UFAHAMU UGONJWA WA MNAYAUKO WA MIGOMBA
UTANGULIZI
Ugonjwa wa
Unyanjano au Mnyauko bakteria wa migomba (Banana Xanthomonas Wilt)
umepewa jina lake kutoka kwa bakteria wanaoambukiza na hatimaye kuua
mgomba. Ugonjwa huo umeongezeka sana nchini Tanzania tangu
ulipogundulika kwa mara ya kwanza mwaka wa 2006 mkoani Kagera ukutokea
nchini Uganda.
Aina zote
za migomba hushambuliwa ingawa matokeo ya utafiti yameonyesha uwezekano
wa kupatikana kwa aina sugu siku zijazo. Aina kuu ya usimamiaji kwa sasa
ni kuzingatia usafi wa shamba: kupanda mazao ya afya, kutumia zana safi
za kukatia na kuondoa maua dume ili kupunguza kuathiriwa kupitia wadudu
wanaobeba bakteria wakati wanapofyonza utomvu.
VISABABISHI
Mnyauko
bacteria ni ugonjwa unaosababishwa na bacteria wanaofahamika kitaalamu
kama Xanthomonas campestris pv musaerum, ambao hushambulia aina zote za
migomba na jamii yake. Ugonjwa huu unaosababishwa na bacteria
husababisha majani ya migomba kuwa ya njano na kisha kunyauka na
kukauka. Pia ugonjwa huu huathiri matunda ya ndizi, shina la mgomba
kuoza na hatimaye kufa.
‘pv.’ husimamia kwa neno pathovar na inaonyesha aina fulani ya X.
campestris ambayo huambukiza tu migomba pekee na jamii yake ya karibu ya
ensete. Hapo awali ilikuwa inajulikana kama X. musacearum. Bakteria
wanaweza kuenea kwa njia ya wadudu wanaotembelea maua ya mimea
iliyoambukizwa na kisha kulisha juu ya mimea safi na pia kupitia njia ya
zana zakukata zilizo na bakteria.
Kimataifa, kuna aina kadhaa za mnyauko bakteria ambazo husababisha
dalili sawa na pia kuishi katika njia sawa kama Banana Xanthomonas Wilt.
Nyauko hizi zinahusishwa na aina tofauti ya bakteria Ralstonia
solanacearum, ambayo haishambulii migomba katika Afrika.
Migomba iliyoathrika na BXW |
UENEAJI
HISTORIA
Ugonjwa wa
unyanjano umekuepo tangu miaka ya 1930, ambapo kwa mara ya kwanza
ulijitokeza nchini Ethiopia, na kasha kujitokeza katika nchi za Afrika
ya Mashariki mwaka 2001. Ugonjwa huu ulianzia Uganda na kusambaa katika
nchi nyingine kama Tanzania, Kenya, Rwanda, Burundi, na Jamhuri ya
Congo. Katika nchi hizo uligundulika kwa vipindi tofauti, na hivi sasa
upo katika nchi zote za Afrika Mashariki na Kati.
Mwaka 2003 utafiti ulianza kufanyika nchini Tanzania Mkoani Kagera ili
kubaini kama ugonjwa huo umeshaenea, ambapo haukugundulika mpaka kufikia
mwaka 2006 Januari uligundulika katika kijiji cha Kabale kilichopo
tarafa ya Izigo wilaya ya Muleba.
Mnamo
Januari mwaka 2006 hadi juni 2012 ugojwa wa unyanjano ulikuwa umeenea
wilaya mbalimbali za mkoa huo, isipokuwa wilaya ya Biharamulo huku jumla
ya kata 110, vijiji 389 na kaya 56,520 zikiripotiwa kuathirika na
ugonjwa huo. Maeneo mengingine ya Tanzania Ugojwa ulithibitishwa ni
pamoja na wilaya ya Tarime Mkoani Mara, Chato na Geita katika Mkoa wa
Geita, kasulu, Kibondo, na Kakonko Mkoa wa Kigoma pamoja na wilaya ya
Ukelewe Mwanza.
UNAVYO SAMBAA
Ugonjwa wa
unyanjano huenea kutoka mmea hadi mmea au shamba hadi shamba kwa njia ya
viumbe kama vile ndege, nyuki, binadamu, ngedere na tumbili.
