MAMBO YA MSINGI YA KUZINGATIA KATIKA UJENZI WA BANDA LA KUKU
Habari ndugu mfugaji, katika ufugaji kuku kitu moja wapo cha kuzingatia
banda bora. Banda bora litawafanya kuku wako wakue vizuri na kuwa Kinga na
magonjwa Karibu tuwe pamoja hapa!! Ujenzi wa mabanda bora ya kuku ni miongoni
mwa mambo ya msingi kabisa katika ufugaji bora wa kuku wawe ni wa asili au wale
walioboreshwa. Hata hivyo si kila mtindo wa ujenzi unafaa, kwahiyo ujenzi huo
ni lazima uzingatie mahitaji halisi ili ufugaji huo uweze kutoa matokeo bora
yanayotarajiwa na mfugaji.
Banda la kuku |
Mambo muhimu katika ujenzi wa banda la kuku ni;
1.Liingize hewa safi wakati wote.
2. Liwe kavu daima.
3. Liwe nafasi ya kutosha.
4. Liwe la gharama nafuu lakini la kudumu.
5. Lizuie kuingia wanyama na
wadudu hatari kwa kuku.
6. Liwe na nafasi ya kuweka vyombo vya chakula na maji. _.
7. Lizuie upepo wakati wa baridi
kali.
Hewa na mwanga:
Hewa ni muhimu kwa kila kiumbe, hivyo banda la kuku ni lazima liingize
hewa safi na kutoa ile chafu na liweze kuingiza mwanga wa kutosha. _. Kwa
kifupi ni kwamba madirisha ya banda ni lazima yawe makubwa na ya kutosha ili
yaingize hewa safi na kutoa ile chafu. _ Ni vema madirisha haya yawe juu kiasi
cha meta moja (1) kutoka chini ili hewa ipite juu ya vichwa vya kuku.
Hewa safi siyo upepo, hivyo
jaribu kuzuia upepo mkali kuingia ndani ya banda la kuku ama sivyo kuku
wataugua ugonjwa wa mafua na niumonia na vifaranga vinaweza kufa kwa ugonjwa wa
baridi.
Jenga Banda lako kwa kukinga upepo unakotokea na kupanda miti kuzunguka
banda hilo la kuku ili kupunguza kasi ya upepo na kuweka kivuli dhidi ya jua
kali na joto.
Ukavu na usafi ndani ya banda.
Kwa vile kuku si ndege wa majini kama bata , ni jambo la busara
kuhakikisha kuwa mahali anapoishi hapana unyevunyevu. Banda la kuku lijengwe
mahali palipoinuka ili kuzuia maji ya mvua yasiingie. Wajengee kuku uchaga wa
kulalia kwa kuweka viguzo vyenye urefu wa meta moja na kutandika miti juu yake
ili usiku walale hapo, kuliko kuwalaza ardhini au sakafuni.
Ukavu wa banda ni muhimu sana hasa kwa vifaranga na kuku wanaotaga.
Ndani ya banda lenye unyevu mayai kuchafuka sana hata wakati mwingine huoza kwa
urahisi na jitihada zako zitakuwa ni bure. Sakafu ya banda ni vizuri ikawa ya
zege lakini kutokana na uhaba wa fedha sakafu inaweza kutengenezwa kwa mabanzi
(mabanda yaliyoinuliwa) au udongo mgumu na au mchanga ambao utafunikwa kwa
mabaki ya taka za mpunga na yale ya mbao. Ili kuepuka unyevunyevu ni vyema
eneo/mahali pla kujenga banda pawe pameinuka na penye kupitisha hewa ya
kutosha.
Paa la banda.
Paa la banda liwe madhubuti ili
kuzuia maji ya mvua kuingia hasa wakati wa masika. Sakafu ya banda iwe juu
zaidi ya usawa wa nje. Paa linaweza kuezekwa kwa mabaki ya vipande vya bati ,
madebe na kama ikishindikana tumia nyasi zinazofaa kwa ajili ya kuezeka nyumba
katika eneo hilo.
Nafasi ya kufanyia kazi.
Banda la kuku lisiwe na nguzo au
mbao nyingi sana ndani kiasi cha kumfanya mhudumiaji wa kuku ashindwe kufanya
kazi zake. Hali hiyo itamfanya apoteze muda mwingi katika kuzizunguka nguzo hizo,
hasa wakati wa kuokota mayai au kufanya usafi.
Vifaa.
Unapotaka kujenga banda la kuku kwanza kabisa tayarisha vifaa
vinavyotakiwa. Vitu kama miti au nyasi, nyavu au fito, misumari au kamba ni
muhimu kuviandaa mapema. Pili ni lazima uwe na plani/ramani kamili ya banda
hilo. Kwa wastani kila kuku anahitaji nafasi ya Meta za eneo la 0.11 hadi 0.22
(futi 1 hadi 2 za eneo.) kutegemeana na umri wa kuku.
Ujenzi rahisi.
Kuku wafugwao hatimaye ni lazima wafidie gharama za Ujenzi wa mabanda na
chakula. Gharama zikiwa kubwa sana huenda ukaifanya shughuli ya ufugaji isiwe
na faida hata kidogo hali hiyo itamfanya mfugaji aone ufugaji hauna maana
yoyote kwake.
Lakini ukijenga banda lako kwa
kutumia vifaa vinavyopatikana kwa urahisi utaongeza faida zaidi kwakuwa umepunguza
gharama za uendeshaji wa mradi.
Vipimo vya banda.
Banda la kuku linatakiwa liwe na Meta 15 hadi meta 22 za eneo yaani Meta
3 hadi 4.5 za upana kwa meta 5 za urefu. Banda hili linaweza kutunza kuku 100
wakubwa kwa wakati mmoja.
Zingatia haya·
Ujenzi wa mabanda unasisitizwa katika kuboresha ufugaji wa kuku wa asili
iliKuongeza uzalishaji na kupunguza vifo vya vifaranga kwa majanga
mbalimbali kama vicheche ,mwewe, mapaka, mbwa na wizi wa kuku wanaozurura
holela. · Vile vile Inatakiwa kwamba kuku wanaozuiliwa kwenye banda na kuwekewa chakula mchanganyiko wataongeza uzalishaji kwa
kiasi kikubwa.
MAMBO YA MSINGI YA KUZINGATIA KATIKA UJENZI WA BANDA LA KUKU
Reviewed by BENSON
on
July 07, 2017
Rating:
No comments