MAKOSA YANAYOFANYWA NA WAFUGAJI WENGI WA KUKU.


Kuna baadhi ya wafugaji huwa wanafuga kwa kutegemea uzoefu walionao katika ufugaji bila ya kujali kuwa kuna mabadiliko kila siku katika sekta ya mifugo, wengi wao huwa wanatatua kesi mbalimbali zinazotokea katika ufugaji kwa kutumia uzoefu hali ambayo inawasababishia kupata hasara kubwa isiyo ya lazima.

Yafuatayo ni baadhi ya mazoea yanayowagharimu wafugaji:-

1. KUINGIZA VIFARANGA BILA MAANDALIZI SAHIHI
Wengi wa wafugaji huwa wanaingiza vifaranga pasipo kufuata utaratibu wa kitaalam katika kuandaa banda pamoja na maandalizi ya kupokea vifaranga. Na kama atabahatika kufanya usafi basi atafanya juujuu tu hali ambayo inasababisha banda kuhifadhi vimelea vingi vya magonjwa na kupelekea kuku kuugua na kufa kuanzia wanaingia hadi kufikia kuuzwa, na hatimaye mfugaji hupata hasara kwani hutumia pesa nyingi kwenye madawa kwa kutibu na pesa nyingi kwenye chakula. 

2. KULISHA BILA KUFUATA MAELEKEZO SAHIHI.
Kila aina ya kuku wanautaratibu wa ulishwaji chakula, utaratibu ambao ukikiukwa huwezi kupata matokeo mazuri ya mifugo yako, ila wafugaji wengi huwa wanalisha kwa utaratibu usio sahihi ambao wao wanadhani kwamba ndio wataongeza uzalishaji wa mayai au watakuwa haraka kwa upande wa kuku wa nyama, na kuna wengine wanadiriki kutumia chakula aina moja mwanzo mwisho, yaani anaweza kutumia chakula cha vifaranga wa nyama (SUPER STARTER) kuanzia mwanzo hadi anauza kuku bila kufahamu kwamba kila aina ya chakula ina kazi yake katika kila hatua ya umri. Lakini pia bila kujali kwamba analisha kwa gharama kubwa hali ambayo itampunguzia faida.

3. KUTIBU KWA DAWA AMBAYO SI CHAGUO KWA UGONJWA HUSIKA
Kama inavyofahamika kuwa wafugaji wa kuku wengi wamebarikiwa kwa kufahamu majina mengi ya dawa za kuku, na kwa kutumia uzoefu walionao huwa wanatibu kuku wao magonjwa mbalimbali bila kupata maelekezo kutoka kwa Dokta au Mtaalamu wa mifugo. Kwa kufanya hivyo hutumia dawa nyingi tofautitofauti kwa kutibu ugonjwa mmoja bila mafanikio na kupelekea ugonjwa kuwa sugu na idadi ya vifo kuongezeka siku hadi siku.

USHAURI: Sio kila mfugaji mzoefu anaweza kuwa Daktari, ila kila Daktari anaweza kuwa mzoefu hivyo kama una tatizo lolote linalohusu masuala ya ufugaji, hususani kuku ni vyema ukamfuata daktari wa masuala ya mifugo.
MAKOSA YANAYOFANYWA NA WAFUGAJI WENGI WA KUKU. MAKOSA YANAYOFANYWA NA WAFUGAJI WENGI WA KUKU. Reviewed by BENSON on September 23, 2017 Rating: 5

No comments