ZIJUE KANUNI BORA ZA UFUGAJI BORA WA KUKU







Watu wengi hapa nchini hujihusisha na ufugaji wa kuku kwa lengo la kujipatia chakula na kipato. Mazao yatokanayo na ufugaji wa kuku ni pamoja na mayai, nyama, mbolea na manyoya kwa matumizi mbalimbali. Mifumo ya ufugaji kuku ambayo hutumika hapa nchini ni huria, nusu huria na shadidi. Ufugaji wa kuku utakuwa endelevu na wenye tija kwa kufuata kanuni za ufugaji bora zifuatazo:-
      Kufuga kuku  kwenye banda bora,
      Kuchagua kuku bora wa kufuga,
      Kutunza na kulisha kuku kulingana na hatua mbalimbali za ukuaji
      Kudhibiti na kutibu magonjwa ya kuku 
      Kutunza kumbukumbu.

1  Banda la Kuku
Kuku huhitaji banda bora ili wasiathirike na madhara mbalimbali. Banda bora la kuku linatakiwa kuwa na sifa zifuatazo:-
      Imara, lenye uwezo wa kuwahifadhi kiafya na pia dhidi ya hali ya hewa hatarishi kwa mfano jua kali, upepo, baridi na mvua pamoja na wanyama hatari,
      Lenye mwanga, hewa na nafasi ya kutosha inayoruhusu usafi  kufanyika kwa urahisi,
      Lijengwe sehemu yenye mwinuko isiyotuama maji, isiyo na upepo mkali na iwe mbali kidogo na nyumba ya kuishi watu,
      Liwe na vichanja kwa ajili ya kuku kupumzika na kulala 
      Liwe na sehemu ya kuwekea chakula, maji, kutagia, kuatamia na sehemu ya kulelea  vifaranga,
      Liwe  na nafasi ya kutosha kulingana na idadi ya kuku na kuweka  vyombo vya chakula na maji,
      Kwenye mazingira ya joto banda liwe la  ukuta mfupi na sehemu ya  kubwa  wazi yenye wavu hadi kufikia kwenye paa
      Kwenye mazingira ya baridi banda liwe na ukuta mrefu unaokaribia paa na sehemu ndogo tu iwe wazi yenye wavu ili kupitishia hewa na mwanga.

1.1   Vifaa Vinavyotumika  kwa  Ujenzi wa Banda
Vifaa vya kujengea banda vizingatie gharama na upatikanaji wake katika eneo husika. Baadhi ya vifaa hivyo ni kama ifuatavyo:-
      Sakafu  -  Saruji, udongo, mbao, mianzi au fito
      Kuta      -  Fito, mabanzi, mbao, nguzo mianzi, udongo, matofali, mawe, mabati na wavu
      Paa      -   Nyasi, makuti, majani  ya migomba, mabati na vigae.
      Wigo    -    Matofali, mbao, fito nguzo, mabanzi,  mianzi,matete, wavu na mabati

1.2   Ukubwa wa Banda
Ukubwa wa banda utategemea idadi ya kuku na aina ya kundi la kuku. Kuku wanahitaji nafasi tofauti kutegemea umri, aina na njia ya ufugaji. Eneo la mita moja ya mraba linatosha kwa vifaranga 16 wa umri wa wiki 1 – 4. Hivyo banda lenye mita za  mradi 16 linaweza  kulea vifaranga  320 hadi wiki 4. Baada ya wiki 4 eneo hili liongezwe kutegemea  aina ya kuku na njia inayotumika katika ufugaji kama inavyoonekana kwenye jedwali Na. 10

Jedwali Na 10: Eneo Linalohitajika Kufuga Kuku Kwenye Sakafu ya Matandazo Kutegemea na Umri na Aina ya Kuku

Umri wa Kuku
Idadi ya Kuku kwa mita 1 ya mraba 
Kuku  wa  mayai 
Kuku wa nyama
Siku 1 hadi wiki 4
18
18
Wiki ya 5 hadi ya 8
9
9
Wiki ya 9 hadi 20
6
-
Wiki 21  kuendelea
3-4
-

           Angalizo:
Mabanda yanayozungushiwa wigo kama ilivyo katika mfumo wa nusu huria, kuku mmoja huhitaji eneo la wazi lenye ukubwa wa mita za mraba 10. Mfano, kuku  100 huhitaji eneo la mita za mraba  1000

1.3   Vifaa na Vyombo Muhimu
Mfugaji anashauriwa kutumia vifaa na vyombo maalum ili kurahisisha na kuboresha  utunzaji wa makundi mbalimbali ya kuku. Vifaa na vyombo vinavyohitajika kwa ajili ya kuwekea chakula na maji, kutagia mayai na kupumzika vinapatikana kwenye maduka ya pembejeo za mifugo. Aidha, mfugaji anaweza kutengeneza mwenyewe kwa kutumia malighafi zilizopo kwenye mazingira yake.

