ZIJUE MBINU BORA YA KUOGESHA MIFUGO
Mfugaji anapoogesha mifugo yake kama vile mbuzi, kondoo,
nguruwe, ng’ombe na wengine husaidia kwa kiasi kikubwa kufanya mazingira
yanayowazunguka wanyama hao kuwa rafiki hasa kwa kuwa maficho au mazalia ya bakteria
au wadudu yanapofikiwa na dawa huwa salama zaidi.
Kuogesha mifugo
kuzuia kupe
Ili kuweza kuzuia kupe kikamilifu na hivyo kutoweza
kuwashambulia mifugo na kuwaambukiza magonjwa mbalimbali, ni muhimu kuhakikisha
kuwa wakati wa kuogesha, dawa imeenea sehemu zote za mwili wa mnyama na kwamba
imeingia hadi kwenye ngozi na kulowanisha ipasavyo badala ya kuishia juu ya
manyoya peke yake.
Nini cha kufanya kabla ya kuanza kuogesha? Kabla ya kuanza
kuogesha kama ni ng’ombe, hakikisha amefungwa vizuri au awekwe moja kwa moja
kwenye kibanio na bomba au pampu litakalotumika kupuliza dawa ifanyiwe
majaribio ili kuhakikisha kuwa inafanya kazi vizuri.
Changanya dawa ya kuogesha pamoja na kiasi maalumu cha maji
kilichopendekezwa na mtaalamu au mtengenezaji wa dawa husika.Mwogeshe
ng’ombe nje au mbali kidogo na banda mahali ambapo dawa inayotumika haitaweza
kuruka na kuingia kwenye malisho au maji ya kunywa.
Njia za kuondoa kupe mwilini
Zipo njia za zamani
na nyingine za kisasa ambazo huweza kutumika kuzuia au kuondoa kupe mwilini mwa
mnyama badala ya kuogesha. Iwapo njia hizi zitatumia vizuri na kwa umakini,
zinaweza kusaidia kupigana na magonjwa yanayoambukizwa na kupe.
Njia hizo ni mosi uondoaji wa kupe kutoka mwilini mwa
ng’ombe kwa kutumia mkono ambayo hufanywa na baadhi ya wanafamilia za wafugaji
katika baadhi ya nchi duniani. Uondoaji wa kupe kwa njia hii ni rahisi na
mazingira hayachafuliwi kwa kuwa hakutakuwa na madawa yaliyotumika.
Hata hivyo njia hii huweza kuleta madhara iwapo haitafanywa
kwa umakini na hivyo baadhi ya kupe kusalia mwilini mwa ng’ombe hasa wale
wadogo.
Mbili, Kutumia dawa ambazo humwagwa mgongoni mwa mnyama kwa
mchirizo kuanzia kichwa hadi kwenye shina la mkia. Licha ya kuzuia kupe, dawa
za aina hii hufukuza pia mbung’o, inzi na wadudu wengine wanaoweza kusumbua
ng’ombe.
Dawa za aina hii zinaweza kutumiwa mara moja tu katika
kipindi cha majuma mawili tofauti na zile za kuogesha ambazo mfugaji huhitajika
kuwanyunyizia ng’ombe mara moja au mbili kwa juma kufuatana na wingi wa kupe
katika eneo lake.
Baadhi ya wafugaji pia hutumia dawa za kupaka
zilizotengenezwa kwa pareto kama vile py-grease kwa ajili ya kufukuza inzi na
vile vile kuzuia au kuua kupe.
Uzuiaji wa kupe utafanywa zaidi iwapo dawa hizi zitapakwa
kwenye sehemu zinazofahamika kushambuliwa zaidi na kupe kama vile eneo la
kuzunguka masikio, chini ya shina la mkia na kati ya miguu na kiwiliwili.
Tatizo mojawapo la matumizi ya dawa hizi ni kwamba kupe huweza kujishika sehemu
ambazo kwa bahati mbaya dawa haikupakwa.
