MAMBO MANNE UNAYOTAKIWA KUFANYA ILI KUJUA THAMANI YA MAZAO YAKO NA KUPANGA BEI YA FAIDA
Habari
za kazi ndugu yangu na karibu tena katika muendelezo wa makala zetu za
kilimo cha kisasa. Leo nimeona nikufahamishe namna sahihi unayotakiwa
kuitumia kujua thamani ya mazao yako na hivyo uweze kupanga bei isiyo na
hasara kwako. Mkulima ni mfanyabiashara, na mfanyabiashara yeyote ni
mtu anayelenga faida kubwa au hasara kidogo. Kwa hiyo ni muhimu kwa
mkulima kujua thamani ya mazao yake ili aweze kujua ni bei gani
anayotakiwa kuuzia mazao yake lakini pia ajue bei ambayo akiuza kwayo
atapata hasara.
Nimeamua
kuleta somo hili kwa sababu wakulima wengi wanauza mazao yao sio kwa
sababu wameiona faida ila tu kwa sababu ya msukumo wa soko/madalali na
bei iliyopo wakati husika. Hivyo basi natarajia mpaka mwisho wa somo
hili utakuwa umejifunza mambo unayotakiwa kufanya ili ujue thamani ya
mazao yako na uweze kujipangia bei yako mwenyewe yenye kukuletea faida
bila ya kushawishiwa na madalali.
Okay tuendelee, sasa basi unachotakiwa kufanya ni:
HATUA YA KWANZA
“Mali bila daftari hupotea bila habari”.
Waliona mbali sana waliosema maneno haya. Mkulima unatakiwa uwe na
daftari la kutunzia kumbukumbu za shughuri zako zote za shamba. Tunza
kumbukumbu za gharama zote ulizozitumia katika kilimo chako. Kama
ulikodi shamba au ulinunua, ulilima kwa trekta, ukaajiri watu wa
kupanda, ukanunua mbolea na madawa ya kuulia magugu na wadudu, kama
uliajiri watu wa kupiga dawa shambani, mpaka kuvuna n.k gharama zote
ulizotumia katika shughuri hizi zihifadhi kwani hii ndio dira yako.
Hakikisha kuwa unatambua ukubwa/eneo la shamba ulilolima kama ni hekta
moja au mbili ama ni ekari tatu au nne. Hapa utapata jumla ya gharama ulizotumia katika uzalishaji kwa eneo husika.
HATUA YA PILI
Pima
jumla ya kiasi cha mavuno yako. Kiasi cha mavuno unaweza kukipima kwa
idadi ya magunia au matunda, kwa uzito (Kg) au ujazo (lita au debe).
Napendekeza upime kwa magunia, kilo au/na idadi ya matunda kwa sababu
ndio vipimo tunavyotumia kuuza bidhaa zetu sokoni. Kama ni vitunguu
utapima kwa kilo au magunia, yaani ujue umevuna magunia mangapi katika
eneo ulilolima. Kama ni matikiti/matango basi utapima kwa idadi ya
matunda, yaani jumla ya matunda uliyovuna. Kama ni mchele basi utaupima
kwa kilo ili ufahamu umepata jumla ya kilogram ngapi. Pima mavuno yako
kwa njia yoyote unayoitumia wewe ilimradi tu mwisho wa siku ujue umevuna
kiasi gani. Hapa utapata jumla ya mavuno kwa eneo husika.
HATUA YA TATU
Katika
hatua hii gawanya jumla ya gharama za uzalishaji kwa kiasi cha mavuno.
Lengo letu hapa ni kujua umegharamia pesa kiasi gani kwa gunia moja au
kilo moja au kwa tunda moja ulilovuna. Hii ndiyo thamani ya mazao yako.
Ili tuelewane vizuri hapa tuchukulie kwa mfano gharama za uzalishaji ni
TSh. Milion moja na nusu ulizotumia katika ekari moja:
- Kama ulilima vitunguu na ukapata (kwa mfano) gunia 50: basi gharama ulizotumia kuzalisha gunia moja ni = 1,500,000/50 ambayo ni = TSh 30,000. Kwa hiyo ulitumia TSh 30,000 kuzalisha kila gunia moja la vitunguu (ikumbuke pointi hii)
- Kama ulilima matikiti na ukavuna matunda 4000: basi gharama ulizotumia kwa kila tikiti moja ni = 1,500,000/4000 = TSh. 375. Kwa hiyo thamani ya kila tikiti moja ulilozalisha ni Tsh 375 (Ikumbuke pointi hii)
- Na kama ulilima mpunga na ukataka kuuza mchele, tuseme umepata Kg 1000 za mchele: kwa hiyo gharama ulizotumia kuzalisha kila kilo moja ya mchele ni = 1,500,000/1000 = Tsh. 1500. Hivyo basi kila kilo moja ya mchele uliyozalisha imekugharimu Tsh. 1500 (ikumbuke pointi hii)
Sasa tupandishe kidogo gharama za uzalishaji, kutoka milioni moja na nusu mpaka milioni tatu kwa eneo lile lile la ekari moja:
- Kwa vitunguu ambavyo umevuna gunia 50, basi gharama za kuzalisha kila gunia zitakuwa ni Tsh. 60,000 badala ya Tsh 30,000 (rejea mahesabu ya hapo juu)
- Kwa matikiti ambayo umevuna jumla ya matunda 4000 basi gharama za kila tikiti zitakuwa ni Tsh 750 badala ya Tsh 375
- Na kwa mpunga ambao umevuna Kg 1000 za mchele basi kila kilo moja itakuwa imekugharimu Tsh 3000 badala ya Tsh 1500
Unajua
ni kwanini tumebadilisha gharama za uzalishaji? Lengo letu hapa ni
kuonesha jinsi gani gharama za uzalishaji zinavyochangia katika thamani
ya mazao yako na hivyo katika kufanya maamuzi ya bei yako ya faida.