2              Uchaguzi wa Kuku Bora wa Kufuga
2.1          Kuku wa Asili
 Aina za kuku wa asili wanaopatikana  hapa nchini ni pamaja na Kuchi (Kuza), pori  (Kishingo), Njachama, Kinyavu, Mbuni na Tongwe (Msumbiji). Mfugaji anaweza kuongeza  uzalishaji kwa kuchagua kuku mwenye sifa zifuatazo:-
      Uwezo wa kutaga  mayai mengi (kati ya 15-200 katika mzunguko mmoja wa utagaji  (Jedwali Na 11),
      Uwezo wa kuatamia na kuangua vifaranga wengi, Uwezo wa kustahimili  magonjwa
      Umbo kubwa na kukua haraka.

Jedwali Na 11: Masuala ya Kuzingatia Wakati wa Kumchagua Kuku Mtagaji Asili
Viungo vya mwili
Sifa
Macho
Maangavu, yenye wekundu kwa mbali na makubwa yamejaa kwenye soketi za macho.
Mdomo
Wenye rangi ya njano kwa mbali
Kisunzu/Upanga
Chekundu, Laini,kimelala kidogo upande na kinang’aa
Shingo
Iliyosimama
Umbali kati ya kidali na nyonga
Upanga wa vidole 3-4 vya mpimaji
Upanga wa nyonga
Upana wa vidole 3 vya mpimaji

   
2.2          Kuku wa Kisasa
Kuku bora  wa kisasa kwa ajili ya mayai au nyama ni mwenye sifa zifuatazo:-
      Uwezo wa kuanza kutaga  wakiwa na umri mdogo (miezi 5-6) kutegemea na koo,
      Umbo  kubwa na anayekula haraka (kilo 1.5-2.0 kwa kipindi cha wiki 8-120 kutegemea na koo kwa kuku wa nyama,
      Anayetaga mayai mengi (250 au zaidi) kwa kuku wa mayai kwa mwaka; na
      Awe na uwezo wa kutaga katika umri wa miezi 6-8.

2.3          Uchaguzi wa Jogoo Bora wa Mbegu
              Jogoo wa mbegu anatakiwa awe na sifa zifuatazo:-
      Achaguliwe kutoka kwenye koo zenye sifa ya kutaga mayai mengi,
      Mrefu, umbo kubwa, miguu imara na yenye nguvu,
      Awe machachari, ushawishi kwa mitetea na ari ya kupanda
      Uwezo wa kupanda akiwa na umri wa miezi 7-10.

    3 Mayai kwa Ajili ya Kutotoa Vifaranga

  3.1   Uchaguzi wa Mayai

                Mayai kwa ajili ya kutotoa vifaranga yawe na sifa zifuatazo:-
      Yaliyorutubishwa na jogoo,
      Yasiwe na nyufa,
      Yasiwe na maganda tepetepe,
      Yasiwe na kiini kilichovunjika,
      Yawe na ukubwa wa wastani; na
      Yasiwe yamekaa zaidi ya wiki 2 baada ya kutagwa.

3.2 Utunzaji wa Mayai

Mayai ya kienyeji kwa ajili ya kutotoa vifaranga yatunzwe kwa kusimamishwa wima sehemu iliyochongoka ikiwa imeangalia chini kwa siku 3 za mwanzo na kisha yageuzwe ili sehemu iliyobutu iangalie chini. Mayai yahifadhiwe kwenye sehemu iliyo na ubaridi kidogo na giza.
         
 4. Utunzaji wa Kuku kwa Makundi

 1. Utunzaji wa Vifaranga

Malezi bora ya vifaranga ni muhimu katika ufugaji wa kuku kwa sababu  vifaranga hawana uwezo wa kustahimili mazingira wakiwa wenyewe mara wanapoanguliwa.Ukosefu wa malezi bora  husababisha vifaranga kuwa dhaifu,kufa kwa wingi na hivyo kupunguza idadi ya kuku wa baadaye. Malezi ya vifaranga yanaweza kufanyika kwa kutumia kuku walezi au kutumia vifaa maalum.