Zaidi ya hayo, katika maeneo yenye kupe wengi, inashauriwa
kutokutumia dawa za aina hizi pekee kama kinga ya kuzuia kupe.
Kuogesha ng’ombe kwenye majosho ya uma yaliyojengwa mahususi
kwa ajili ya uogeshaji huo. Faida ya kutumia majosho haya ni kwamba wafugaji
walio wengi wanaweza kuogesha ng’ombe au mifugo yao kila mara bila gharama
kubwa ambazo zingehitajika kwa ununuzi wa dawa na bomba au pampu la kuogeshea.
Pia, majosho ya kuogeshea hayahitaji marekebisho ya mara kwa
mara na matumizi yake huokoa dawa nyingi ambayo ingepotea bure kama vile
mfugaji angetumia bomba au pampu kuogeshea wanyama nyumbani kwake.
Mashine za kuogeshea (spray race) pia hutumiwa na baadhi ya
wafugaji. Aidha mashine za uma ambazo pia zilikuwa zikitumika kuogesha
zimepoteza umaarufu wake kutokana na ukweli kuwa imekuwa vigumu kununua spea na
kuzifanyia matengenezo pale zinapoharibika.
Mbali na hayo, uendeshaji wa mashine hizo ni wa gharama kubwa
ukilinganisha na njia nyingine za kuogeshea kama vile majosho. Kukoroga dawa na
kutumia brashi kuogeshea. Wapo pia baadhi ya wafugaji ambao wamekuwa wakitumia
njia hii kuogesha mifugo yao kutokana na ukosefu wa fedha kwa ajili ya kununua
pampu au bomba kwa ajili ya kuogeshea na wakati mwingine kutokuwepo kwa majosho
maalumu ya kuogeshea katika maeneo yao.
Baadhi ya wafugaji pia hukwepa moja kwa moja gharama za
uogeshaji na kubaki kujiandaa vyema kwa ajili ya kutibu mifugo yao mara tu
wanapoona dalili za maradhi kwa mifugo yao yanayotokana na kuambukizwa na kupe.
Utaratibu huu si mzuri sana kwani mara nyingine huweza
kusababisha kutokea kwa vifo vya wanyama kwa wingi na kwa ghafla kutokana na
gharama za madawa na hata malipo kwa wataalamu wa mifugo watakaotumika kutibu
mifugo hiyo.
Njia zingine za
asili zinazoweza kutumika kuzuia kupe
Moja, tumia unga wa diatomite, ambao ni unga mweupe
unaotokana na diatomaceous kudhibiti kupe. Chembechembe zake kali husambaa
katika mwili wote wa mdudu na kunyonya majimaji yote mwilini.
Kukosekana kwa maji mwilini husababisha mdudu kufa. Kutokana
na sababu kuwa unga huo husambaa katika mwili wote na kunyonya maji yote, ni
vigumu kwa mdudu kujitengenezea kinga kwa wakati huo na ndiyo maana hufa.
Mbili, chukua gramu 250 za maua yaliyokauka ya pareto, weka
kiasi kidogo cha maji kisha tia kwenye kinu na twanga. Baada ya kumaliza, weka
maji hadi kufikia lita 10 na chemsha kwa dakika 20. Epua na uiache kwa muda wa
saa 12 kisha nyunyizia mifugo yako.
Tatu unaweza kuchukua gramu 250 za maua ya pareto
yaliyokauka, weka maji lita 10 , peleka katika chumba cha giza na uache kwa
muda wa saa 12 kisha tayari kwa kutumia kuitibu mifugo yako.
Nne, chukua kilo moja ya majani mabichi ya tumbaku, tumbukiza
katika maji lita 10 kisha iache kwa muda wa dakika tatu.
Chukua kitambaa safi na tumia kumpaka ng’ombe. Kwa ng’ombe
mmoja, lita 5 zinatosha.
SOURCE; MWANANCHI
By Patrick Jonathan
ZIJUE MBINU BORA YA KUOGESHA MIFUGO
Reviewed by BENSON
on
November 27, 2017
Rating:
No comments