubwa
3.   Lishe bora itapunguza maambukizi ya magonjwa.
4.   Lishe bora huongeza kiasi cha mayai yatakayoivishwa na mama Nguruwe na hivyo kuongeza idadi ya watoto watakaozaliwa
5.   Lishe bora huongeza kiasi cha maziwa yatakayotengenezwa na mama Nguruwe kwa ajili ya watoto hivyo kuwafanya wawe na afya bora itakayo wawezesha wakue haraka na kupunguza idadi ya vifo kwa watoto.
6.   Lishe bora inaongeza ufanisi wa madume ya Nguruwe na hivyo kuongeza uwezo wa kupanda

C.       Viini lishe muhimu kwenye lishe ya nguruwe
Nguruwe wanauwezo wa kula aina nyingi za vyakula lakini vyenye uwezo wa kumeng’enywa kwa urahisi. Chakula cha Nguruwe kilichokamilika kinahitaji kuwa na mchanganyiko wa viini lishe vitano, navyo ni
1.   Vyakula vyenye kutia nguvu mwilini (vyakula vyenye asili ya wanga) kamavile Pumba za mchele, Pumba za mahindi, Pumba za ngano, Machicha ya pombe yaliyokaushwa, Mihogo, Viazi vitamu, Viazi mviringo, Miwa, Ndizi mbichi, zilizoiva au zilizopikwa na makombo ya vyakula vya asili vya wanga n.k.
2.    Vyakula vya kujenga mwili (Vyakula vyenye asili ya protini) k.m  
Mashudu ya alizeti, mashudu ya pamba na mawese, unga wa dagaa/samaki, damu iliyokaushwa, soya n.k
3.   Vyakula vya asili ya madini Chumvi ya mezani, chokaa ya mifugo (Limestone), mifupa iliyosagwa (bone meal), madini maalum ya nguruwe (Pig mix), madini mchanganyiko (k.m. maklic), madini ya chuma (hasa kwa watoto wa nguruwe) n.k.
4.   Vyakula vya asili ya vitamini k.m Majani mabichi laini, Mbogamboga, Matunda k.m parachichi, maembe, mapapai n.k, viungo mboga kama nyanya, bilinganya n.k. Michanganyiko maalumu yenye viasilia vya vitamini k.m. Vitamini premix n.k.
5.   Maji Hii ni lishe muhimu kwenye chakula cha nguruwe, ila tofauti na viini lishe vingine vilovyotajwa hapo juu ambapo nguruwe anapewa kwa vipindi/muda na kiwango maalum, maji yanahitajika kwa nguruwe muda wote.

      Mahitaji ya maji ya kunywa kwa nguruwe ni kama ifuatavyo:-
·         Nguruwe anayenyonyesha lita 20 kwa siku
·         Nguruwe aliyeachishwa kunyonyesha lita 5 kwa siku
·          Nguruwe wanaokuzwa na kunenepeshwa wenye kilo 20 hadi 90 lita 5 kwa siku
·         Watoto wa nguruwe lita 1 kila mmoja   
      
D.        Jinsi ya kutengeneza chakula cha nguruwe
Wakati wa kutengeneza chakula cha nguruwe inabidi kuzingatia yafuatayo:
·         Mchanganyiko wako uwe na viinilishe vinne vilivyotajwa hapo mwanzo
·         Chagua aina ya viinilishe vinavyoweza kupatikana kwa urahisi na bei nafuu kwenye mazingira yako.
·         Aina ya mchanganyiko wa chakula ni muhimu uzingatie mahitaji ya nguruwe kama umri (k.m. nguruwe wanaonyonya, waliochishwa kunyonya, wanaokua, na wanaonyonyesha)

Mfano jedwali Na 1 linaonyesha michanganyiko mbalimbali ya vyakula vya nguruwe.
1.            Mchanganyiko namba 1: inapendekezwa kwa wafugaji  walioko kwenye mazingira ambayo pumba za mahindi na mashudu ya alizeti yanapatikana kwa urahisi
2.            Mchanganyiko namba 2: kwa wale ambao pumba za mahindi, za mpunga, machicha ya pombe  na mashudu ya alizeti yanapatikana kwa urahisi.
3.            Mchanganyiko namba 3: kwa wale ambao pumba  za mpunga na mahindi yanapatikana kwa urahisi.


Jedwali namba 1: Michanganyiko mbalimbali ya vyakula vya nguruwe
Na
Aina ya viinilishe
Michanganyiko
Namba 1
Namba 2
Namba 3
1
Vyakula vya wanga



1. Pumba za mahindi
70.25
32
30.00
2. Pumba laini za mpunga
-
25
33.00
3.  Machicha ya pombe
     yaliyokaushwa
-
21
-
4. Mahindi yaliyoparazwa
-
-
10.00
2
Vyakula vya protini



A. Protini ya nafaka



1. Mashudu ya alizeti
22.00
14
22.00
2.Mashudu ya michikichi
-
-

3. Soya iliyochemswa na kuparazwa
-
-
-
B. Protini ya Wanyama



4.Unga wa dagaa/samaki
4.00
2.00
3.25
5.Damu iliyokaushwa
-
2.25
-
3
Vyakula viasili vya madini




1. Chumvi ya mezani
0.50
0.50
0.50

2. Chokaa ya mifugo    
   
2.00
2.00
2.00

3.  Unga  wa mifupa
1.00
1.00
1.00

4. Madini na vitamini    
    mchanganyiko
0.25
0.25
0.25

         Jumla
100.
100
100.


