ELIMU JUU YA VIOTA BORA KWA AJILI YA KUKU.
Viota ni
mahali ambapo kuku hutaga mayai, kuhatamia na kuangua vifaranga. Hii
inamaanisha kuwa viota ni sehemu muhimu sana ya kuzingatia ili kuweza kupata
mayai mengi yaliyo salama pamoja na vifaranga.
Kuku
anapotagia porini, mayai huliwa na wanyama kama vile nyoka na wengineo. Kuku
pia anaweza kudhuriwa na wanyama hao na wakati mwingine kuibwa.
Aina za
viota
Kuna
makundi mawili ya viota vinavyotumiwa na kuku pamoja na ndege wengine
wafugwao.
• Kiota
kilicho tengenezwa na kuku mwenyewe
Hii ni
aina ya viota ambavyo kuku huchagua mahali pa kutaga na kuhifadhi mayai.
Inaweza kuwa mahali popote ambapo kuku ataona mayai hayataweza kudhurika au
kuonekana. Kwa mfano, vichakani, stoo au kona yenye giza. Njia hii si nzuri
kwani husababisha upotevu wa kuku na uharibifu wa mayai.
Kwa
kutagia stoo au sehemu iliyojificha ya ndani, japokua ni sehemu salama ambayo
haiwezi kufikiwa kirahisi na wezi au wanyama, mayai yanaweza kuharibika. Kuku
akitaga sakafuni, sehemu yenye nailoni au magunia mayai yanaweza kuharibiwa na
unyevu. Mayai hayo si mazuri kwa kutotoleshea. Itabidi mfugaji ayatumie au
ayauze kwa ajili ya chakula.
Katika
ufugaji wa ndani, kuku hutaga mayai sehemu yoyote hasa kipindi ambacho kuku
huanza kutaga. Hii husababisha mfugaji kuyakanyaga mayai kwa bahati mbaya au
kuku wenyewe kula mayai hayo na kupunguza uzalishaji wa mayai.
Kiota
kilicho andaliwa na mfugaji
Kuku
wanapotengenezewe viota vizuri huhatamia kwa utulivu kuongeza uzalishaji
Hii ni
aina ya viota vilivyo andaliwa kiustadi na kuwekwa mahali stahiki kwa
kumrahisishia kuku sehemu ya kutagia. Viota hivi huwekwa ndani ya banda au
sehemu nyingine iliyoandaliwa. Viota vya aina hii huandaliwa kwa kuzingatia
idadi ya kuku wanaotarajiwa kutaga, pamoja na upatikanaji wa vifaa vya
kutengeneza viota.
Mahitaji
Unaweza
kutumia vifaa kama vile boksi la karatasi, mbao, nyasi, nguo aina ya pamba
(isiwe ya tetroni), matofari na maranda. Boksi, tofali, na mbao husaidia
kutengeneza umbo na ukubwa wa kiota. Nyasi maranda na nguo (viwe vikavu)
husaidia katika uhifadhi wa mayai yasiharibiwe na unyevu, pia ni mazuri kipindi
cha kuhatamia kwani hutunza joto.
Ukubwa wa
kiota unatakiwa uwe ni wa kumwezesha kuku kuenea na kujigeuza. Hii ina maana
kuwa unatakiwa uwe wastani wa sentimita 35 upana sentimita 35 na urefu
sentimita 35.
Namna ya
kupanga viota kwenye banda
Ili kuwa
na ufanisi mzuri, inabidi idadi ya viota kwenye banda iwe robo tatu ya matetea
yaliyofikia umri wa kutaga. Hii huondoa msongamano wa kutaga katika kiota
kimoja. Kwa mfugaji mwenye kuku wengi inampasa kuchagua vifaa ambavyo atajengea
viota vinavyoweza kutumia eneo dogo na huku akipata viota vingi.
Kwa kuku
wanaohatamia, inabidi watengewe chumba chao ili kuzuia uchanganyaji wa mayai.
Kila sehemu katika banda si nzuri kuweka viota. Hivyo, katika uchaguzi inakupasa
uzingatie mambo yafuatayo:
• Viota
visiwe karibu au chini ya kichanja cha kupumzikia, vyombo vya chakula na maji.
• Kiota
kisiwe sehemu ambayo mfugaji atakua anapitapita. Mfano, karibu na mlango au
dirisha.
• Kiota
kisiwe mkabala na sehemu ambayo upepo mkali au mwanga utakua unaingia.
Wakati wa
ujenzi wa banda unaweza kujenga vyumba viwili ambavyo kimoja kikubwa utatenga
sehemu ya chakula, maji na sehemu ya kupumnzika.
Chumba
cha pili utatengeneza viota tu ili kuku anayetaka kutaga aende huko. Kwa
kufanya hivyo, kuku wachache watakua wakienda chumba hicho, na usumbufu kwa
kuku wanaotaga utakuwa mdogo.
Kulingana
na kiasi cha nafasi, unaweza kujenga viota mwisho wa banda na vyombo vya
chakula na maji upande wa mbele karibu na mlango. Hii itasaidia kuku kushinda
sehemu yenye chakula na maji hivyo kuepusha usumbufu kwenye viota.
Kuku
wanaohatamia
Viota vya
kuku wanaohatamia inabidi viwe sehemu tofauti na viota ambavyo kuku wanatagia
mayai kila siku. Hii itasaidia kuzuia uchanganyaji wa mayai yaliyoanza
kuhatamiwa na mapya. Viota hivyo viandaliwe vizuri kwani hukaa na mayai kwa
muda mrefu. Ni vema kuwatenga kuku katika chumba chao ambapo watapatiwa maji na
chakula.
Umuhimu
wa viota
• Kwa
kuwa na viota vya kutosha itapunguza usumbufu wa kuingia kukusanya mayai kwa
mfugaji.
• Njia
mojawapo ya kuzuia kuku kula mayai.
• Upotevu
wa kuku na mayai utapungua.
• Utapata
mayai bora kwa ajili ya kutotolesha.
•
Kupunguza mayai kupasuka, pia mayai kuwa safi.
• Kuku
kuwa huru wakati wa kutaga au kuhatamia.
ELIMU JUU YA VIOTA BORA KWA AJILI YA KUKU.
Reviewed by BENSON
on
October 14, 2017
Rating:
No comments