KANUNI ZA MSINGI KATIKA UFUGAJI WA BATA MZINGA
Kabla ya kuanza ufugaji wa bata mzinga ni lazima kuhakikisha una chakula cha kutosha kwa sababu ulishaji wa ndege hawa kadri wanavyokua huwa na gharama kubwa zaidi. Ni muhimu pia kujifunza kwa undani na kufahamu namna ya kutunza vifaranga wa bata mzinga kwa kuwa hufa kwa urahisi sana. Pia, unapaswa kujikita kutafuta soko kwa sababu wanapokuwa ni vigumu kuwatunza kwa muda mrefu kutokana na ukubwa wa gharama ya chakula.
Wafugaji wachache kati ya wengi waliojaribu kuwafuga ndege hawa na kufanikiwa hata kufikia malengo yao ni kutokana na kuzingatia lishe kamili. Pamoja na hayo, wapo wafugaji ambao walishindwa kutokana na magonjwa pamoja na gharama ya utunzaji.
Chakula
Chakula cha bata mzinga hakina tofauti na cha kuku. Vifaranga wanahitaji kupata lishe kamili yenye protini kwa wingi ili waweze kukua vizuri. Vifaranga kwa siku za awali wanahitaji kiasi cha asilimia 27 ya protini mpaka wanapofikia umri wa wiki sita. Baada ya hapo mfugaji anaweza kupunguza hadi kufikia asilimia 18, na kuendelea hivyo hadi wanapokomaa. Kutokana na gharama ya kununua chakula kuwa kubwa, unaweza kutumia reseheni ifuatayo kwa ajili ya kutengeneza chakula cha bata mzinga wewe mwenyewe.
Mahitaji
Mahindi 5kg (yasiyokuwa na dawa)
Karanga 5kg
Dagaa 5kg
Mashudu 10kg
Chokaa 5kg (chokaa inayotumika kwa lishe ya mifugo)
Namna ya kutengeneza chakula
Twanga au saga pamoja kiasi cha kulainika kisha walishe vifaranga. Mchanganyiko huu hutegemeana na wingi wa bata mzinga unaowafuga. Hakikisha kila bata anapata chakula cha kutosha na chenye uwiano ulioelekezwa. Pia waangalie mara kwa mara kuhakikisha wana chakula cha kutosha.
Uhifadhi
Hifadhi chakula cha ziada kwenye mifuko au debe kisha weka sehemu isiyo na unyevu.
Kutaga
Bata mzinga huanza kutaga anapofikisha umri wa mwaka mmoja. Ndege hawa wana uwezo wa kutaga kati ya mayai 15 hadi 20 kwa mara ya kwanza na kisha kuhatamia. Anapoendelea kukua huweza kutaga hadi mayai 30. Hii ni kulingana na lishe nzuri atakayopatiwa.
Kuhatamia
Bata mzinga anaweza kuhatamia mayai 17 hadi 20. Mayai hayo huhatamiwa kwa siku 28 na huanza kuanguliwa vifaranga kwa muda wa siku 3, kuanzia siku ya 28 hadi 31. Baada ya hapo mayai yaliyosalia bila kuanguliwa hutakiwa kutupwa kwa kuwa hayatoanguliwa tena na hayafai kwa matumizi mengine.
Utunzaji wa vifaranga
Baada ya vifaranga kuanguliwa, watenge na mama yao kwa kuwaweka kwenye banda safi lisilopitisha baridi. Unaweza kuwawekea taa ya kandili au ya umeme endapo upo kwenye sehemu unakopatikana.
Banda
Ni vyema banda liwe limesakafiwa au banda la asili la udongo usiotuhamisha maji. Pia, unaweza kutumia banda lenye mbao au mabanzi kwa chini. Unaweza pia kutandaza maranda kwenye mabanda. Hakikisha kuta za banda zimefunikwa vizuri ili kuwakinga dhidi ya baridi.
Maji
Kama ilivyo ndege wengine, bata mzinga pia wanahitaji kupatiwa maji masafi na ya kutosha wakati wote. Wawekee maji katika chombo ambacho hawatamwaga na wanakifikia vizuri. Hakikisha maji hayamwagiki bandani kwani kwa kufanya hivyo banda litachafuka na kukaribisha magonjwa kwa urahisi. Ni vizuri kuwalisha bata mzinga vyakula vingine kama majani. Majani husaidia kuwapatia protini: mfano; kunde, fiwi na aina nyingine za majani jamii ya mikunde huhitajika zaidi kwa kiasi cha 25% hadi 30%.
Magonjwa
Bata mzinga hushambuliwa na magonjwa kama taifodi, mafua na kuharisha damu. Wanapougua ni rahisi kuambukiza kuku, bata na ndege wengine wanaofugwa kwa haraka sana. Pia, ndege hawa husumbuliwa na viroboto wanaosababishwa na uchafu wa banda hasa linapokuwa na vumbi.
Chanjo
Bata mzinga wanatakiwa kupatiwa chanjo ya ndui (mara moja kila mwaka), kideri (kila baada ya miezi mitatu), gumboro (kwa muda wa wiki tano – ukiwapa jumatatu, basi unawapatia kila jumatatu ya wiki), na vitamini A mara baada ya kuanguliwa.
KANUNI ZA MSINGI KATIKA UFUGAJI WA BATA MZINGA
Reviewed by BENSON
on
April 10, 2018
Rating:
No comments