E.     Kiasi na namna ya kulisha
·         Nguruwe wanahitajika kulishwa aina hii ya chakula mara mbili (asubuhi na mchana) au zaidi kwa siku
·          Kiwango/kiasi cha kulisha kwa nguruwe wa aina na rika tofauti kimeonyeshwa kwenye jedwali Namba 2
·         Pamoja na vyakula vilivyotajwa, wafugaji wanashauriwa kuwapatia nguruwe vyakula vyao vya asili kama vyakula vya ziada mfano, majani mabichi laini, majani ya maboga, mbogamboga, matunda kama maparachichi, majani ya viazi n.k.     

Jedwali na 2:  Viwango vya kulisha Nguruwe wa uzito mbalimbali
Na
Wakati
Uzito wa nguruwe (kilo)
kiasi cha chakula  (kilo kwa siku)
1.
Baada ya kuachishwa kunyonya hadi uzito kiasi
10 - 17
0.75
2.
Uzito uliozidi kiasi kidogo
18 - 29
1.00
3.
Uzito wa kawaida
30 - 40
1.50
4.
Uzito mkubwa kiasi
41 - 60
2.00
5.
Uzito mkubwa
61 - 80
2.5
6.
Uzito mkubwa sana
81 - 100
3.00


Jinsi ya kulisha makundi mbalimbali ya nguruwe

1.        Kipindi cha mamba, kuzaa hadi kuachisha kunyoyesha

Kipindi cha miezi mitatu baada ya kupandishwa
·         Apatiwe chakula kiasi k.m. kilo mbili kwa siku
·         Kiasi hiki kiendelee hadi wiki 3 kabla ya kuzaa

Wiki tatu kabla ya kuzaa
·         Ongeza chakula kufikia kilo 2½.

 Wiki moja kabla ya kuzaa
·         Anza kuopunguza chakula taratibu hasa vyakula vya nafaka (Concentrate rations).
·         Ongeza vyakula vya  mbogamboga, majani laini na matunda (laxative meals).

Siku ya kuzaa
·         Usimpe chakula chochote cha nafaka.
·         Mpe vyakula vya mbogamboga,na  vilaini kwa kiasi kidogo tu
·         Mpatie maji ya kutosha.

 Siku ya 1 – 2 baada ya kuzaa
·         Mpe ½ kilo ya chakula kamilifu.

Siku ya 3 na kuendelea
·         Ongeza chakula cha nafaka kwa kiasi cha kilo 1 kwa siku.
·         Ongeza kufikia kiwango kinachohitajika kulingana na idadi ya watoto alionao mama nguruwe.
Zingatia
·         Mama nguruwe anahitaji kilo 3 za chakula kwa matumizi yake ya kawaida.
·         Atahitaji kiasi cha theluthi moja (1/3)  ya kilo ya chakula kwa kila mtoto aliyenae
Mfano: kama mama ana watoto 9 atahitaji kiasi gani cha chakula?
Mahitaji mama peke yake
Mahitaji kutokana na watoto
Kiasi cha chakula kwa siku
3kg
Theluthi moja x 9
Kilo 6 kwa siku
                  3     +         (1/3   x  9)       =      6 Kg

·         Endelea kumpa kiwango hicho cha chakula mpaka ifikapo wiki moja kabla ya kuwaachisha watoto kunyonya.
·         Wiki moja kabla ya kuwachisha punguza kiwango taratibu mpaka kufikia kilo 3½ kwa siku.

Baada ya kuachisha kunyonya
·         Mama nguruwe apatiwe chakula bora kilicho na kiwango kikubwa chamadini na vitamini  kiwango cha kilo 2 – 3 kwa siku.
·         Hii itamsaidia kuivisha mayai, hivyo kumsaidia kupata joto mapema.

Chakula kwa ajili ya watoto wa nguruwe (Creep feed)
·         Hiki ni chakula wapewacho nguruwe wachanga wakiwa na umri wa wiki ya pili hadi wiki ya tatu.
·         Kipindi hiki mahitaji ya watoto ni makubwa ambayo hayawezi kuteshelezwa na maziwa pekee ya mama yao.
·         Chakula hiki kitawasaidia watoto kuzoea chakula kigumu, kutosheleza mahitaji yao, na hivyo huwawezesha watoto kukua kwa haraka
·         Creep feed inaweza kutengenezwa kwa kuchanganya viini lishe vifuatavyo


Aina ya  viinilishe
Asilimia

Mahindi yaliyobarazwa

30
Pumba za mahindi
40
Mashudu ya alizeti
18
Unga wa Dagaa
10
Unga  wa mifupa
0.5
Chokaa ya mifugo (limestone)
0.75
Chumvi ya mezani
0.5
Premix
0.25
Jumla
100


JINSI YA KUTENGENEZA CHAKULA CHA NGURUWE JINSI YA KUTENGENEZA CHAKULA CHA NGURUWE Reviewed by BENSON on September 04, 2017 Rating: 5

No comments