TAJIRIKA KWA KILIMO BORA CHA VITUNGUU SWAUMU.

Vitunguu swaumu ni miongoni mwa mazao ambayo yana faida lukuki kwa mkulima hasa pale anapoamua kujiwekeza katika kilimo hiki. Hivyo ili uweze kulima kilimo hicho chenye tija unatakiwa kuzingatia yafuatayo;

Udongo Ufaao kwa kilimo hiki. 
Vitunguu swaumu vina uwezo mkubwa wa kuhimili aina nyingi za udongo, ila vinastawi zaidi katika udongo usiotuamisha maji kabisa na wenye mbolea asili, kama mbolea si ya kutosha kwenye udongo, tumia samadi iliyokwisha oza vizuri usitoe samadi bandani na kuipeleka shambani moja kwa moja kwenye shamba la vitunguu swaumu, labda kama utaliacha shamba bila kulimwa kwa zaidi ya miezi 6 ndipo upande vitunguu hivyo, pia unaweza kutumia mbolea za viwandani kama ammonium nitrate, ammonium sulphate, urea n.k wakati wa kupanda na kila baada ya wiki 4 – 6 mara mbili zaidi 

Upandaji
Kipindi kizuri kwa upandaji ni kipindi ambacho hakuna joto hasa miezi ya mwezi wa tano mpaka mwezi wa nane, nama bora ya upandaji unashauriwa kunachukua kitunguu swaumu na kutenganisha vitunguu kimoja kimoja (bulbs) na kuchagua vile vikubwa maana hivi ndivyo vitakavyo kupa mazao mengi na bora, nafasi kati ya kitunguu na kitunguu ni sentimeta 10 na kati ya mistari ni sentimeta 30.


Baada ya kupanda pandishia udongo na uukandamize kuhakikisha kwamba kimekaa vizuri na hakiwezi kuathiriwa na mvua au maji wakati wa kumwagilia, pia ili kisikae upande au kungolewa kabisa. Uotaji mzuri hutegemea pia namna vitunguu swaumu vilivyo hifadhiwa kabla ya kupandwa, kama vilihifadhiwa sehemu zenye joto na hewa finyu uotaji wake utakuwa duni na dhaifu. 


Umwagiliaji. 
Kama kuna upungufu wa mvua au ni kipindi cha kiangazi basi ni vizuri ukamwagilia shamba lako, wakati mzuri wa kumwagilia vitunguu swaumu ni wakati wa asubuhi na sio jioni au mchana, hii inasaidia vitunguu swaumu kujijengea uwezo wa kupambana na magonjwa. Lakini  baada ya miezi miwili unaweza kupunguza umwagiliajai huku ukiangalia kwa kuchimba kidogo kama vitunguu swaumu vimezaliana vya kutosha na kuanza kukomaa, ukiona vimekomaa acha kabisa kumwagilia ili visioze 

Uangalizi.
Aina nyingi za vitunguu swaumu vitakuwa kama vinatoa mbegu kwenye mmea, ingawa kuna nadharia nyingi lakini inashauriwa kukata hizi mbegu chini kabisa kwa kisu kikali na kisafi, usikate mapema mara baada ya kutokeza bali subiri mpaka mmea unapoanza kama kujikunja ndipo ukate, kwa wale wanaoacha mbegu hizi ukiamua kuzipanda kwa msimu wa kwanza zitazaa kitunguu kimoja tu cha duara lakini chenyewe ukikipanda tena kwenye mzunguko wa pili kitazaa vitunguu vingi kama kawaida 

Ungoleaji wa magugu na majani ni muhimu muda wote ili kuondoa kugombea rutuba, hewa na maji shambani, kwa wenye mashamba makubwa wanaweza kutumia dawa za kemikali kama ROUNDUP na nyinginezo ili kudhibiti magugu, ingawa mimi sishauri hivyo

Magonjwa 
Magonjwa kama botrytis (kuoza shingo) blue mould na fusarium (kuoza kwa vitunguu) husababisha hasara kubwa kama hayatadhibitiwa kwa kutumia viuatilifu mara unapoona dalili, pia magonjwa kama white rot huchukua zaidi ya miaka 20 kuondoka kama yatavamia shamba lako, inashauriwa kufanya mabadiliko ya zao kila baada ya miaka mitano kwa kupanda mazao mengine yasiyo jamii moja kama vitunguu maji, unaweza kupanda maharage, mahindi, karoti na kabichi katika mzunguko huo.


Pia magonjwa kama kutu ya majani husababisha na unyevu mwingi hasa kama mimea itakuwa kwenye udongo unaotuamisha maji au mimea kumwagiliwa jioni au usiku, kumbuka kumwagilia asubuhi tu Ili kudhibiti ugonjwa huu wa kutu mimea ingolewe na ichomwe au utumie viuatilifu vya kuulia fangasi wa mimea


TAJIRIKA KWA KILIMO BORA CHA VITUNGUU SWAUMU. TAJIRIKA KWA KILIMO BORA CHA VITUNGUU SWAUMU. Reviewed by BENSON on July 21, 2017 Rating: 5

3 comments

  1. Asante kwa somo zuri but naomba kuuliza hivi karoti huwa zinalimwa wapi wa Tanzania?

    ReplyDelete
  2. Naomba kujua mbolea ya samadi unaiandaaje mpaka ioze ndo uipeleke shambani?

    ReplyDelete
  3. Ningependa kuuliza zinachukua mda gan kukomaa??.

    ReplyDelete