Zana
Zana za
kufanyia kazi shambani ni moja ya njia zinazotajwa kuchangia kuenea kwa
ugonjwa wa unyanjano. Zana kama vile panga, chezo, chimbuo, visu na
nyengo (mundu), husambaza ugonjwa huu vinapotumika kuondoka makuti,
majani, kuvuna ndizi na kukatakata mashina na migomba ambayo imeathiriwa
na ugonjwa huu na kasha kutumika kwenye mimea ambayo haijaathirika bila
kuvisafisha. Chimbuo hueneza ugonjwa wakati wa kung’oa vikonyo na
kupunguza machipukizi. Nyengo nayo wakati wa kuondoa majani inaweza
kueneza ugonjwa kutoka shina hadi shina, au shamba hadi shamba.
Binadamu
Binadamu anachangia kuenea kwa ugonjwa huu anaposafirisha miche ya
migomba, ndizi na majani kutoka shamba lililoathirika kwenda sehemu
nyengine pamoja na kutumia ua-dume kama kizibo kwenye madumu ya maji au
pombe.
Nyuki na Ngedere
Viumbe hawa huweza kueneza ugonjwa wakati wanapofyonza utomvu mtamu
kutoka kwenye ua dume la ndizi iliyoathirika, kasha kupeleka kwenye mmea
mwengine. Viumbe hawa hubeba bacteria katika miguu yao.
Zingatia:
Bakteria wanaosababisha ugonjwa huu huwasafirshwi kwa njia ya upepo
wala hewa, na inachukua kupindi cha miezi miwili bila kuona dalili za
ugonjwa huu (incubation period)
DALILI MUHIMU
Ugonjwa huu huweza kutambulika kwa hatua au muonekano tofauti kwenye migomba na mimea mingine ya jamii yake.
- Majani machanga, sehemu ya juu hubanduka na kuonekana kama yamepitishwa kwenye moto, kisha kukauka kwenye ncha na kujikunja.
- Ndizi huiva kabla ya kukomaa
- Sehemu ya ndani ya ndizi huwa na rangi ya ugoro na kutoa harufu ya uozo, hivyo binadamu au wanyama hawawezi kula
Ndizi iliyoharibiwa na unyanjano |
- Ndizi huwa ngumu na haiwezi kuiva ikipikwa.
- Ukikata shina, utomvu huwa wa njano (kata shina kisha subiri kwa dakika 5-15 utaona utomvu mzito wenye rangi ya njano).
Utomvu mzito uliosababishwa na unyanjano |
- Ua dume hunyauka isivyo kawaida, huoza, hukauka na kisha hudondoka
Ugonjwa wa kuvu wa migomba, unaojulikana kama Fusarium wilt au ugonjwa
wa Panama, pia husababisha rangi ya manjano lakini kwenye majani
yaliyozeeka. Jani halijikunji na manjano yake ni kali zaidi
ikilinganishwa na ya unyanjano. Matunda huendelea kawaida. Dalili ya
kutofautisha Fusarium wilt ni rangi nyeusi ndani ya shina ambayo haiko
kwenye migomba iliyoambukizwa na mnyauko bakteria/unyanjano.
ATHARI
Unyanjano ni ugonjwa mharibifu sana unaoathiri kila aina ya migomba.
Mimea na matunda huharibiwa. Ugonjwa unaweza kuenezwa mbali kwa njia ya
vipandikizi na mabaki ya mimea. Haja kubwa ya ndizi katika Kampala
huvutia kuletwa kwa bidhaa kutoka mbali. Habari nyingi kuhusu madhara
hutoka Kagera, ambapo ugonjwa huo umesababisha hasara kubwa na ukawa na
msisimko wa juu wa katika kuchochea juhudi za utafiti na ushauri wa
ugani ili kuudhibiti na kusimamia kuzuka.
USIMAMIZI (MANAGEMENT)
Ifahamike kwamba ugonjwa huu hauna dawa. Hivyo ni lazima kuchukua hatua
madhubuti na kuokoa migomba yetu. Ni muhimu kwa wakulima kuwa na uelewa
na ufahamu juu ya ugonjwa huu, madhara yake na kudhibitiwa ipasavyo.
