JINSI YA KUFANYA KILIMO BORA CHA GILIGILANI


Kilimo cha giligilani (coriander) ni mradi mkubwa unaojitosheleza na zao hili huchukua muda mfupi toka kuotesha hadi kuvuna.
giligilani hutumika kama kiungo cha chakula katika mapishi mbalimbali kama nyama, supu au mchuzi. Giligilani hulimwa katika maeneo mengi ya Tanzania hususani mikoa ya Mbeya, Iringa na Arusha. 
Aina ya Giligiliani
Giligilani fupi: Aina hii ni nzuri kwa mkulima yeyote anayetaka kulima kwa lengo la kuvuna mbegu. Hii ni kwa sababu inatoa maua ikiwa fupi, inakomaa kwa haraka na mbegu zake huwa nyingi.
Giligilani ndefu: Hii ni aina ambayo ni bora kwa ajili ya kilimo cha kuvuna majani lakini pia mbegu zake hufaa kwa viungo. Aina hii hurefuka zaidi kabla ya kutoa maua na mbegu zake ni chache.
Hali ya hewa
Giligilani hustawi katika maeneo yenye joto lisilozidi nyuzi 20°C hadi 25°C, kiasi cha mita 1000 hadi 1800 kutoka usawa wa bahari. Pia hustawi katika maeneo yenye nyuzi joto zaidi ya 25°C . Mikoa ya Mbeya na Iringa ni maeneo mazuri kulima giligiliani kulingana na hali ya hewa ya ubaridi katika msimu wote wa mwaka.
Udongo
Kilimo cha Giligilani  kinastawi katika udongo wa aina yoyote lakini hustawi vizuri zaidi katika udongo tifutifu (Loam soil) na udongo wa kichanga (Sandy soil).
Mbolea
Weka mbolea ya mboji kwa ajili ya kurutubisha udongo na kuongeza mavuno. Mwagilia shamba lako kwa siku mbili na baada ya kufanya hivyo, tifua tena kwa kutumia rato, kisha sawazisha vizuri kuondoa mabonde na kisha sia mbegu za giligilani. 
Uoteshaji kwa ajili ya kiungo
Endapo unakusudia kuzalisha giligilani kwa ajili ya kuvuna majani ambayo hutumika kama kiungo kwenye chakula, ni lazima uoteshe giligilani ndefu na unatakiwa kusia kama unavyosia mbegu za mchicha ila hakikisha mbegu hizo hazitarundikana mahali pamoja.
Nafasi
Umbali wa shimo hadi shimo liwe sentimita 10-15 na umbali kati ya mstari na mstari iwe ni sentimita 20.
Kuota
Giligilani huanza kuchipua kuanzia siku ya 8 hadi 15 toka kuoteshwa. Hakikisha katika siku 12 za mwanzo unamwagilia kila baada ya siku mbili, na baada ya hapo kila wiki mara mbili au tatu. Ikiwa mvua zinanyesha, hakuna haja ya kumwagilia.
Kukomaa na Kuvuna
Giligilani hukomaa vizuri baada ya siku arobaini (mwezi na siku kumi) na hapo huwa tayari kwa kuvunwa. Kama unakusudia kuvuna majani, hakikisha unaanza kuvuna kabla ya kuanza kutoa maua au mara baada ya kufikia urefu wa sentimeta 20. Hakikisha unang’oa wakati wa asubuhi kwa kung’oa mche pamoja na mizizi yake kisha kuziosha ili kuondoa udongo wote. Baada ya hapo, funga kulingana na soko husika.
Ikiwa unakusudia kuvuna mbegu, hakikisha mbegu zimekomaa kwa kubadilika rangi na kuwa kahawia. Ng’oa miche na rundika mahali pasipokuwa na maji au unyevu kwa muda wa siku saba, kisha zipige polepole hadi mbegu zote zitoke katika majani. Pepeta na fungasha tayari kwa kuuza.
Magonjwa na Udhibiti
Giligilani ni zao hushambuliwa na ugonjwa ukungu ambao husababishwa na wingi wa maji shambani hasa linapooteshwa wakati wa mvua kubwa na wakati wa baridi kali. Hakikisha unamwagilia kwa kiwango cha wastani huku ukiepuka kuotesha wakati wa mvua nyingi na wakati wa baridi kali.
JINSI YA KUFANYA KILIMO BORA CHA GILIGILANI JINSI YA KUFANYA KILIMO BORA CHA GILIGILANI Reviewed by BENSON on April 06, 2018 Rating: 5

No comments