Kulea Vifaranga kwa Kutumia Kuku Mlezi

   Vifaranga wanaweza kulelewa na mama yao au kuku mlezi. Endapo kuku wengi wametotoa vifaranga kwa wakati mmoja, achaguliwe kuku mlezi aliye na uwezo wa kulea vifaranga wengi  kati ya waliototoa aendelee kulea na wengine waliototoa waachwe huru ili warudi kwenye mzunguko wa kutaga. Kuku mmoja anaweza kulea vifaranga 20 hadi 25. Mfugaji wa kuku,pamoja na kanuni nyingine, anapaswa kuzingatia yafuatayo:-
      Kuku anayelea vifaranga atengewe chumba maalumu, apewe maji ya kutosha na chakula chenye virutubisho muhimu,
      Vifaranga wasiachiwe kutoka nje hadi watakapofika umri wa wiki 6,
      Vifaranga watengwe na mama/mlezi baada ya wiki 4 kuruhusu mama aendelee na mzunguko wa kutaga;na
      Katika maeneo yenye hali ya hewa ya ubaridi vifaranga  wacheleweshwe  kutenganishwa na mama/mlezi hadi wiki ya 6 au mpaka  waonekane  wameota  manyoya  ya  kutosha

 Kulea Vifaranga kwa  Kutumia Bruda    

   Bruda ni chombo/sehemu iliyoandaliwa mahusus kwa ajili ya kuwapatia joto vifaranga badala ya mama/mlezi. Mfugaji anaweza kulea vifaranga wengi kwa kutumia bruda ambayo ni mduara unaweza kutengenezwa kwa kutumia mbao, karatasi ngumu au kwa kuziba pembe za chumba.Aidha, njia hii hupunguza vifo vya vifaranga vinavyosababishwa na ndege au wanyama hatari,huruhusu kuku kutaga mapema zaidi na kuwa na mizunguko mingi ya utagaji (kwa kuku wanaoatamia). Vilevile, hurahisisha udhibiti wa magonjwa.
Mfugaji anapaswa kufuata taratibu zifuatazo katika kulea vifaranga kwa kutumia bruda:-
      Kuweka vifaa vya kuongeza joto kwa mfano taa ya umeme, chemli au jiko la mkaa. Zingatia kiwango cha joto kinachohitajika katika bruda.
Wiki ya  kwanza ni 35oc, wiki ya pili ni 33oc, wiki ya tatu ni 31oc na wiki ya nne  ni 29oc,
      Kuchunguza mtawanyiko wa vifaranga ndani ya bruda ili kutathimini hali ya joto.Wakijikusanya kwenye chanzo cha joto, inaashiria kuwa baridi imezidi hivyo joto liongezwe. Wakiwa mbali na chanzo cha joto maana yake joto limezidi hivyo joto lipunguzwe,
      Bruda iwe na sakafu yenye malalo yatokanayo na maranda ya mbao au pumba za mpunga. Malalo yabadilishwe endapo yataonekana yameloana,
      Bruda  iwekwe vifaa vya maji na chakula. Maji na chakula kiwekwe kabla ya kuweka vifaranga,
      Vifaa vya joto viwekwe ndani ya bruda masaa 6 kabla ya kuingiza vifaranga,
      Vifaranga walishwe chakula cha kuanzia gramu 12-15 kwa kipindi cha wiki ya 2. Katika wiki ya 3 wapewe gramu 21-35 kwa kifaranga na chakula hicho kiwepo muda wote,
      Vifaranga wapatiwe vitamin, madini na dawa za kinga (antibiotics); na
      Vifaranga wapatiwe chanjo kulingana na maelekezo ya mtaalamu wa mifugo.Chanjo dhidi ya magonjwa muhimu kwa mfano,Marek’s (mara anapototolewa), Mdondo (siku ya 3-4 na kurudiwa baada ya siku  ya 21 na kila baada ya  miezi 3) na Gumboro (siku ya 7na kurudia tena siku ya 21).Wapatiwa dawa ya minyoo (wiki ya 8) na coccidiosis(wiki ya 3-4). Siku ya 45 wapewe chanjo ya ndui ya kuku.
   2. Kutunza Kuku Wanaokua (Wiki 8-18)
 Utunzaji wa kundi hili unategemea mfumo unaotumika.