Vifaaa vinavyotumika shambani, visafishwe kabla ya kutumika shambani na
baada ya kutumika. Fyeka migomba yote iliyoathiriwa na ondoa ua dume
kuzuia kuenea kwa ugonjwa.
KINGA – mambo ya kufanya kabla dalili kuonekana
- Mbinu za kitamaduni: (Cultural practices)
Ugonjwa wa unyanjano huenea kwa njia ya machipukizi ya kupanda, na
wadudu ambao huingiza bakteria kupitia maua ya mgomba. Bakteria pia
wanaweza kusafirishwa kwenye zana za kukatia. Aina zote za migomba
hushambuliwa ingawa ni vigumu kwa bakteria kuambukiza baadhi ya aina
mashambani kwa sababu ya hali zao za maua. Aina hizi pia zinaweza
kuambukizwa kwa kupitia zana za kukatia ambazo zimebeba bakteria.
Njia muhimu kwa mafanikio ya usimamizi ni uteuzi makini wa machipukizi
yasiyokuwa na ugonjwa na kuweka zana za kutumika kwa ajili ya kukata
mikungu ya ndizi na majani kuwa safi na zisizo na bakteria.
Chagua kwa makini machipukizi ya kupanda kutoka maeneo ambapo ugonjwa
huo hauko. Pata machipukizi kutoka kwa vyanzo vya kuaminika. Usitumie
machipukizi kutoka kwa mimea iliyoathiriwa na BXW, hata kama machipukizi
yataonekana kuwa yenye afya.
Kuondolewa
kwa ua dume kwa kutumia mkono au mti panda (ili kupunguza hatari ya
kuhamisha bakteria kupitia zana za kukata) kutapunguza athari ya
kuambukizwa kupitia wadudu wanaobeba mbelewele na utomvu ambao awali
wamezichukua kutoka kwa mimea iliyoambukizwa. Majira ya kuyaondoa ni
muhimu; maua dume yanastahili kukatwa haraka baada ya chana ya mwisho.
Shida ya njia hii ni kwamba huchukua muda mwingi na baadhi ya wakulima
wanaamini kuwa ua dume ni muhimu kwa ajili ya uzalishaji wa juisi nzuri
katika aina ya ndizi za kutengeza bia.
- Mbinu za kikemikali:
Vifaa vya kukata vinaweza kusafishwa kwa kutumia dawa ya jik (sehemu
moja ya dawa na sehemu nne za maji), dawa za mimea ya kienyeji zenye
uwezo wa kuua bacteria, kama vile tumbaku au pilipili, au kwa kupitisha
kwenye moto. Jik ni njia ya ufanisi zaidi kwa kuua bakteria ingawa
wakulima wachache huonekana kutumia njia hii.
UDHIBITI – mambo ya kufanya baada ya dalili kuonekana
- Mbinu za kitamaduni (cultural practices)
Ushauri wa awali wakati BXW ilipogunduliwa kwa mara ya kwanza nchini
Uganda ulikuwa ni kuchimba na kuchoma koo zima la mgomba. Sasa tunajua
kwamba bakteria hawavamii kabisa mmea wote.Ushauri sasa hivi kwa hivyo,
ni kung’oa mashina yanayoonyesha dalili ya BXW na kuyatupa kwa makini.
Kutoa shina moja kutapunguza kiasi cha bakteria wanaoweza kuambukiza
mimea mipya, lakini hii haitaondoa kabisa ugonjwa. Kuchagua vipandikizi
vyenye afya na kusafisha vifaa vya kufanyia kazi ndio ushauri mhimu wa
kufuata uliobaki.
- Mbinu za kikemikali: Mmea unapoambukizwa, hakuna tiba ya kudhibiti ugonjwa huo.
Ushauri: Baada ya wakulima kung’oa migomba yote iliyoathirika na
kuiteketeza, inashauriwa kununua mbegu bora kutoka katika vituo vya
utafiti ili kuhakikisha wanakuwa na uzalishaji mzuri. Mbegu ya FHIA ni
bora zaidi na huzalisha kwa kiwango kizuri.
UFAHAMU UGONJWA WA MNAYAUKO WA MIGOMBA
Reviewed by BENSON
on
February 20, 2018
Rating: 5
No comments