ZIJUE KANUNI BORA ZA KUFUGA BATA BUKINI.

Mara nyingi nimekuwa nikipokea maswali kutoka kwa wasomaji wetu, wengi wao wanasema ya kwamba wanatamani sana kufuga bata bukini lakini wamekuwa hawajui mbinu za kuweza kufanya hivyo, hivyo kwa kuwa nami sina hina nitaenda kukupa leo mbinu bora za kufuga bata bukini.

Bata Bukini ni ndege ambao asili yao ni India na Japan. Hii ni jamii ya ndege wafugwao lakini tofauti kubwa ya bata wa kawaida wao wana asili ya usafi, hivyo hawapendi uchafu na kamwe hawali mizoga.

Tofauti na ndege wengine au bata wengine wa kawaida, mfugaji wa bata bukini anaweza kupata kipato kikubwa kwa haraka na kwa gharama ndogo ukilinganisha na bata wengine.
Kuna aina mbili ya bata bukini ambao ni weupe na wenye mchanganyiko wa rangi. Hali kadhalika hutofautiana katika utagaji wa mayai.

Chakula

Ndege hawa wanakula chakula kama wanacholishwa kuku, wanapendelea kula majani jamii ya mikunde kwa 50% na hawahitaji chakula kingi. Vifaranga ni lazima wapatiwe lishe kamili hasa protini kwa wingi ili waweze kujenga mwili, kukua vizuri na kuwa na afya nzuri.

Kwa maana hiyo, vifaranga wanahitajika kupata walau 20% ya protini kwa wiki mbili za awali na baada ya hapo waweza kupunguza hadi 15% kulingana na kukua kwao hadi wanapokuwa wanaelekea kukomaa.

Kama ambavyo mfugaji anaweza kutengeneza chakula kwa ajili ya mifugo wengine, pia anaweza kutengeneza cha bata bukini kama ifuatavyo:

Mahitaji

1. Mahindi kilo 10 ( hakikisha hayana dawa)
2. Chokaa kilo 5 (ya kulishia mifugo)
3. Dagaa kilo 10 (wanaotumika kulishia kuku)
4. Mashudu kilo 20.


Utengenezaji na Uhifadhi

Baada ya kupima vyakula hivi kwa usahihi chukua pipa, changanya vizuri kisha walishe bata kulingana na wingi wao na uhakikishe wanapata chakula cha kutosha.Vipimo hivi hutegemea wingi wa bata unaowafuga lakini hakikisha uwiano huo unazingatiwa. Baada ya kutengeneza chakula unaweza kuhifadhi katika mifuko na kuweka katika eneo lisilokuwa na unyevu.


Kuatamia

Jinsi ilivyotofauti katika idadi ya utagaji wa mayai hivyo ndivyo uwezo wa kuatamia pia ulivyo. Bata Bukini weupe huatamia mayai 6 na wale wa rangi huatamia mayai 12
Ndege hawa huatamia kwa siku 29, huangua vifaranga kwa siku 3 na mara nyingi hutotoa mayai yote, si rahisi mayai kubaki bila kutotolewa au kuharibika.


Namna ya kutunza vifaranga

Mara tu vifaranga wanapoanguliwa, wachukue na kuwatenga na mama yao kisha waweke katika banda safi lisilopitisha baridi. Unaweza kuwawekea taa ya umeme kama una uwezo ili kuwatengenezea joto.
Pia, waweza kuzungushia banda lao kitu kizito kama blanketi ili kuwakinga na baridi au upepo.


Banda

Bata Bukini wanahitaji nafasi ya kutosha hivyo andaa banda kulingana na wingi wa bata unaotarajia kufuga.

Hakikisha banda limesakafiwa au banda la udongo lisilotuamisha maji au unaweza kuweka mbao au mabanzi kisha unaweka maranda ili kuwakinga na baridi.

Maji

Ni lazima bata wapatiwe maji ya kunywa kila siku na hakikisha banda halikosi maji wakati wote. Safisha chombo cha maji na kubadilisha maji kila siku.
Ndege hawa wanahitaji maji ya kunywa ya kutosha kama ilivyo kwa kuku. Hakikisha maji yako kwenye chombo ambacho hayatamwagika , kwani kumwagika kunaweza kusababisha kuibuka kwa magonjwa. Bata Bukini hawapendi uchafu. Hivyo maji yawe mahali ambapo hayatachafuka.


Magonjwa

Ni mara chache sana bata bukini kushambuliwa na magonjwa kama watawekwa katika hali ya usafi. Magonjwa yanayoweza kuwasumbua ni mafua na wakati mwingine kuharisha.


Tiba za asili

Unaweza kutibu bata bukini kwa njia za asili. Tumia mwarobaini, vitunguu (maji na saumu).

1. Mwarobaini
Unaweza kutumia dawa hii kutibu mafua kwa bata bukini wakubwa au vifaranga.


Maandalizi

Chukua kiasi kidogo cha mwarobaini kisha twanga vizuri kupata maji maji. Kamua maji ya mwarobaini, kisha changanya na maji uliyo andaa kuwanywesha vifaranga.


2. Kitunguu Saumu na Kitunguu Maji:

Dawa hii hutumika kukinga na kutibu bata bukini wanaoharisha.


Maandalizi

Unachukua kitunguu saumu au maji na kuondoa maganda ya nje kisha safisha na kukata vipande vidogovidogo na kuwawekea kama chakula.Unaweza kuwapatia kila siku hadi watakapopona.


3. Majani: Bata Bukini chakula chao kikubwa ni majani. Majani yana vitamini A, hivyo hakikisha unawapatia ya kutosha. Wapatie majani jamii ya mikunde.

Kutaga

Bata Bukini huanza kutaga baada ya miezi saba na hutaga mara tatu kwa mwaka. Isipokuwa, utagaji wa bata bukini weupe na wa rangi hutofautiana katika idadi ya mayai, Bata Bukini weupe hutaga mayai sita tu lakini wale wa mchanganyiko wa rangi hutaga mayai kumi na mbili (mara mbili ya weupe)



ZIJUE KANUNI BORA ZA KUFUGA BATA BUKINI. ZIJUE KANUNI BORA ZA KUFUGA  BATA BUKINI. Reviewed by BENSON on September 12, 2017 Rating: 5

No comments