KILIMO BORA CHA PAPAI.
Papai ni
tunda lenye ladha nzuri, na rahisi kuliwa. Aina hii ya tunda ni chanzo cha
virutubisho muhimu mwilini, ambavyo husaidia kujenga mwili. Zao hili asili yake
ni ukanda wa kitropiki ambao hauna baridi kali na joto kiasi.
Udongo
Mipapai hustawi vizuri kwenye udongo
usiotuhamisha maji. Endapo maji yakituama kwenye eneo lililopandwa mipapai kwa
muda wa siku mbili, mpapai unaweza kuoza kwa haraka na kufa. Kwa kuwa
mipapai haina mzizi mkuu, inahitaji udongo wenye rutuba ya kutosha. Halikadhalika,
zao hili halihitaji udongo wenye kina kirefu, hivyo ni muhimu kumwagilia
mipapai wakati wa kiangazi. Wakati wa mapapai kuiva kama kuna ukame basi
hali hiyo huongeza ubora wa papai ikiwamo kutooza mapema baada ya kuvunwa.
Kupanda
Mipapai ipandwe sehemu ambazo hazina
upepo mkali. Hii itasaidia mipapai kukua vizuri bila kuvunjika kwani mti wa
mpapai huvunjika kirahisi. Inashauriwa kupanda miti ya kukinga upepo kuzunguka
shamba la mipapai. Ili kuwa na tija zaidi, unaweza kupanda aina nyingine ya
miti ya matunda kama vile miparachichi, na miembe.
Hakikisha miti ya kukinga upepo inakuwa
mirefu kuzidi mipapai. Miti hiyo inaweza kutangulia kupandwa miezi kadhaa kabla
ya kupanda mipapai.
Mbegu
Kusanya mbegu toka kwenye mapapai
makubwa na yaliyo komaa na kuiva, kisha kausha mbegu vizuri kabla ya kupanda.
Inashauriwa kununua mbegu kutoka kwa wazalishaji wanaoaminika na
waliothibitishwa, ili kuwa na mazao bora zaidi na yanayoweza kukabiliana na
magonjwa.
Mbegu aina ya red royal F1, inasifika zaidi kwa
kuwa na uwezo mkubwa wa kukabiliana na magonjwa yanayoshambulia mipapai, na
huanza kuvunwa mapema zaidi, kati ya miezi 6 hadi 12. Aina hii huvunwa
mfululizo kwa miaka 5 hadi 7.
Uandaaji wa
shamba
Inashauriwa kuandaa shamba vizuri kwa
kuondoa visiki na magugu yote. Shamba lilimwe vizuri, na kuhakikisha udongo
umelainika vizuri.
Mashimo
• Chimba shimo kwa ajili ya kupanda
mpapai, liwe na kina cha sentimita 60 na upana wa sentimita 60.
• Weka mboji debe moja kisha changanya
na nusu ya udongo uliotoa kwenye shimo, kisha rudishia kwenye shimo.
• Mwagilia maji kwa kipindi cha wiki
mbili kabla ya kuotesha.
Kuotesha
Sia miche kwenye kitalu, kasha hamishia
shambani inapokuwa na urefu wa sentimita 30. Chomeka mche kwenye ardhi kina cha
kati ya sentimeta 1 – 2 chini ya udongo kwenye shimo uliloandaa. Hii itasaidia
mche kupata joto la wastani na kuepuka mche kuoza na kufa. Baadhi ya wakulima
hupenda kuotesha mipapai moja kwa moja shambani.
Endapo unapenda kufanya hivyo, zingatia haya;
• Kabla ya kupanda mbegu weka
mchanganyiko wa majivu na mbolea ya kuku au mboji sehemu unayokusudia kupanda.
Mbolea husaidia ukuaji haraka na jivu husaidia kukinga mipapai na magonjwa.
• Panda mbegu 3 – 4 kila shimo, hii ni
kwa sababu miche mingine inaweza kufa kutokana na magonjwa, kuliwa na wadudu au
ikaota mipapai dume.
Nafasi
Shimo hadi shimo, liwe na nafasi ya
mita 3, na mstari hadi mstari mita 3. Hii itasaidia miche ya mipapai kukua
vizuri bila kusongamana.
Punguza miche
Baada ya miezi 3 – 5 tangu kupanda,
mipapai itaanza kutoa maua na hapo jinsia ya mipapai itajulikana. Inapofikia
wakati huo inabidi kupunguza mipapai mingine hasa midume.
Mipapai yenye jinsi zote isizidi
asilimia 10 – 20 ya miche yote iliyopo shambani, na midume ibaki mmoja katika
kila majike 25.
Utunzaji
• Weka kilo 2 – 5 za samadi kwenye kila
mpapai kwa mwaka ili kuongeza ukuaji na uzalishaji.
• Mabaki ya mimea yanaweza kuwekwa kama
matandazo. Hii ni muhimu zaidi kipindi cha kiangazi ili kuzuia unyevu usipotee.
• Chunguza mipapai mara kwa mara ili
kuangalia kama kuna magonjwa, ing’olewe na kuchomwa au kufukiwa chini endapo
itabainika kuwa na maonjwa.
• Unaweza kunyunyiza dawa zisizo na
madhara za kukinga au kukabiliana na magonjwa ya ukungu na virusi.
Kupogoa
• Kata matawi yote yatakayojitokeza
pembeni ya mpapai. Hili lifanyike mapema kabla ya tawi kuwa kubwa.
• Ondoa mipapi yote ambayo
hayakuchavushwa vizuri na ubakize yenye afya tu.
Palizi
• Mipapai inapopandwa tu inaweza
kuwekewa matandazo kuizunguka ili kuzuia uoataji wa magugu.
• Magugu yang’olewe yakiwa machanga.
• Epuka kuchimbua sana wakati wa palizi
kwa kuwa mizizi ya mipapai huwa juu juu.
Magonjwa
Zao la papai halina magonjwa mengi sana
yanayoshambulia endapo litatunzwa vizuri. Hata hivyo kuna baadhi ya magonjwa
ambayo yamezoeleka kwenye zao hili kama vile Ugonjwa wa madoa kwenye majani (Papaya spot) na Ugonjwa wa virusi
unaojulikana kama Mozaic virus.
Mimea yenye magonjwa inaweza kung’olewa na kufukiwa ili kudhibiti ueneaji
kwenye mimea mingine.
Mavuno
Mavuno huanza mara baada ya mapapai
kukomaa na kuanza kuiva.Mavuno hutegemea na uhifadhi mzuri na huduma nzuri za
miti ya mipapai ikiwemo dawa na mbolea mara kwa mara.
KILIMO BORA CHA PAPAI.
Reviewed by BENSON
on
September 06, 2017
Rating:
No comments