MAGONJWA YA KUKU NA TIBA ZAKE.
Mfugaji wa kuku hana budi ajitahidi kuyazuia magonjwa
kuliko kuyaponya kwa kuwalisha kuku chakula bora, na cha kutosha. Kama
itawezekana chakula chao kichanganywe na dawa zinazotumika kwenye chakula.
Usafi wa nyumba ya kuku ni muhimu sana.
Sehemu zinazozunguka nyumba pia zisafishwe. Vyombo vya
maji , chakula na vitu vinginevyo lazima viwe safi. Kwenye milango ya nyumba za
kuku ziwekwe dawa za kuuwa wadudu wa magonjwa. Nyumba za kuku zisiruhusiwe
wageni kuingia mara kwa mara kwa sababu wanaweza kuingiza magonjwa kutoka
sehemu walizotoka.
Panya na wadudu wengine wazuiwe kabisa kuingia ndani ya
nyumba za kuku. Pamoja na usafi katika nyumba ya kuu, kuna baadhi ya magonjwa
ya kuku ambayo ni ya hatari sana kwa sababu yanapoingia huuwa kuku wengi kwa
mara moja.
Baadhi ya magonjwa ni kama ifuatavyo.
1. Mharo Mweupe ( Pullorum au Bacillary White Diarrhoea)
Dalili za ugonjwa huu ni kama
ifuatavyo:
1. Toka siku tatu hadi majuma mbili baada ya kupata vijidudu vya ugonjwa,
vifaranga huharisha kinyesi cheupe na vingi hufa.
2. Kuku wakubwa wanaotaga, hupunguza kutaga mayai ghafla na baadhi yao hufa
ghafla.
3. Mpaka sasa hakuna matibabu ambayo yanafahamika yanayoweza kutibu ugonjwa
huu. Kitu ambacho mfugaji anawezaa kufanya ni kuchoma moto
kuku wote wanaougua, na kusafisha nyumba nzima kwa dawa. Mfugaji amjulishe
haraka bwana mganga wa wanyama aliye karibu naye. Njia nzuri ya kuzuia
magonjwa, kwa mfugaji kununua vifaranga kutoka vituo vyenye sifa nzuri ya
kutokuwa na ugonjwa huu, hasa vituo ambavyo hupitisha uchunguzi wa mara kwa
mara kutafuta kama ugonjwa huu upo kwenye kutuo chao. Kituo hicho cha kuangua
vifaranga lazima kiwe kinatumia dawa za kusafisha mashine za kuangua vifaranga.
Mharo Mwekundu ( Coccidiosis au Red
Diarrhoea)
Kuku walioathiwa na ugonjwa huu huonyesha dalili zifuatazo. Kati ya majuma
manne hadi kumi hivi, baada ya kuambukizwa kuku huharishadamu , Kuku ambao wameshikwa sana na ugonjwa huu, huonekana wemedhoofika sana
na huwa kama wemavaa koti, na shingo yao huinama chini. Kuku hao hawashughuliki
kutafuta chakula wala maji, na husinzia mara kwa mara kwenye pembe za nyumba.
Vifo hutokea vingi kila siku. Kuku wakubwa ambao hawakufa hukuwa taratibu sana.
Utagaji wa mayai hucheleweshwa au hupunguzwa. Wakati mwingine kinyesi cha kuku
hao huwa na rangi ya kahawia baadaye kuwa na damu.
Ugongwa huu hupona haraka kama matibabu yaanza mapema.
Mfugaji amwone haraka bwana mganga wa wanyama aliye karibu naye, ili amshauri
dawa ambazo zinatumika, kwa sehemu mbalimbali. Uzingatiaji wa masharti ya dawa
ni jambo muhimu sana. Kuushinda ugonjwa huu kunategemea usafi wa mfugaji.
Mfugaji inampasa ahakikishe kuwa haruhusu unyevunyevu kwenye takataka
zinazowekwa ndani ya chumba kwa kulalia kuku, hasa kwenye nyumba ya kulelea
vifaranga sehemu ambazo humwagwa sana maji ovyo kuzunguka vyombo vya maji.
Sehemu hizi ni lazima zitupiwe macho mara kwa mara. Ikiwezekana vyombo vya maji
na chakula viwekwe kwenye chakula au maji.
Vifaranga wasisongamane sana kwenye chumba kidogo. Chakula
cha vifaranga kitiwe dawa ya kuzuia ugojwa huu, na hii ndio njia iliyo bora
zaidi na yenye uhakika katika kuzuia ugonjwa huu. Dawa huleta matokeo mazuri
sana iwapo itaambatana na usafi.
