KILIMO BORA CHA MPUNGA CHA UMWAGILIAJI
Maandalizi sahihi ya shamba ni jambo la msingi katika
kuboresha kilimo cha umwagiliaji wa mpunga. shamba lisipoandaliwa vema
husababisha mbinu bora zinazoshauriwa kutoonyesha matokeo katika kiwango
kinachotarajiwa hasa katika uzalishaji. Kimsingi maandalizi ya shamba
yanatakiwa yafanyike kwa usahihi na
kwa wakati katika mtiririko unaotakiwa. Zifuatazo ni hatua saba muhimu na za
msingi katika kilimo cha mpunga.
1. KUSAFISHA SHAMBA
Safisha shamba mapema kabla ya msimu kuanza. Kusanya na
kuangamiza visiki na takataka nyingine zote. Masalia ya mazao yanaweza kutumika
kutengeneza mbolea ya mboji. Inapobidi tumia moto kwa uangalifu sana maana moto
unaweza kuharibu mazingira, unaua wadudu rafiki, unaharibu udongo na kuteketeza
mboji.
2. KULIMA
Kulima husaidia kupunguza kiasi cha magugu, huruhusu mzunguko
mzuri wa hewa na maji, hurahisisha mizizi kupenya na kuchanganya masalia ya
mazao kwenye ardhi. Wakati wa kulima uangalifu unahitajika ili kuzuia kuharibu
usawa wa ardhi. Kina cha kulima kiwe kati ya sentimeta 10 na 15. Ili
kurahisisha na kuharakisha kazi ya kulima ni vema kutumia zana/mashine rahisi
kama Trekta la mkono na wanyamakazi.
3. KUKARABATI/KUJENGA MAJARUBA
Baada ya kulima hakikisha kuwa kingo za jaruba zimekarabatiwa
ili kuweza kuhifadhi maji vema. Kama ni shamba jipya, ujenzi wa kingo za jaruba
ufanyike kwa kufuata utaalamu unaotolewa. Kingo imara ni muhimu kudhibiti vema
maji shambani.
4. KUVURUGA
Weka maji shambani kiasi cha sentimeta 3 hadi 5 juu ya usawa
wa ardhi ili kukamilisha vema uvurugaji. Jembe la mkono linatumika lakini ili
kurahisisha na kuharakisha kazi hii ni vema kutumia trekta la mkono au
wanyamakazi. Unapotumia wanyamakazi au trekta la mkono weka maji shambani si
zaidi ya siku moja kabla. Shamba lililovurugwa vema huiwezesha mizizi ya miche
kupenya vema ardhini.
5. KUSAWAZISHA SHAMBA
Baada ya kuvuruga ni lazima kuhakikisha kwamba shamba
limesawazishwa vema. Shamba lililosawazishwa vema linaruhusu usambaaji
mzuri wa maji. Wakati wa kusawazisha kina cha maji kiwe kiasi cha
sentimeta 3-5 juu ya usawa wa ardhi Ili kurahisha kazi hii tumia reki ya ubao
ili kuvuta udongo kutoka sehemu zilizoinuka kuelekea sehemu zilizo bondeni.
6.VYANZO NA ATHARI ZA UPOTEVU WA MAJI YA UMWAGILIAJI
Ili kupata maji ya kutosha inabidi kuhakikisha kwamba upotevu
wa maji ya umwagiliaji unapungua kwa kiwango kikubwa na wakulima wanamwagilia
maji kwa kiasi kinachohitajika bila kuzidisha kiwango.
Vyanzo vya upotevu wa maji ya umwagiliaji katika skimu za
mfano ni pamoja na:
• Maji yanayopotea kwenye mifereji mikuu, ya kati na ile
midogo ya kusambaza maji mashambani.
• Maji yanayopotea mashambani wakati wa kumwagilia.
