KILIMO BORA CHA PILIPILI HOHO
Jina la kitalaamu la pilipili hoho ni Capsicum annum. Asili ya
zao hili ni bara la Amerika ya Kusini. Kwa
hapa nchini zao hili hulimwa katika mikoa ya Iringa, Tanga (Lushoto), Mbeya,
Ruvuma, Tabora na Arusha. Hoho hutumika katika kutengeneza rangi za asili za
vyakula ambazo kwa sasa hupendwa zaidi kuliko zile zinazotokana na kemikali na
pia huongeza ladha na harufu katika vyakula. Hivyo hutumika katika viwanda vya
kusindika vyakula, kwa mapishi ya nyumbani. Lakini pia pilipili hoho Ina
virutubisho muhimu vinavyohitajika mwilini kama madini ya chuma, vitamin A na
C.
Tabia ya zao hili.
Hoho ni zao la jamii ya pilipili isiyo kali, tunda lake ni nene kiasi la duara
pia linaweza kuwa lililochongoka,.
Eneo na hali ya hewa ifaayo kwa kilimo hiki
Hoho hustawi vema katika maeneo ya usawa wa bahari hadi mwinuko wa mita 2,000
yenye mvua ya wastani wa mm.600-1,250 na wastani wa joto la nyuzi za sentigredi
21 hadi 24. Udongo wa tifitifu wenye rutuba, usiotuamisha maji na wenye hali ya
uchachu (pH) kati ya 5.0-6.5 hufaa zaidi. Lakini ikumbukwe Umwagiliaji ni
muhimu pale mvua inapokuwa chache.
Utayarishaji wa kitalu kwa jaili ya kilimo hiki.
Chagua eneo katika ardhi isiyo na mtelemko mkali na yenye rutuba ya kutosha.
Ardhi iwe imepumzishwa bila kuoteshwa mazao ya jamii ya pilipili, biringanya,
nyanya, n.k. ili kuepukana na mashambulizi ya wadudu na magonjwa.
Tayarisha kitalu kabla ya msimu wa mvua. Andaa vizuri matuta manne yenye urefu
wa wastani wa mita 10 kila moja na upana wa mita moja (1) ili kustawisha miche
inayotosha ekari moja.
Acha njia ya nusu mita kati ya tuta na tuta. Mwagilia maji ya kutosha siku moja
kabla ya kusia mbegu na endelea kunyweshea kulingana na hali ya hewa na hali ya
udongo. Sia mbegu kwenye, mstari, nafasi kati ya mstari na mstari ni sm 10 na
kina cha sm1. Kiasi cha mbegu cha nusu kilo kinatosha eneo la hekta moja. Weka
matandazo kwenye kitalu au tumia nailoni nyeusi ili kuhifadhi unyevunyevu na
kuzuia uotaji wa magugu.
Utayarishaji wa shamba kwa ajili ya kilimo hiki
Shamba lilimwe vizuri na kuweka matuta ili kuhifadhi unyevunyevu na kurahisisha
umwagiliaji. Matuta yanaweza kuwa makubwa au madogo kulingana na matakwa ya
mkulima. Matuta makubwa hupandwa mistari miwili na matuta madogo hupandwa
mstari mmoja.
Upatikanaji wa mbegu
Mbegu ambazo hutumika ni chotara ambazo huuzwa kwenye maduka ya pembejeo za
kilimo nchi nzima. Haishauriwi kutumia mbegu kutoka zao la msimu uliopita kwani
ubora wa paprika utaharibika na hivyo kuharibu soko unashauriwa kununua mbegu
bora.
Namna ya kupanda miche shambani
Mbegu huoteshwa na kukuzwa kitaluni kwa muda wa wiki 6-8 na miche hupandikizwa
shambani ikiwa na urefu wa sm.6-10. Mwagilia maji kitaluni kabla ya kuhamisha
miche. Panda shambani kwa nafasi ya sm.75-90 kati ya miche kwa sm.90-105 kati
ya mistari, wastani wa miche 12,500 itapatikana kwa hekta. Weka samadi shambani
tani 25-37 kwa hekta wiki 1-2 kabla ya kupandikiza miche, au kilo 560-670 za
NPK (mbolea ya viwandani) kwa hekta kwa uwiano wa 4:7:7 katika udongo usio na
rutuba ya kutosha.
Kuhudumia shamba
Palizi ifanyike mara magugu yanapotokea shambani. Umwagiliaji maji ufanyike
kama ilivyo kwa mazao mengine kama nyanya. Tumia mbolea kiasi cha kilo 140 za
SA au CAN kwa hekta hasa wakati mmea inapotoa matunda ili kupata matunda
makubwa na kuvuna kwa muda mrefu (hadi miezi 10).
Magonjwa na wadudu.
Wadudu
• Funza wa vitumba
• Vidukari
• Kidomozi (Leaf miner)
Kudhibiti: Tumia dawa aina ya
permethrin
Magonjwa
• Kuoza mizizi
• Mnyauko wa
majani
• Batobato
Kudhibiti: Choma nyasi kwenye kitalu
kabla ya kusia mbegu.
Badilisha mazao yasiyo ya jamii ya pilipili.
Uvunaji.
Matunda ya kwanza huwa tayari kuvunwa kuanzia miezi 2-3 baada ya
kupandikizwa; matunda yaliyokomaa vizuri na kuwa na rangi nyekundu ndiyo
huvunwa. Matunda 30-80 hupatikana kwa mmea mmoja.
Ubora wa hoho huongezeka kutegemeana na kiwango cha rangi yake ikiwa ni
nyekundu njano au kijani. Mazao kiasi cha tani 3.5 kwa hekta hupatikana. Baada
ya kuvuna mwagilia maji, piga dawa (kama ni muhimu) na weka mbolea kuongeza
uzalishaji unaofuata.
usindikaji.
Hoho huuzwa ikiwa bado fresh tofauti na jamii nyingine za pilipili ambazo
zinaweza kukaushwa na kusindikwa kasha kuuzwa baadae.
Soko la pilipili hoho
Soko la hoho lipo nchi nzima kwenya masoko makubwa na hata magengeni, hoho
hutumiwa zaidi kama kiungo cha kupikia mapishi mbali mbali au kutia kwenye
kachumbari. Tatizo kubwa wanalokabiliana nalo wakulima ni kutokuwa na soko la
uhakika ndani na nje ya nchi, mazao huweza kuoza shambani au njiani kutokana na
tabu ya usafiri hasa vijijini ambapo mvua zikinyesha barabara hazipitiki kwa
urahisi
KILIMO BORA CHA PILIPILI HOHO
Reviewed by BENSON
on
July 19, 2017
Rating:
No comments