USIYOYAFAHAMU KUHUSU KILIMO CHA NJUGU.
Njugu ni mbegu za mmea wa njugu. Mmea huo
unapoendelea kusitawi huwa unachanua maua ya manjano ambayo hujichavusha
yenyewe. Kilimo hiki kina faida hasa pale mkulima anapoamua kujiwekeza katika kulima kilimo hiki.
Ovari iliyotiwa mbegu ya kiume ambayo iko kwenye
ncha ya shina ya mmea huo huanza kuingia udongoni. Ovari hiyo huwa na
mbegu. Mbegu hiyo inapoingia udongoni, hukua sambamba na udongo wa juu, halafu
inakomaa ikielekea chini. Kisha mbegu hiyo inakuwa njugu. Mmea mmoja unaweza
kuwa na njugu 40.
Njugu husitawi vizuri katika maeneo yenye joto na
mvua ya wastani. Kuna kipindi cha siku 120 au 160 kati ya wakati wa kupanda na
kuvuna, ikitegemea aina ya njugu na hali ya hewa. Wakati wa kuvuna, ni lazima
wakulima wa njugu wachimbue mimea hiyo na kuipindua, halafu wanaiacha ikauke
ili isioze wakati inapohifadhiwa. Siku hizi, wakulima wengi hutumia mashine za
kilimo za kisasa zinazowawezesha kuchimbua mimea hiyo, kuikung’uta, na
kuipindua kwa wakati mmoja.
Matumizi Mengi ya Njugu
Njugu ni chakula chenye virutubisho vingi sana.
Njugu husaidia sana umeng’enyaji wa chakula, na zina vitamini 13 na madini
26. Vingi kati ya virutubisho hivyo havipatikani katika vyakula vya
kisasa. Kitabu The Encyclopædia Britannica kinasema: “Njugu
zina protini nyingi zaidi, madini mengi zaidi, na vitamini nyingi kuliko maini
ya ng’ombe.” Lakini watu wanaotaka kupunguza uzito wao wanapaswa kutahadhari!
Njugu zina “mafuta mengi kuliko malai nzito” na “kalori nyingi kuliko sukari.”
Njugu hutumiwa katika vyakula vingi vinavyopikwa
katika nchi nyingi na ni rahisi sana kutambua ladha yake. Anya von
Bremzen, mwandishi katika fani ya upishi, anasema: “Ladha ya njugu ni tamu sana
na haina kifani, kwa hiyo chakula chochote kilichotiwa njugu kitakuwa na ladha
kama ya njugu. Kwa hiyo, uwe ni mchuzi wa njugu wa Indonesia, supu ya Afrika
Magharibi, spageti za Kichina, kitoweo cha Peru, au mkate uliopakwa siagi ya
njugu, ladha ni ileile.”
Vilevile, njugu ni kitafuno kinachopendwa na wengi
kotekote ulimwenguni. Kwa mfano, huko India njugu huchanganywa na maharagwe
makavu na kuuzwa barabarani. Kulingana na
kitabu The Great American Peanut, inasemekana kwamba
siagi ya njugu, ambayo hupakwa kwenye mkate katika nchi kadhaa, “ilivumbuliwa
na daktari mmoja kutoka St. Louis [Marekani] wapata mwaka wa 1890 kwa madhumuni
ya kutunza afya ya watu wazee.”
Lakini mbali na kutumiwa kama chakula, njugu zina
matumizi mengineyo. Katika bara lote la Asia, njugu hutumiwa kutengeneza mafuta
ya kupikia. Mafuta ya njugu yanaweza kutumiwa pia kupikia vyakula vinavyohitaji
kupikwa kwa moto mkali, na hayapati harufu ya vyakula vinavyopikwa.
Huko Brazili, masalio ya njugu zilizotumiwa
kutengeneza mafuta ya kupikia hutumiwa kutengeneza chakula cha mifugo. Na
bidhaa nyingi hutengenezwa kutokana na njugu.—Ona maelezo yaliyo juu.
Jihadhari na Mizio ya Njugu!
Njugu zinaweza kukaa kwa muda mrefu bila
kuhifadhiwa kwenye friji. Hata hivyo, tunapaswa kutahadhari. Njugu ambazo zilizoanzwa
kuwa kuvu zina kemikali hatari inayoitwa aflatoxin ambayo ina uwezo
mkubwa wa kusababisha kansa. Isitoshe, watu wengine wana mizio ya njugu.
Wanapokula njugu ‘wanaweza kutokwa na kamasi puani na kupata vipele au
kuathiriwa mwili mzima (anaphylactic shock),’ lasema
gazeti Prevention.Uchunguzi mbalimbali umeonyesha kwamba siku hizi watoto
wengi zaidi wanapata mizio ya njugu.
Gazeti Prevention linaripoti kwamba ikiwa
wazazi wote wawili wana ugonjwa wa pumu, mzio wa kupata uvimbe puani, au
ukurutu, kuna uwezekano mkubwa kwamba mtoto wao atapata mzio wa njugu.
Jambo hilo pia linawahusu watoto ambao mama zao
wana mizio na pia watoto wanaopata mzio wa maziwa kabla ya kufikia umri wa
mwaka mmoja. Dakt. Hugh Sampson, profesa wa magonjwa ya watoto kwenye Kituo cha
Kitiba cha Chuo Kikuu cha Johns Hopkins huko Marekani, anasema: “Ni afadhali
wazazi wasiwape watoto wao siagi ya njugu hadi wanapofikia umri wa miaka
mitatu.”
Iwe unapenda njugu au la, huenda mazungumzo haya
kuhusu matumizi yake mengi yamekufanya uthamini mbegu hiyo ndogo inayopendwa na
wengi.
USIYOYAFAHAMU KUHUSU KILIMO CHA NJUGU.
Reviewed by BENSON
on
July 26, 2017
Rating:
No comments