MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA KATIKA KILIMO CHA ALIZETI.
Katika kuhakikisha unalima kilimo bora cha alizeti yapo
mambo muhimu ya kuzingatia na mambo hayo ni;
· Kiasi cha kilo 3 – 4 za mbegu zinatosha kupanda
eneo la ekari moja.
· Panda mbegu 3 – 4 katika kila shimo moja kwa
nafasi ya sentimita 75 kutoka mstari hadi mstari na sentimita 30
kutoka shimo hadi shimo. Shimo la mbegu liwe na kina cha sentimita 2.5 – 5.
·
Wiki mbili baada ya kuota, punguza miche katika
kila shimo na kubakiza mche mmoja.
Kiasi cha mbolea
· Mbolea zinazofaa kwa kilimo cha alizeti ni zile
za kupandia na kukuzia hasa kwenye maeneo yasiyo na rutuba.
· Wakati wa kupanda tumia nusu mfuko kwa ekari
moja ya mbolea ya kupandia na mfuko mmoja kwa ekari moja
ya mbolea ya kukuzia kwa kuigawa mbolea hiyo mara mbili. Nusu ya kwanza iwekwe
wakati wa kupanda na nusu ya
pili iwekwe wiki mbili baadaye.
· Wakati wa kuweka mbolea angalia isigusane na
mbegu au mche wa alizeti kwani huunguza.
Palizi
· Alizeti hukua taratibu katika wiki chache za
mwanzo. Hivyo unashauriwa kupalilia mapema ili kupunguza hasara.
Katika maeneo yaliyo na magugu machache, palizi moja tu inatosha. Vile vile
maeneo yenye upepo mkali, wakati
wa kupalilia inulia matuta ili kuzuia kuanguka.
Wanyama na wadudu waharibifu wa zao hili.
Ndege
Alizeti hushambuliwa sana na ndege ambao huweza kuteketeza
hadi asilimia 50 ya mazao shambani.
Kuzuia
- Usipande alizeti
karibu na msitu/pori
- Vuna mapema mazao yako mara tu kichwa kinapobadilika rangi
na kuwa manjano
- Panda alizeti kwa wingi katika shamba moja
- Amia ndege kwa mutumia sanamu, makopo na ua kuweka watu
ingawa ni gharama.
Funza wa vitumba
(American bollworm)
Funza huyu hutoboa mbegu changa kuanzia mara tu vitumba vya
maua vikifunguka mpaka karibu na
kukomaa kwa mbegu.
Kuzuia:
- Tumia dawa yo yote ya kuulia wadudu inayopatikana katika
eneo lako.
Magonjwa
Alizeti hushambuliwa na magonjwa yakiwemo madoa ya majani,
kutu, kuoza kwa mizizi, shina, kichwa na
kushambuliwa na virusi.
Kuzuia:
- Tumia kilimo cha mzunguko wa mazao
- Panda mbegu safi zilizothibitishwa na wataalamu
- Choma masalia ya msimu uliopita.
Uvunaji
Unashauriwa kuvuna alizeti mara tu inapokomaa ili kupunguza
hasara ya kushambuliwa na ndege. Alizeti
iliyokomaa kichwa hubadilika rangi toka kijani kibichi na
kuwa njano. Kata vichwa na kuvianika juani ili vikauke vizuri.
Piga piga vichwa ili kutoa mbegu za alizeti, kisha upepete na
kuendelea kuzianika ili zikauke vizuri.
Utafiti unaonyesha kuwa mkulima anaweza kupata magunia kati
ya 10 -12 kutoka katika ekari moja.
MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA KATIKA KILIMO CHA ALIZETI.
Reviewed by BENSON
on
October 03, 2017
Rating:
No comments