YAJUE MATUNZO SAHIHI KWA KUKU WANAOTAGA.
Kwa kawaida kuku huanza kutetea(Kutoa mlio wa ishara ya
kutaga) anapofikisha miezi sita hadi minane. Hivyo ni vyema viota viandaliwe
mapema wakiwa na umri wa miezi mitano. Kuku anapoanza kutaga akifikisha mayai
matatu mfugaji anashauriwa kuondoa kila yai linalozidi hayo matatu kila siku
linapotagwa na kuliweka alama ya tarehe au namba kwa kutumia penseli ili
kumfanya kuku aendelee kutaga kwa lengo la kufikisha mayai 15 mpaka 20. Mayai
yanayoondolewa yawekwe kwenye chombo kikavu kinachopitisha hewa ni vizuri pia
kuweka mchanga ndani ya chombo hicho.
Pia katika kufuga kuku wanaotaga
unatakiwa kufanya yafuatayo.
1. Sehemu iliyochongoka katika yai iwe chini, aehemu pana ya yai
iwe juu.
2. Hifadhi sehemu yenye hewa ya kutosha na isiyohifadhi
joto
Mayai yasikae kwenye hifadhi hiyo zaidi ya wiki mbili toka siku ya kuanza
kutagwa.
Uatamuaji wa mayai na uanguaji wa viwanda.
Uatamiaji na uanguaji wa kubuni - Mfumo huu hutumia mashine za kutotoleshea
vifaranga (Incubators) hutumika kuangua mayai mengi kati ya 50 hadi 500 kwa
wakati mmoja Mashine zinazotumika kutotoleshea vifaranga wa kisasa zinaweza
kutumika pia kutotoleshea wa kienyeji.
Uatamiaji na uanguaji wa asili
KUCHAGUA MAYAI YA KUANGUA.
Hili nalo ni muhimu kuzingatia. Ni vizuri
kuchagua mayai ya kuatamia ili mayai yasiyofaa yaweze kuuzwa au kutumiwa
nyumbani kwa chakula. Mayai ya kuatamia yawe na sifa zifuatazo
1. Yasiwe na uchafu yawe masafi
2. Yasiwe na nyufa
3.Yatokane na kuku aliyepandwa na jogoo
4. Yasiwe madogo wala makubwa bali yawe na ukubwa wa wastani kulingana na
umbile la kuku.
5. Yasiwe mviringo kama mpira pia yasiwe na ncha kali sana.
6. Yasiwe yamekaa muda mrefu zaidi ya wiki mbili toka yalipotagwa
7. Yasiwe yaliyohifadhiwa kwenye sehemu yenye joto.
KUMTAYARISHA KUKU WA KUATAMIA
Pamoja na matayarisho hayo zingatia kumuwekea mayai yasiyozidi 15 pia ni vizuri
yasipungue 12. Kuku wanaotazamiwa kuatamia ni lazima wachunguzwe kwa makini
kabla ya kuatamia ili kuhakikisha kwamba hawana chawa, utitiri n.k. Kuwepo kwa
wadudu hao huwafanya kuku wakose raha na kutotulia kwenye viota vyao. Hali hii
husababisha kuanguliwa kwa Vifaranga wachache.
Sasa unatakiwa kufanya yafuatayo:-
1. Nyunyiza dawa ya kuua wadudu ndani ya kiota
2. Pia mnyunyuzie dawa kuku anayetarajia kuatamia
3. Weka mayai kwenye kiota huku mikono yako ikiwa imepakwa jivu ili kuepuka
kuwa na harufu kwani kuku anaweza kuyasusa.
4. Ni vizuri kuifanya kazi hii ya kumuandaa kuku anayetaka kuatamia wakati wa
usiku. Pia ifahamike kuwa kwa kawaida kuku huatamia mayai yake siku 21.
PIA JIFUNZE MBINU ZA KUATAMIA MAYAI
MENGI KWA NJIA ZA ASILI.
Iwapo una kuku wengi wanaotaga kwa wakati mmoja ni vema
ukawafanya wakaatamia na kutotoa pamoja. Unachotakiwa kufanya ni kuchagua mayai ya kuatamia ukianzia na yai la mwisho
kutaga.
Unaweza kuwaandaa kuku wako zaidi ya mmoja ili waanze kuatamia kwa pamoja na
kupata vifaranga vingi kwa mara moja kuku wa kwanza anapoanza kuatamia. Mwekee
mayai viza au ya kuku wa kisasa kwani kuku huatamia hadi mayai yanapoanguliwa
hivyo ukimuwekea mayai yasiyo na mbegu atakaa hapo muda mrefu hadi vifaranga
watoke.
UTEKELEZAJI WAKE.
Kuku anapotaga kila siku weka alama ya namba au tarehe kulinganisha na siku
anayotaga. Yanapofika mayai matatu yaondoe na muwekee mayai viza au ya kisasa
huku ukiendelea kuweka alama mayai yanayotagwa kila siku. Mara kuku anapoanza
kuatamia muongezee mayai ya uongo yafikie 8 hadi 10.
Fanya hivyo kwa kila kuku anayetaga hadi utakapoweza
kupata idadi itakayoweza kukupatia vifaranga wengi kwa wakati mmoja.
Wawekee kuku wote mayai siku moja kwa kuondoa mayai ya uongo na kuwawekea mayai
ya ukweli wakati wa usiku.
MUHIMU.
Mayai ya kuatamia yasishikwe kwa mkono ulio wazi na wala yasipate harufu za
mafuta ya taa, manukato n.k.
JIFUNZE PIA KUTAMBUA MAYAI YALIYO NA
MBEGU NA YALE YASIYO NA MBEGU.
Mfugaji anaweza kutambua mayai yaliyo na mbegu na yale
yasiyo na mbegu siku ya saba baada ya kuanza kuatamia iwapo atapima mayai kwa
kutumia box lililotengenezwa maalum pamoja na tochi yenye mwanga mkali ndani ya
chumba chenye kiza. Hii itamuwezesha mfugaji ayatumie mayai yasiyo na mbegu kwa
chakula cha familia au kuyauza.
YAJUE MATUNZO SAHIHI KWA KUKU WANAOTAGA.
Reviewed by BENSON
on
November 11, 2017
Rating:
No comments