Magonjwa ya Kupumua ( Respiratory
Diseases )
Haya ni magonjwa ya kooni, nayo hutokana sana katika kuku waliosongamana, na
kwenye nyumba zilizojengwa vibaya. Sehemu za joto kama Tanzania magonjwa haya
ya kooni yanaweza kuzuiliwa kwa urahisi kwa kujenga nyumba zenye kupitisha hewa
ya kutosha, kwa sababu hakuna hofu ya baridi kali. Kuku wadogo wanaweza kuugua
ugonjwa huu kama kuna upepo mkali. Kwa hiyo nyumba za kulelea vifaranga
ziwekewe pazia la gunia, au vitamba au makaratasi. Vumbi lipanguswe mara kwa
mara kwenye kuta za nyumba za kuku.
Ndui ya Kuku (Fowl Pox)
Hii ni ndui ya kuku. Kuku huonekana na vipele vya rangi ya
kijivujivu, kwenye ngozi yake, hasa kwenye upanga wa kichwa. Baada ya muda
mfupi vipele hivi huwa vikubwa na kukutana na kufanya majeraha mabichi na yenye
kutoa damu . Baada ya siku kumi hadi kumi na nne hivi, majeraha haya hukauka na
kufanya makovu meusi. Kuku wanaougua wanaweza kutibiwa lakini mfugaji inampasa
atoe taarifa haraka kwa bwana maganga wa wanyama aliye karibu naye ili ampatie
dawa zinazofaa. Kuku wanaougua watengwe haraka wanapoonekana ili wasiambukize
wazima. Usafi ni muhimu katika kuzuia ugonjwa huu usitokee. Kuku wapewe nafasi
ya kutosha na wasisongamane. Ugonjwa huu unaweza kuzuiwa kabisa kwa kuchanja
dawa kuku wote mapema.
Sotoka au Ndigana ( Newcastle Disease )
Kuku walioshikwa na ugonjwa huu huwa wazembe na hutokwa na hamu ya chakula.
Shingo ya kuku hulegea na manyoya hukunjamana. Upanga na ndevu hugeuka na kuwa
na rangi ya bluu. Koo la chakula huwa kubwa na hutoa mate yanayotoa harufu
mbaya. Kuku huyu hulemewa kuvuta pumzi, na huharisha kinyesi chenye rangi ya
kijani. Kichwa cha kuku huinamia nyuma au mbele au pembeni. Kuku wengi, hasa
wachanga hufa. Ugonjwa huu haujapata dawa maalum ya kutibu. Mfugaji awatenge
kuku haraka na amwarifu mganga wa wanyama aliye karibu naye. Usafi wa nyumba na
uwanja wa kuku ni jambo muhimu sana katika uzuiaji wa ugonjwa huu. Kuku
wachanjwe dawa mapema. Kuku ambao wamepata ugonjwa huu wachomwe moto au wazikwe
kwenye shimo lenye kina kirefu kwenda chini.
Kipindupindu cha Kuku (Fowl Cholera)
Ugonjwa huu unapomjia kuku kwa nguvu, hufa ghafla. Unapomjia taratibu kuku
husinzia na manyoya yake huvurugika. Shingo huinamia nyuma. Upanga na ndevu
hupanuka. Kuku huishiwa hamu ya kula chakula, na kuharisha kinyesi cheupe.
Baadhi ya kuku huvuta pumzi kwa shida na kutoa sauti ya mkwaruzo. Mfugaji
amwarifu bwana mganga wa wanyama aliye karibu naye, na atamshauri dawa za
kutumia. Usafi wa nyumba na uwanya wa kuku ndiyo msingi wa kuzuia ugonjwa huu.
Kuku walioshikwa na ugonjwa huu watengwe haraka na baadaye wachomwe moto. Kuku
wachanjwe dawa mapema kwenye sehemu ambazo ugonjwa huu hutokea mara kwa mara.
Homa ya Matumbo ya Kuku (Fowl
Typhoid)
Kuku anapojiwa na ugonjwa huu kwa nguvu sana upanga na
ndevu zake hukunjamana. Kuku hufa ghafla japokuwa huonekana bado ana afya sana.
Ikiwa ugonjwa unamjia kwa taratibu hadi ukakomaa, upanga na ndevu hufifia na
kunyauka. Kuku huhara kinyesi cha rangi ya manjano. Hamu ya chakula humtoka,
isipokuwa hunywa maji mengi, na kuku huyo huonekana ana wasiwasi sana. Kuna
dawa nyingi ambazo zinaweza kusaidia kuponya baadhi ya kuku wakati ugonjwa huu
unapoingia.
