UTUNZAJI SAHIHI WA BUSTANI UNA FAIDA ZIFUATAZO



Je wewe  hufurahia kutunza bustani? Huenda unanufaika hata zaidi kutokana na utendaji huo. Kulingana na gazeti moja la London (Independent), watafiti wamegundua kwamba “kutunza bustani hukusaidia kuwa na afya nzuri zaidi, hupunguza mifadhaiko, hushusha shinikizo la damu na hata kukusaidia kuishi kwa muda mrefu zaidi.”

Mhariri G. Search anasema: “Baada ya siku yenye shughuli nyingi na mambo mengi yenye kufadhaisha, kurudi nyumbani na kutunza bustani yako huburudisha sana.” Mbali na kuwa jambo lenye kuthawabisha na kupendeza, kutunza bustani kunakuwezesha kupata mazoezi mazuri zaidi ya mwili kuliko kwenda katika chumba cha mazoezi. Jinsi gani? Kulingana na Search, “utendaji kama vile kulima na kukusanya majani ni mazoezi mazuri yanayotumia kalori nyingi zaidi kuliko kuendesha baiskeli.”

Kutunza bustani huwanufaisha hasa wazee. Kusubiri chipukizi au mche mpya uibuke huwasaidia kutazamia wakati ujao wakiwa na uhakika. Pia, “bustani hutuliza maumivu na mfadhaiko” unaosababishwa na uzee, asema Dakt. Brigid Boardman wa Royal Horticultural Society. Mara nyingi wazee huvunjika moyo kwa sababu ya kuwategemea sana wengine. Hata hivyo, kama Dakt. Boardman anavyosema, “ile hisia ya kutaka kujitegemea inatoshelezwa kwa kuamua kitakachopandwa, mahali kitakapopandwa, na jinsi ya kuitunza bustani. Na ule uhitaji wa kutunza unatoshelezwa pia.”

Wale walio na matatizo ya akili mara nyingi hutulia wanapofanya kazi katika mazingira mazuri, matulivu. Isitoshe, kupanda maua au chakula kwa ajili ya wengine kwaweza kuwasaidia watu hao wajiamini tena na kujiheshimu.

Hata hivyo, wanaofaidika na bustani hizo si wale wanaozitunza tu. Profesa Roger Ulrich wa Chuo Kikuu cha Texas alifanya majaribio kwa kutumia kikundi cha watu waliokuwa wametiwa chini ya mkazo. Aligundua kwamba wale waliopelekwa mahali penye miti na majani mengi walipata nafuu haraka—kulingana na mpigo wa moyo na shinikizo la damu—kuliko wale ambao hawakuwekwa katika mazingira hayo ya asili. Jaribio kama hilo lilionyesha kwamba wagonjwa wanaoendelea kupata nafuu katika hospitali baada ya kufanyiwa upasuaji walinufaika kwa kukaa katika vyumba ambamo wangeweza kuona miti. Tofauti na wagonjwa wengine, “walipata nafuu haraka, wakarudi nyumbani mapema, hawakuhitaji dawa nyingi za kutuliza maumivu, na walikuwa na malalamiko machache zaidi.”
UTUNZAJI SAHIHI WA BUSTANI UNA FAIDA ZIFUATAZO UTUNZAJI SAHIHI WA BUSTANI UNA FAIDA ZIFUATAZO Reviewed by BENSON on June 16, 2018 Rating: 5

No comments