Kuku  Wanaofugwa Katika Mfumo Huria

Kuku  wanaofugwa katika mfumo huu wapatiwe matunzo bora yakiwemo yafuatayo;
      Wapewe chakula cha ziada asubuhi kabla ya kutoka na wanaporudi kwenye banda. Chakula hicho kinaweza kugawanywa  mara ya 2 kwa  siku,
      Wapatiwe maji safi na ya kutosha wakati wote
      Wapatiwe chanjo na dawa kulingana na ushauri wa mtaalam wa mifugo. Wiki ya kumi warudie chanjo ya mdondo, wiki ya 12 kuhara (fowl cholera), wiki ya 14 ndui ya kuku,

Kuku Wanaofugwa Katika Mfumo Shadidi

      Majogoo watenganishwe na mitetea katika  wiki 7 hadi 10 ili kuzuia uzaliano usio na mpangilio,
      Wapewe chakula cha kukuzia kuanzia wiki ya 8-15 gramu 55-60 na kuanzia wiki ya 16 gramu 65-80 kwa wanaofugwa mfumo huria na gram 120-125 kwa kuku kwa siku kwa wanaofugwa mfumo wa shadidi,
      Kuku wa nyama wapatiwe chakula cha kuku wa nyama muda wote,
      Wapatiwe maji safi ya kunywa  kwa muda wote kwenye vyombo safi,
      Kuku wachunguzwe dalili zozote za ugonjwa ili waweze kupata tiba sahihi kutoka kwa mtalaamu wa mifugo,
      Kuku wa wiki 9-20 wanahitaji nafasi ya mita za mraba 0.15 kwa kuku na wiki 21 au zaidi mita za mraba 0.2 kwa kuku, 
      Kuwe na vyombo maalum vya kutosha kwa ajili ya chakula na maji,
      Wafanyiwe usafi wa banda mara kwa mara ili kuzuia magonjwa yanayotokana na uchafu
      Wakatwe midomo ili kuzuia kudonoana.

3. Kuku Wanaotaga

       Mahitaji ya kuku wanaotaga ni tofauti na makundi mengine.
       Mambo ya kuzingatia kwa kuku wanaotaga  ni pamoja na:-  
   Banda liwe na viota vya kutagia mayai (kiota 1 kwa kuku 3-5).Viota viwekwe bandani mara kuku watakapofikisha  umri wa wiki 18 ili waanze kuzoea kuvitumia,
   Wapatiwe chakula na maji safi wakati wote kwa kutumia vyombo maalum ambavyo ni visafi,
   Kuku  wasiotaga waondolewe kwenye kundi.Kuku hao huonekana wasafi na sehemu ya kutolea yai huwa ndogo na kavu,upanga wake kichwa (comb) huwa mdogo na mwekundu,
   Wapatiwe dawa ya minyoo kila baada ya miezi 3,
   Wawekewe fito au ubao mwembamba kama sehemu ya kupumzikia na mazoezi ili kuzuia kudonoana,
   Mayai yakusanywe mara 4 au zaidi kwa siku ili yasidonolewe na kuku,
   Kuwe na malalo makavu na yabadilishwe mara yanapochafuka,
   Vyombo vifanyiwe usafi kila ili kuzuia magonjwa; na
   Watundikiwe majani mabichi aina ya mchicha,papai, alfaafa,majani jamii ya mikunde ili kuboresha lishe.

Udhibiti na Tiba  Dhidi ya Magonjwa ya Kuku

    Kuku wanaopata lishe bora, kutunzwa  vizuri na kupatiwa chanjo dhidi ya magonjwa yanayotokea mara  kwa mara huwa na afya nzuri. Ni bora kuzuia magonjwa kuliko kutibu ili kupunguza vifo na gharama. Iwapo ugonjwa utatokea kuku wagonjwa watenganishwe  na kuku wasio wagonjwa na wapatiwe tiba. Kanuni muhimu za kufuata ili kuzuia magonjwa ni:-
      Banda liwe  safi muda wote,
      Kabla ya kuweka kuku, banda  linyunyuziwe  dawa ya kuua wadau wa magonjwa mbalimbali,
      Kuku wakaguliwe kila siku ili kubaini wagonjwa au wenye matatizo, kuwatenga na kutoa  taarifa kwa mtaalam wa mifugo,
      Kuku wapatiwe chanjo dhidi ya magonjwa mbalimbali,
      Watu wasiohusika wasiingie eneo la kufugia kuku bila utaratibu,
      Ndege na wanyama wengine wasifike eneo la kufugia kuku,
      Banda la kufugia kuku litenganishwe na mabanda ya mifugo mingine,
      Lango la kuingia katika banda la kuku liwekewe dawa ya kukanyaga kwa wanaoingia ndani ili kuzuia kuingiza vimelea vya wadudu wa magonjwa;na
      Vifaa vya chakula na maji viwe safi wakati wote.