Dawa hizi mara nyingi hutengenezwa
ili zitumiwe kwenye chakula au maji. Mfugaji amwone bwana mganga wa wanyama
aliye karibu naye ili amshauri dawa ya kutumia. Nyumba za kuku ziwekwe kwenye
hali ya usafi, na uwanja usafishwe pia. Vyombo vya maji na chakula visafishwe
kwa dawa. Kuku wanaougua wote wachomwe moto. Kuku wazima wachanjwe dawa mapema
na ikiwezekana wachunguzwe kila mmoja kuona kama wapo wenye ugonjwa huo.
Wadudu wanaokaa kwenye manyoya
Mfugaji inampasa awachunguze kuku wake mara kwa mara, ili ahakikishe kuwa kuku
wake hawana viroboto , chawa , papasi au wadudu wengine ambao ni wadogo sana
hata ni vigumu kuwaona kwa urahisi kwa macho. Wadudu hawa huwasumbua kuku na
kuwapunguzia uwezo wao wa kutoa mazao mengi ya mayai au nyama. Ni jambo la
busara kutumia dawa za wadudu ambazo hutengenezwa katika hali ya unga. Dawa
hizi hutumika kwa kuwapaka kuku au kumwagia sakafu, au kwenye masanduku ya
kutagia, au kwenye ngazi za kupumzika kuku.
Mfugaji amwone maganga wa wanyama aliye karibu naye ili
amshauri dawa zinazofaa kwa sehemu yake. Kuna baadhi ya wadudu wa kuku ambao
wanakaa kwenye miguu ya kuku na kufanya magamba miguuni. Mfugaji anaweza
kutumia mafuta ya taa kwa kupaka miguu mpaka atakapoona kuwa wadudu wote
wametoweka.
Wadudu wa tumboni
Kuku hushambuliwa na aina nyingi za minyoo ambayo huishi
tumboni na kuwanyonya damu au chakula na kuwadhoofisha, au kuwauwa kabisa. Njia
iliyo bora ya kuzuia minyoo hii ni usafi wa nyumba na uwanja wa kuku. Hali ya
kuambukiza ya minyoo ikizidi, mfugaji amwarifu bwana mganga wa wanyama aliye
karibu naye, ili amshauri dawa za kutumia.
Kudonoana manyoya, vidole, kulana wenyewe kwa wenyewe na
kula mayai
Tabia hizi mbaya za kuku hutokana na sababu nyingi mbalimbali. Sabubu mojawapo
ni upungufu wa nafasi ambayo hufanya kuku wasongamane sana. Kwa hiyo kuku
wapewe nafasi ya kutosha ya chakula maji na ya kupumzika. Kuku wanaweza
kuanzisha tabia hizi ikiwa chakula chao hakina aina zote za chakula hasa nyama
au chumvi au vitamini . Kwa hiyo njia mojawapo ya kuepukana na tabia hizi mbaya
ni kuwapa kuku chakula bora.
Wakati mwingine kuku hushawishiwa
kula mayai kutokana ukosefu wa kuondoa mayai kwenye nyumba ya kutagia, mara kwa
mara. Kwa hiyo mayai ni lazima yaondolewe kwenye nyumba za kutagia mara tatu au
zaidi kwa siku.
Uchovu wa kukaa mahali pamoja unaweza kuwafanya kuku waanze baadhi ya tabia
hizi mbaya. Wafugaji wengi wenye busara huwazuia kuku wasianze tabia hizi kwa
kuwapatia majani mabichi ambayo huwafanya wawe na mchezo wa kupoteza na kusahau
kudonoana. Majani hayo hutundikwa kwa kamba.
Njia nyingine ambazo hutumika kwa kuzuia tabia hizi mbaya
za kuku ni kuwakata midomo kwa kutumia kisu kilichopashwa moto , au chuma cha
moto wanachotumia mafundi kuungia. Ubora wa chombo kilichopashwa moto ni kwamba
mdomo wa kuku hukatwa na kuzuia damu isitoke. Kwa hiyo jeraha hupona haraka.
Kuku wakubwa na wadogo wanaweza kutumia vyombo hivi, lakini mfugaji inambidi
kukata kuku midomo kati ya majuma matatu hadi tano. Mdomo unaokatwa ni wa juu,
na ukatwe kuanzia robo hadi nusu ya mdomo. Majogoo ya kupandisha yasikatwe kwa
sababu yatashindwa kupanda.
MAGONJWA YA KUKU NA TIBA ZAKE.
Reviewed by BENSON
on
November 29, 2017
Rating:
No comments