KILIMO BORA CHA UYOGA -sehemu ya 01
Miaka ya karibuni, utaalamu wa kilimo cha uyoga umeanza hapa
Tanzania baada ya watu kutilia maanani lishe bora ya protini na manufaa mengine
ya zao hilo. Kwa kuwa uyoga upo wa aina mbalimbali, usitawishaji wake hutofautiana
katika mahitaji yake, ikiwa ni pamoja na hali ya hewa, malighafi za kuoteshea,
urahisi wa teknologia ya kuotesha katika mazingira ya Tanzania na soko lake kwa
wananchi na katika hotel. Hata hivyo ni wananchi wachache tu wanaojua kilimo
cha uyoga. Uyoga unaozalishwa unafahamika. Aina zinazofaa kwa Tanzania ni zile
ambazo hustawi vizuri, kwenye maeneo ya joto la wastani wa nyuzi joto 20C hadi
33C.
Namna Ya Kuotesha Uyoga
Kabla ya kuanza kuzalisha uyoga inabidi kuwa na chumba chenye paa
ambalo litazuia jua, mvua, na vumbi. Chumba hiki kinatakiwa kiwe na sakafu
inayohifadhi unyevunyevu pamoja na sehemu ya giza ambayo ni muhimu kwa kuotesha
utando wa uyoga.
Mbegu za uyoga huzalishwa kwenye maabara zenye vifaa vinavyowezesha kuotesha
mbegu hizo bila kuchafuliwa au kuchanganyika na vimelea kama bakteria, ukungu
au jamii nyingine za uyoga ambazo haziliwi. Hapa Tanzania hivi sasa maabara
hizo zipo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, kituo cha utafiti wa kilimo-Uyolena taasisi ya utafiti wa kilimo cha
bustani- Tengeru (HORTI – Tengeru, Arusha).
Hatua Muhimu Katika Kuotesha Uyoga
Hatua muhimu za kuotesha uyoga baada ya kupata mbegu ni kama ifuatavyo:
- Kusanya masalia ya mzao kama vile mabua, majani ya mpunga, ngano, pumba za
- mpunga au mahindi, masalia ya miwa baada ya kukamua nk. Vitu hivi hutumika kama mali ghafi kwa kuoteshea uyoga.
- Mabua, majani ya mpunga au migomba yakatwe kwa urefu usiozidi sm 6, au urefu wa vidole kwa kutumia panga au kisu.
- Loweka mali ghafi kwenye maji ya kawaida kwa muda wa siku nzima (saa 24).
- Kisha yachemshe kwa muda wa saa mbili ili kuua vijidudu pamoja na vimelea vilivyomo.
- Ipua na umwage maji yote halafu tandaza kwenye kichanja kisafi ili yapoe bila kuchafuliwa na vumbi au vijidudu.
- Kisha jaza mali ghafi hii katika mifuko ya nailoni tayari kwa kupanda mbegu.
Namana ya kupanda
Kuna aina mbili za upandaji:
1. Aina ya kwanza:
Chukua
mfuko wa nailoni wenye upana wa sm 40 - 45 na kimo sm 75. Weka tabaka ya mali
ghafi ya kuoteshea yenye kina cha sm 10 katika mfuko halafu tawanya mbegu ya
uyoga juu yake.
Baada ya kuweka mbegu, weka tena tabaka nyingine ya vioteshea na
kuweka mbegu juu yake. Endelea kuongeza tabaka kwa namna hii mpaka ifike ujazo
wa robo tatu ya mfuko.
2.Aina ya pili:
Changanya malighafi ya kuoteshea (baada ya kuchemshwa na kupoa) na
mbegu ya uyoga katika uwiano wa 1: 25 (mbegu : mali ghafi ya kuoteshea) kwa
uyoga aina ya mamama (Pleurotus spp.).
Kisha mchanganyiko huo ujazwe katika mifuko ya nailoni, mifuko hii iwe na
ukubwa wa sm 20 kwa sm sm 40 ambamo unaweza kujaza kilo 1 - 11/2 ya mali ghafi
ya kuoteshea. Funga mifuko na toboa matundu kwenye mifuko yenye kipenyo cha sm
1 kwa kila umbali wa sm 6 hadi 10 kwa kila mfuko.
Zingatia: Matundu yawe mengi ili kuingiza hewa ya kutosha ndani ya mifuko.
Kumbuka uyoga ni kiumbe hai hivyo unahitaji kupumua.
uotosheaji wa uyoga kwa njia ya mifuko |
Matunzo Ya Zao La Uyoga
Weka mifuko kwenye chumba cha giza. Kwa mkulima wa kawaida waweza
kutumia kasha lisilopitisha mwanga kama chumba cha giza. Acha mifuko humo kwa
muda wa siku 14 - 21 bila kufunua ili ukungu mweupe uweze kutanda vizuri.
Utando wa uyoga ukishatanda vizuri kwenye malighafi ya kuoteshea, hamishia
kwenye chumba chenye mwanga na hewa ya kutosha kisicho pigwa na jua. Katika
chumba chenye mwanga, mifuko inaweza kuwekwa kwenye, meza, chanja la waya au
miti. Mifuko inaweza pia kuning’inizwa kwenye kamba toka kwenye boriti.
Zingatia: Unatakiwa kudumisha hali ya unyevu kwenye chumba hicho cha mwanga
kwa kumwaga maji sakafuni. Ukiona vipando vinakauka unaweza kunyunyizia maji
yaliyochemshwa na kupoa juu ya mifuko mara tatu au zaidi kwa siku. Tumia bomba
la mkononi lenye ukubwa wa lita moja kunyunyizia maji.
Tahadhari: Usizidishe maji kwani maji yakiwa mengi sana yaweza kuozesha uyoga
uliyoanza kuota. Aina nyingi za uyoga huanza kutoa vichwa (pini) siku 2 - 3
baada ya kuwekwa kwenye mwanga.
Uvunaji Wa Uyoga
Uyoga huwa tayari kuchumwa siku tatu baada ya vichwa /pini
kuonekana. Uyoga uvunwe kwa mkono kwa kushika katikati ya shina la uyoga kisha
zungusha hadi uyoga ung’oke. Usiondoe kichwa peke yake katika kuvuna uyoga
kwani kubakiza shina huzuia uyoga mwingine kutokea.
Zingatia: Mkulima anatakiwa ajue soko la
uyoga kabla ya kuvuna ili kuepuka gharama za kuhifadhi. Kwani uyoga ukishavunwa
unatakiwa uliwe kabla haujaharibika.
somo hili litaendelea siku ya kesho
KILIMO BORA CHA UYOGA -sehemu ya 01
Reviewed by BENSON
on
July 05, 2017
Rating:
tunashukuru kwa elim ila ningependa kujua soko la huu uyoga nitalipataje?
ReplyDelete