KILIMO BORA CHA UYOGA- sehemu ya 02


Siku ya jana tuliangalia sehemu ya kwanza ya kilimo cha oyoga na siku ya leo tutaona sehemu ya pili ya kilimo hiki.

Mambo Ya Kuzingatia katika kilimo hiki.
1. Uzalishaji wa uyoga huzingatia sana hali ya hewa na vifaa ulivyonavyo, hivyo basi, kabla hujachagua aina ya uyoga unaotaka kupanda pata ushauri kwa wataalamu walio karibu nawe.

2.  Ukishanunua mbegu, kama hupandi kwa muda huo, hakikisha umehifadhi mbegu hiyo kwenye jokofu. Kama huna jokofu la kuhifadhia, nunua mbegu baada ya kuandaa kila kitu. Hata hivyo, uotaji wa mbegu huwa mzuri kama zitakaa nje ya jokofu kwa siku mbili.

3. Mbegu za uyoga huwekwa ndani ya chupa yenye ujazo wa mililita 300, waweza kutumia chupa moja katika kupanda kwenye kilo 15 ya mali ghafi ya kuoteshea. Hakikisha unamaliza mbegu yote iliyo ndani ya chupa kwani ikibaki itapata maambukizo ya vimelea.

4. Hakikisha unaponunua mbegu iwe ni nyeupe. Mbegu ambayo siyo nyeupe ni dalili za maambukizo ya vimelea vingine na hivyo haifai kwa kupanda.

5. Hakikisha chumba cha kupandia ni kisafi na hakipati vumbi toka nje ili kuzuia maambukizo ya magonjwa ya uyoga.

6. Usimwagilie uyoga maji yasiyochemshwa kwani maji hayo mara nyingi si salama. Yaweza kusababisha vimelea vingine kuota, kwani uyoga ni dhaifu kuhimili ushindani wa vimelea.

7. Pia waweza kusababisha magonjwa ya uyoga ambayo kutibu kwake kunahitaji kutumia dawa za viwandani ambazo ni sumu na hivyo kusababisha madhara kwa mlaji.

faida zitokanazo na kilimo cha uyoga.
Unaweza kupata faida nyingi kutokana na uzalishaji wa uyoga, faida hizo ni kama zifuatazo:-
1.       Lishe kama protini inayolingana na ile ipatikanayo kwenye maziwa, samaki na kunde. Pia utapata vitamini B, C, na D, na madini ya joto, phosphoras, chuma na potashi.

2.      Uyoga husadikika kutibu maradhi kama kifua kikuu, kisukari, moyo, shinikizo la damu na figo.

  Masalia ya mazao hutumika katika kuzalishia uyoga, na baadaye yanaweza kutumika kama mbolea asili kwa kilimo cha bustani. Masalia ya kilimo cha uyoga pia hutumika kama chakula cha mifugo kama ng’ombe.

4.      Kilimo hiki huhitaji eneo dogo sana la ardhi na kiasi kidogo cha maji, hivyo hupunguza tatizo la ukosefu wa ardhi na ugomvi katika jamii ambao unatokana na tatizo hilo.

5.       Kilimo cha hiki cha uyoga ni njia nyepesi ya kutoa ajira kwa familia kutokana na gharama ndogo, teknolojia rahisi inayotumika na pato lake kubwa.


KILIMO BORA CHA UYOGA- sehemu ya 02 KILIMO BORA CHA UYOGA- sehemu ya 02 Reviewed by BENSON on July 06, 2017 Rating: 5

No comments