KILIMO BORA CHA UFUTA
Ufuta ni zao linalolimwa kwa wingi katika mikoa ya Lindi,
Mtwara, Ruvuma, Pwani, Morogoro, Dodoma, Tanga na ukanda wa chini katika mikoa
ya Rukwa na Mbeya. Zao hili hulimwa kwa ajili ya chakula na biashara. Mbegu za zao
hili huwa na wastani wa mafuta kiasi cha asilimia 45.
MAMBO YA KUZINGATIA WA KATI WA KUZALISHA MBEGU
1. Chagua aina ya mbegu inayotoa mazao mengi na bora, inayovumilia mashambulizi
ya magonjwa na wadudu, inayokomaa mapema
na kutoa mafuta mengi.
2. Chagua mbegu inayokomaa kwa pamoja ili kurahisisha uvunaji na pia kuepuka
upotevu wa zao shambani.
3. Aina nyeupe ya mbegu
ya ufuta hupendelewa zaidi kuliko aina nyeusi.
UPANDAJI
Panda mbegu nusu inchi chini ya udongo, inchi sita umbali wa mbegu na mbegu na
futi mbili nafasi ya msitari na msitari, kabla ya kupanda hakikisha ardhi
imelowana vya kutosha na upande mbegu masaa mawili au matatu baadae
MBOLEA
Ufuta unahitaji rutuba ya kutosha ili kutoa mazao bora. Katika kudumisha rutuba
ya udongo, tumia kilimo cha mzunguko wa mazao au weka mbolea za asili pale
inapobidi.
PALIZI
Dhibiti magugu kwa kupalilia ili kuruhusu ufuta kutumia vizuri unyevu na
virutubishi. Magugu mengine huwa ni maficho ya wadudu waharibifu wa zao la
ufuta.
MAGONJWA NA WADUDU
Ufuta hushambuliwa na magonjwa na wadudu mbalimbali ambao huweza kusababisha
upungufu na ubora wa mazao. Hivyo kagua shamba mara kwa mara hasa kwenye maua
na mapodo ili kuona dalili za mashambulizi. Endapo kuna dalili zamashambulizi,
chukua tahadhari mapema kabla ya uharibifu mkubwa haujatokea.
MAANDALIZI KABLA YA KUVUNA
1. Kagua shamba kuona kama ufuta
umekomaa, Ufuta hukomaa, kati ya miezi
mitatu na minne tangu kupanda kutegemea
aina.
2. Aina ya ufuta usiokuwa na
matawi hukomaa mapema kuliko ile yenye matawi.
3. Ni muhimu kuwahi kuvuna ili kuepuka ufuta kupukutikia shambani.
DALILI ZA KUKOMAA UFUTA SHAMBANI
• Kwa kawaida majani hubadilika rangi kutoka kijani na kuwa ya manjano na
hatimaye kudondoka.
• Mashina hubadilika rangi kutoka kijani na kuwa ya kahawia.
VIFAA VYA KUVUNIA
• Kamba
• Siko
• Panga
VIFAA VYA KUKAUSHIA
• Sehemu ya kukaushia yenye Sakafu ya saruji
• Maturubai
• Sakafu safi
KUVUNA
1. Vuna ufuta mapema kabla mapodo kukomaa sana na kuanza kupasuka na kuachia
punje.Mapodo ya ufuta yaliyokomaa sana yakiguswa au kutikiswa na upepo hupasuka
na kuachia mbegu, hali inayosababisha upotevu mkubwa.
2. Mbegu za ufuta ni ndogo na zikidondoka chini ni vigumu kuziokota.
Vilevile mbegu zilizodondoka ni vigumu kuzitenganisha na uchafu.
3. Kwa aina za ufuta zenye mapodo yanayopasuka, uvunaji ufanyike wakati mimea
bado ni kijani ili kuepuka upotevu wa mbegu.
4. Aidha uvunaji ufanyike wakati hakuna upepo wala jua kali.
5. Baada ya kukata mashina yafunge katika mizigo midogo na kuweka katika
vyombo vya kusafirisha kama vile mikokoteni, matela au magari hadi sehemu ya
kukaushia.
6. Panga mizigo midogo kwa kusimamisha katika malundo madogo yasiyozidi mizigo
minane kwenye sehemu safi za kukaushia.
KUKAUSHA
Mapodo ya ufuta hukaushwa yakiwa yamefungwa katika vitita. Vitita huwekwa kwa
kuegeshwa kwenye fremu ya kukaushia kwa muda wa wiki mbili hadi tatu kutegemea
hali ya hewa. Fremu hii huwekwa juu ya turubai au sakafu ili kuzuia upotevu wa
punje kutokana na kupasuka kwa mapodo.
KUPURA
Upuraji hufanyika kwenye turubai, mkeka au kwenye sakafu safi.
• Vitita hupigwa taratibu kwa kutumia mti au hutikiswa vikiwa vimegeuzwa
vichwa chini ili kuruhusu punje za ufuta kudondoka kwenye sakafu safi au
turubai.
KUPEPETA NA KUPEMBUA
Kupepeta na kupembua hufanywa ili kuondoa takataka kama vile mawe, vipande vya
mapodo,vijiti na vumbi. Njia bora ya kupepeta na kupembua ni kwa kutumia
mikono.
Ufuta huwekwa kwenye vyombo kama vile ungo kwa kiasi cha kilo
mbili hadi tatu. Ufuta hurushwa hewani kwa kasi ndogo na takataka nyepesi
huchukuliwa na upepo. Zile nzito huondolewa kwa mikono.
KUFUNGASHA
Mbegu za ufuta zilizo safi huwekwa kwenye vifungashio kama vile magunia madogo
ya aina ya juti ya ujazo wa kilo 50. Fungasha mbegu za ufuta kwenye magunia
yenye uzito usiozidi kilo 50. Kabla ya kufungasha hakikisha mbegu zimekauka
hadi kufikia unyevu wa asilimia 10.
KUHIFADHI
• Panga magunia ya ufuta juu ya chaga.
• Panga kwa kupishanisha ili kuruhusu mzunguko wa hewa kati ya magunia.
KUSINDIKA MBEGU ZA UFUTA
Ufuta husindikwa kupata bidhaa ya mafuta ambayo hutumika katika mapishi
mbalimbali. Mafuta hukamuliwa kwa kutumia njia za asili na kwa kutumia mashine.
Njia za asili zina ufanisi mdogo ukilinganisha na zile za kukamua kwa mashine,
hivyo ni vyema kutumia mashine. Kuna mashine za aina mbili zinazotumika kukamua
mafuta; mashine za mkono na zile zinazoendeshwa kwa injini au mota ya umeme.
Mashine za mikono zinazotumika zaidi hapa nchini ni za aina ya daraja (Bridge
press) na Ram.
MATUMIZI
Mafuta ya ufuta hutumika katika mapishi mbalimbali ili kuongeza
ladha. Pia husaidia kuleta nguvu na joto mwilini. Mbegu za ufuta huchanganywa
na vyakula mbali mbali kama mikate, keki, mboga na kadhalika.
KILIMO BORA CHA UFUTA
Reviewed by BENSON
on
August 01, 2017
Rating:
No comments