Dalili za Kuku Mgonjwa

     Dalili za ujumla zinazoonekana kwa kuku mgonjwa ni kama zifuatazo:-
      Kuzubaa,
      Kupoteza hamu ya kula,
      Kujitenga na wenzake katika kundi; na
      Kupunguza au kusimama kutaga.
      Mfugaji anapoona mojawapo ya dalili hizo atoe taarifa kwa mtaalum wa mifugo

 Ufugaji wa Aina Nyingine za Ndege

   Aina ya ndege wengine wanaofugwa hapa nchini ni pamoja na Bata maji,Bata bukini, Bata bukini, Kanga na Njiwa. Ndege hao hufugwa kwa kiasi kidogo ukilinganishwa na kuku kwa kuwa soko lao ni dogo.Utunzaji wao hautofautiani sana na kuku;
      Wajengewe banda la kuishi ambalo ukubwa wake utagemea idadi ya ndege wanaofugwa,
      Wapatiwe chakula chenye virutubisho na maji ya kunywa yakutosha,
      Wapatiwe kinga na tiba dhidi ya magonjwa,
      Bata maji na Bata bukini wajengewe bwawa lenye nafasi ya kukutosha kwa ajili ya kuogelea; na
      Njiwa wajengewe viota sehemu ya juu kama kwenye mapaa ya nyumba.

Utunzaji wa Kumbukumbu

Utunzaji wa kumbukumbu ni muhimu sana katika ufugaji wa kuku na ndege wengine wafugwao ili kusaidia mfugaji kujua maendeleo ya ufugaji wake. Utaratibu wa kuweka kumbukumbu mara tukio linapotokea ni lazima ili kuepuka kusahau.Mfugaji ahakikishe anaweka kumbukumbu ambazo ni sahihi na zinazoeleweka.

Aina za Kumbukumbu

     Kumbukumbu zinazopaswa kuwekwa ni pamoja na:-
      Aina na idadi ya kuku waliopo kwenye kila kundi (mfano vifaranga,wanaokua,wanaotaga,majogoo),
      Uzalishaji wa mayai kwa kundi la kuku waliopo,
      Utotoaji wa vifaranga,
      Kinga na matibabu,
      Mapato na matumizi,
      Utagaji wa kila kuku na utunzaji (kwa kuku wa asili); na
      Kumbukumbu za vifo.


Chakula na uchanganyaji wake


Chakula ndicho huchangia sana katika gharama za uzalishaji kwa zaidi ya asilimia 60. Na gharama ya chakula huongezeka kila mwaka kuliko hata gharama za mayai au kuku wenyewe.

Mfugaji anaweza kununua chakula kilichochanganywa au kuchanganya mwenyewe. Ila anapaswa kuzingatia virutubisho na viini lishe vilivyopo katika chakula hicho pia kuzingatia mahitaji ya kuku wake.

Virutubisho vinavyotakiwa ni vingi lakini vimegawanywa katika makundi sita ya vyakula ambavyo ni; protin, wanga, mafuta, madini,vitamini na maji.

Protini inahitajika kujenga mwili wa kuku. Ni muhimu kwa ukuaji wa kuku, uzalishaji wa mayai na kuimarisha afya. Wanga na mafuta vinahitajika ili kuupa mwili nguvu na joto na kuwezesha mwili kufanya kazi zake ipasavyo. Vitamini vinahitajika ili kumwezesha mwili wa kuku kufanya kazi zake vizuri. Madini yanahitajika ili kuimarisha mifupa na uzalishaji.
Uchanganyaji wa chakula

Vyakula
Vifaranga
Nyama
Nyama
kuzia 
Vifaranga
Mayai
Mayai
Kuzia
Mayai
Taga
Ng’ombe maziwa
Mahindi 
38
28
28
26
20
0
Pumba
mahindi
19
26
24
30
30
40
Pumba mpunga
15
18
24
25
30
33
Mashudu
alizeti
8
8
6
5
6
15
Soya 
4
6
6
5
6
5
Dagaa
10
7
5
3
3
0
Damu 
4
5
4
3
2
0
Chokaa mifugo
1
1
2
2
2
5
Madini
0.5
0.5
0.5
0.5
0.5
1.5
Chumvi 
0.5
0.5
0.5
0.5
0.5
0.5
Jumla 
100
100
100
100
100
100


ZIJUE KANUNI BORA ZA UFUGAJI BORA WA KUKU ZIJUE  KANUNI BORA ZA UFUGAJI BORA WA KUKU Reviewed by BENSON on January 28, 2018 Rating: 5

No comments