Ikiwa gharama za uzalishaji ni kubwa basi mazao yako yanathamani kubwa
na hivyo basi ili upate faida ni lazima uuze kwa bei kubwa kuliko
thamani yake kama tutakavyoona hapa chini.
HATUA YA NNE:
Sasa
baada ya kujua thamani ya gunia moja au kilo moja au tunda moja, hatua
nyingine ambayo ndio muhimu zaidi ni kupanga bei sahihi yenye faida
utakayouzia mazao yako. Hapa tunahitaji kupanga bei ya mazao kwa kipimo
husika yaani bei ya gunia moja au kilo moja au tunda moja. Bei yenye
faida kwako ni ile itakayorudisha gharama zote ulizotumia katika
uzalishaji wako. Sasa rejea hatua ya tatu hapo juu:
- Kama jumla ya gharama za uzalishaji ni milioni moja na nusu: gunia moja la vitunguu lilikugharimu Tsh 30,000 hivyo basi bei nzuri kwako hapa ni kuanzia Tsh 35,000 kwani itarudisha gharama zako za uzalishaji (30,000) na kukupa faida ya Tsh 5000 kwa kila gunia moja.
- Na kama jumla ya gharama za uzalishaji ni milioni tatu: gunia moja la vitunguu lilikugharimu Tsh 60,000 hivyo basi ili upate faida ni lazima uuze vitunguu vyako kuanzia Tsh 65,000 hapo utakuwa umejilipa gharama zako na kubaki na faida ya Tsh 5000 kwa kila gunia.
- Hivyo hivyo utafanya kwa mchele, matikiti na mazao mengine yote uliyolima
Baada
ya kujipangia bei yako sasa toka nje uangalie soko likoje, je bei
uliyojipangia ni ndogo au kubwa kuliko iliyoko sokoni? Ikiwa bei
uliyopanga kuuza mazao yako ni ndogo kuliko inayotembea sokoni kwa
wakati huo (au bei ya sokoni ni nzuri zaidi kuliko uliyotegemea wewe)
basi fanya hima uuze kwani utakuwa umevuka matarajio yako katika
uzalishaji kitu ambacho kila mtu anakitamani.
Lakini ukiona bei ya sokoni ni mbaya yaani ni ndogo kuliko ile uliyotaka kuuzia mazao yako fanya moja kati ya yafuatayo:
- Kwa mazao yanayohifadhika basi yahifadhi kwa muda ili kupisha hali mbaya ya soko. Hakikisha kuwa mazao yako yanahifadhika na una miundombinu ya kuhifadhia kwa angalau miezi mitatu hadi sita. Kumbuka kuwa unapoamua kuhifadhi unaongeza gharama za ulinzi na za kuhifadhi hivyo utakapotaka kuuza itabidi uzitilie maanani gharama hizi. Kwa maana nyingine ni kwamba unaongeza gharama za uzalishaji kwa hiyo utatakiwa kuongeza ile bei ya kuuzia (Fuata hatua nne tulizoelezea hapo juu).
- Na kwa mazao yasiyohifadhika kama mboga mboga na matunda (nyanya, matikiti) basi epuka hasara kubwa. Ninaposema epuka hasara kubwa namaanisha uza mapema kadri uwezavyo, kwani kuchelewesha kuna hasara tatu: (1) kuendelea kusubiri kunakuongezea wewe gharama za ulinzi na uhifadhi, (2) kusubiri kunaweza kusababisha kuoza kwa mazao yako kitu ambacho kitapunguza ubora na uwingi wa mazao na hatimaye kipato chenyewe na (3) Inawezekana wakati wewe unaendelea kusubiri bei ikazidi kushuka hivyo utajisababishia hasara kubwa zaidi. Kwa hiyo kwa mazao yasiyohifadhika uza mapema ili uepuke hasara kubwa zaidi.
Ushauri:
katika kilimo chochote utakacho kifanya jitahidi sana kupunguza gharama
za uzalishaji ili ujiongezee nafasi ya kupata faida kubwa zaidi.
Punguza gharama zote zisizo za lazima, lakini usijisahau kiasi cha
kuathiri ubora na wingi wa mavuno.
Kabla hatujamaliza kabisa nikukumbushe kuwa tumeshaandika baadhi ya makala za jinsi ya kufanya kilimo bora na chakisasa, zipo hapa chini (bofya kuzisoma):
Kabla hatujamaliza kabisa nikukumbushe kuwa tumeshaandika baadhi ya makala za jinsi ya kufanya kilimo bora na chakisasa, zipo hapa chini (bofya kuzisoma):
Hivi
ndivyo tunamaliza somo letu la leo, je umejifunza kitu chochote?
Ulikuwa unafanyaje unapotaka kujua thamani ya mazao yako? Weka mawazo
yako hapa chini kwenye comments. Tukutane tena Jumatatu ijayo katika
makala nyingine tena...
MAMBO MANNE UNAYOTAKIWA KUFANYA ILI KUJUA THAMANI YA MAZAO YAKO NA KUPANGA BEI YA FAIDA
Reviewed by BENSON
on
February 28, 2018
Rating:
I found this document very helpful and useful... I need further informations through my email please manasehphilip@gmail.com
ReplyDeletejamani nice sana,
ReplyDeletenafatilia sana masomo yako,ila naomba kujua kama kuna huduma zaid ya hapa (kwenda deep) unaitoa kwa kulipia ,maana nahtaji kujifunza vyote vinavyohitaji katika zao husika,kwan tumeona wengi huwa wanaweka asilimia 50 na asilimia zilizobaki mteja anazilipia
ReplyDelete