ZIJUE FAIDA NA HASARA ZA KILIMO CHA GREEN HOUSE.

Image result for green house
Green house, kwa tafsiri isiyo rasmi, ni nyumba kitalu. Nyumba ambayo imejengwa kukidhi mahitaji ya mimea. Nyumba hizi hujengwa kwa ustadi mkubwa wa kitaalumu kwa kuzingatia baadhi ya mambo muhimu.

Baadhi ya mambo hayo muhimu ni pamoja na hali ya hewa ya eneo husika joto, baridi, mwanga wa jua, uelekeo wa upepo, muinuko kutoka usawa wa bahari, aina ya udongo, ubora wa maji, mteremko wa eneo husika.

Lakini pia kuna mambo ya kuzingatia kama aina za malighafi za kutumika na ubora wake nailoni, neti kivuli, mbao au chuma, plastiki, upatikanaji wa maji, kufikika kwa eneo, muinuko wa jengo (Gutter height), ni muhimu kuzingatia urefu kutoka usawa wa ardhi kabla ya kuezeka green house Mazao yanayooteshwa kwenye mfumo huu yako ya aina maalumu kwa maana ya aina ya mbegu za kutumika/hybrid/F1, zenye sifa mbalimbali kama urefu, ipo namna yake ya uwekaji mbolea, kumwagilia ambazo ni njia tofauti sana na inavyofanyika katika mashamba ya wazi.

Sababu za watu kupenda kutumia aina hii ya kilimo Kwanza kabisa sababu kubwa inayowasukuma wengi kuingia katika kilimo hiki ni ile ya kutoa mavuno mengi katika eneo dogo, kwa mfano kuna taarifa ambazo huenezwa na watu kuwa unaweza kupata tani 60 za zao kama nyanya ndani ya green house kwa eneo la upana wa mita 8 na urefu wa mita 15.
Aina hii ya taarifa ni moja ya kichocheo ambacho huwavutia sana watu, kwani mtu hupiga haraka hesabu za mapato na kuona kuwa inalipa.

Pia taarifa nyingine ambazo huwatia watu faraja na matumaini juu ya kilimo hiki ni kwamba ni aina ya mfumo ambao hauna usumbufu badala yake mtu hujipatia fedha zake kwa haraka.
Ukiacha taarifa za namna hiyo pia zipo zile zinazosema kuwa ukimaliza kujenga tu jengo la Green House, basi wewe ni tajiri yaani utakuwa na kazi ya kupanda na kusubiri kuvuna tu hata kwa miaka 10 mfulululizo.

Kwa taarifa kama hizi hufanya mtu kuwaza mapato makubwa, kuwa ikiwa kwa labda miezi 3 tu nina tani 60 za nyanya kwa eneo la mraba la mita 120, na anaambiwa unavuna tu, na jengo ni imara linadumu kwa miaka 10 bila matengenezo wala marekebisho.
Pamoja na kwamba aina hii ya kilimo imekuwa na faida lakini pia imekuwa na changamoto zake zinazowakumba wakulima wanaotumia mfumo huu wa kilimo.

Kwa maeneo ya miji mikubwa kama, Dar es Salaam na mikoa mingine zipo baadhi ya greenhouse ambazo zimejengwa mwaka jana, lakini wamiliki wake wamezitelekeza na wengine wamezibomoa baada ya kuona wanapata mashambulizi ya magonjwa na wadudu.
Wapo baadhi ya wakulima kwa kupata taarifa zisizo sahihi waliaminishwa kuwa hakuna magonjwa wala wadudu wanaoshambulia mazao yaliyopo ndani ya green house, hivyo wakulima wakaishi kwa kujiamini kwa kujua kuwa wanachosubiria ni mapato ya tani 60.
Matokeo yake wamejikuta wanapata magonjwa na wadudu kama mazao ya shamba wazi, unakuta ni greenhouse ya nyanya lakini ndani unakuta kuna changamoto ya wadudu.
Kuna baadhi ya wakulima mazao yao yamenyauka na kufa yakiwa ndani ya green house, kuna wakulima walijenga greenhouse kwa matumaini ya kupata pesa ya haraka na wameishia kupata hasara kwa kuwa hawakupata ushauri sahihi na mazao yao yamekauka pia kama vile yapo kwenye shamba la wazi.