Upotevu wa maji kwenye mifereji mikuu, ya kati na ile ya
kusambaza maji unasababishwa na aina ya udongo uliotengeneza kingo za mfereji,
uchafu na matengenezo hafifu ya mifereji. Katika baadhi ya skimu upotevu
wa maji kwenye mfereji mkuu uliosababishwa na kuvuja maji kwenye tuta la
mfereji mkuu na kunywea chini ya ardhi ulikuwa mkubwa kiasi cha kuathiri
upatikanaji wa maji kwenye mashamba yaliyoko mbali na banio.Vilevile
athari nyingine ilikuwa ni maji mengi kuingia sehemu yasikohitajika na
kusababisha tatizo la maji kutuama kwa muda mrefu.Hivyo wakulima wanashauriwa
kupunguza upotevu huu wa maji kwenye mfereji kwa kujengea na kusakafia. Upotevu
wa maji mashambani wakati wa kumwagilia unasababishwa na kuvuja kwenye tuta
linalozunguka jaruba, kunywea chini na kuzidisha kiwango cha maji ya kumwagilia
kinachotakiwa. Hii mara nyingi inasababishwa na utengenezaji mbovu wa jaruba.
utengenezaji wa majaruba na uimarishaji wa kingo za jaruba umesaidia kupunguza
upotevu wa maji kwa kiwango kikubwa na hatimaye kuongeza mavuno na kipato cha
mkulima.
7. UPANDIKIZAJI
MPUNGA
Ili kupata mavuno mengi na kukifanya kilimo cha mpunga kuwa
cha faida ni muhimu wakulima kuzingatia mbinu hii muhimu na kuachana na kilimo
cha kiholela kwa kumwaga mbegu moja kwa moja shambani. Aidha kwa wakulima
wanaofuata kanuni hii wamepata mafanikio makubwa.
Faida zinazopatikana kwa kupandikiza mpunga
• Mkulima huweza kuchagua miche bora na mizuri ikiwa
kitaluni.
• Miche hukua haraka na yenye afya .
• Kiasi kidogo cha mbegu huhitajika.
• Mavuno huwa mengi.
Njia za kupandikiza miche ya mpunga
Zipo njia kuu mbili za kupandikiza miche ya mpunga, nazo ni:
• Kupandikiza kwa mistari
• Kupandikiza bila ya kufuata mistari (Mchaka mchaka).
Aidha kati ya njia hizi mbili, njia ya kupanda kwa mistari
ndiyo inayopendekezwa.zaidi. Pamoja na kwamba upandikizaji wa mistari unahitaji
nguvu kazi zaidi, njia hii imeonyesha kuwa na mafaniko mengi ikilinganishwa na
kupandikiza kiholela. Shamba lililopandwa kwa mistari ni rahisi kupalilia kwa
kutumia kipalizi cha kusukuma kwa mkono. Pia ni rahisi kwa mkulima
kupanga idadi ya mashina/mimea kwa eneo kwa uchagua nafasi aitakayo itakayompa
mazao mengi.
Uandaaji wa miche
Kabla ya kupandikiza miche shambani ni muhimu kufanya
maandalizi yafuatayo:
• Inashauriwa kumwagilia miche kwanza ili kupata urahisi wa
kungo’a
• Ili kuzuia miche isikatike ovyo, miche ing’olewe kwa
kushikwa chini zaidi ya shina
• Epuka kung’oa miche mingi kwa wakati mmoja
• Miche ifungwe kwenye mafungu madogo madogo ili kurahisisha
usafirishaji na upandikizaji shambani
• Miche bora tu ndio ichaguliwe. Sifa za miche bora
• Iwe na kimo kinacholingana,
• Iwe na majani mafupi yaliyosimama, yenye mizizi mingi na
yenye afya, isiyoshambuliwa na wadudu wala magonjwa,
Jinsi ya kupandikiza miche
• Miche ishikwe kwa vidole vitatu kama inavyoosha kweye picha
chini
• Pandikiza kati ya miche 2 -3 kwa kila shina
• Kwa mafanikio zaidi, miche ipandikizwe katika kina cha
sentimita 2-3
KILIMO BORA CHA MPUNGA CHA UMWAGILIAJI
Reviewed by BENSON
on
November 04, 2017
Rating:
No comments