Mara nyingi greenhouse hizi zimekuwa kwenye eneo lenye joto kubwa ikilinganishwa kuwa kimo chake kinapaswa kuwa chini ya mita 2.5, hivyo kufanya joto kuwa kali sana na mazao kunyauka, ambapo wataalamu wanashauri kuwa ni bora zaidi kujengwa kulingana na mazingira ya eneo au mkoa husika.

Mavuno kidogo .
Wapo wakulima waliolima ndani ya green house, mbali ya kwamba walikuwa wakiaminishwa kuwa watapata mavuno mengi yatakayowafanya kurudisha gharama zao ndani ya msimu mmoja matokeo yake imekuwa kinyume kabisa (mavuno hafifu na yasiyo bora) jambo ambalo linatokana na kutozingatia kanuni bora za uandaaji wa aina hii ya kilimo.

Kukosekana kwa soko
Baadhi ya wakulima waliowekeza kwenye kilimo hiki wamekuwa wakiaminishwa kuwa kwa kuwa ni mavuno ya green house, basi yatapata soko zuri muda wowote atakaovuna, jambo ambalo ni kinyume ambapo kwa sababu hizo wamekuwa wakizalisha mazao bila ya kuwa na hofu ya kukosa soko.

Na hivyo kujikuta kwamba pindi inapofikia wakati wa mavuno imekuwa kilio kwani mazao hayo yamekuwa yakipata bei sawa tu na yale ya mashamba ya kawaida huku wakati mwingine mazao hayo yakiharibika kabisa kwa kukosa soko.
Ubora hafifu wa mazao
Kwa mujibu wa wataalamu wanabainisha kuwa mazao huwa si mazuri na kutofanana hatua zote za ukuaji.
Kwani baadhi ya wakulima waliaminishwa kuwa mazao yote yaliyomo ndani ya green house yatakuwa katika kiwango sawa na yatafanana kwa kuwa yapo katika mazingira mazuri ya aina moja.
Hivyo kumfanya mmiliki kuamini kuwa kwa kuwa ni green house ni lazima ukuaji uwe bora na mzuri, hata kama hatofanya jitihada zozote, yeye atasubiri kuvuna na kupata pesa tu.
Ili kuweza kufanikiwa kwenye kilimo hiki cha green house basi kuna mambo ya kuzingatia kabla ya kuingia katika aina hii ya kilimo.

Wataalamu wa kilimo hiki wanasema kuwa kwanza kabisa ili mtu aweze kufanikiwa basi hana budi kuhakikisha kuwa anaweka juhudi, umakini na malengo katika jambo husika, kwani unaweza kuwa na green house lakini bado ukaambulia hasara na usifaidike na chochote kinyume na matarajio yako.

Na hivyo kwa sababu hiyo ukajikuta uko sawa tu kama siyo nyuma ya yule aliyelima kilimo cha kawaida ambacho ni cha wazi.

Lakini pia jambo jingine la kuzingatia ni kuhakikisha kuwa unafahamu vizuri kilimo hiki, ikiwamo pia kutambua mbegu zilizobora na zinazoendana na soko unalolilenga kwani kinyume na hivyo unaweza kujikuta unaambulia hasara.

Hivyo ni busara kabla ya kuanza aina hii ya kilimo ni vizuri iwapo utatafuta ushauri kwa watu waliokwisha kufanikiwa kupitia mfumo huu lakini pia kutafuta taarifa mbalimbali juu ya aina hii ya kilimo.

Hii itakusaidia kujua changamoto na namna gani unavyoweza kuzikabili ikiwamo, gharama, magonjwa kwani usipokuwa makini unaweza kujikuta unakabiliana na changamoto zilizoko kwenye kilimo cha kawaida cha shamba wazi ilihali una green house.

Pia jambo jingine la kuzingatia ni kuhakikisha kuwa unafanya utafiti wa kina kabla ya kuamua kuingia kwenye aina hii ya kilimo, hii itakusaidia kuweza kulibaini soko linavyokwenda na upande na kuvuna wakati gani.


Pia hakikisha kuwa unapata fundi ambaye ni mzoefu kwenye uandaaji huu wa green house ikiwamo kujiridhisha kwanza kuhusu ubora wa kazi zake alizowahi kufanya kabla ya kuingia makubaliano ya kukutengenezea green haouse yako.
ZIJUE FAIDA NA HASARA ZA KILIMO CHA GREEN HOUSE. ZIJUE FAIDA NA HASARA ZA KILIMO CHA GREEN HOUSE. Reviewed by BENSON on January 12, 2018 Rating: 5

No comments