KILIMO BORA CHA TANGAWIZI.
Tangawizi ni aina ya zao la kiungo
ambalo huonekana kama mizizi ya mmea. Asili ya zao hili ni maeneo ya kitropiki
ya bara la Asia na hasa katika nchi za India na China. Zao hili linazalishwa
kwa wingi kutoka katika nchi ya Jamaica. Hapa nchini zao hili hulimwa katika
mikoa ya Kigoma, Tanga, Morogoro, Pwani, Mbeya na Kilimanjaro.
Tangawizi hutumika kama kiungo katika
kuongeza ladha, harufu na kuchangamsha katika vinywaji (kama chai, soda, juisi,
vilevi n.k) na vyakula mbalimbali kama mikate, biskuti, keki, nyama za kusaga,
achari n.k. Hutumika pia katika viwanda vinavyotengeneza madawa ya tiba
mbalimbali kama dawa za meno, kikohozi, tumbo na muwasho wa ngozi n.k. pia
hutumika katika vipodozi kama poda n.k).
Tabia za mmea wa tangawizi
Tangawizi ni mmea unaotambaa chini ya ardhi, wakati wa masika hutoa majani juu
ya ardhi. Mmea una urefu wa futi mbili na majani yake ni membamba marefu ambayo
hufa kila mwaka yakiacha tunguu ardhini likiwa hai. Maua ya mmea huu yana rangi
nyeupe au manjano.
Hali ya hewa na udongo ufaao kwa
kilimo hiki.
Zao hili hustawi katika maeneo yenye hali ya kitropiki, kutoka usawa wa bahari
hadi mwinuko wa mita 1,500 au zaidi. Huhitaji mvua kiasi cha mm.1,200-1,800 na
joto la wastani wa nyuzi za sentigredi 20-25. Hustawi vema katika udongo
tifutifu wenye rutuba na usiotuamisha maji.
upandaji
Zao la tangawizi hupandwa kwa kutumia vipande vya tunguu vyenye kichipukizi
kizuri angalau kimoja na huweza kukatwa katika urefu wa sm.2.5-5. Wakati
mwingine, vichipukizi vinavyopatikana katika kumenya tangawizi huweza
kuhifadhiwa na kutumika kwa kupanda. Kiasi cha kilo 840-1700 cha vipande vya
tunguu huweza kutumika kwa kupanda katika hekta moja. Nafasi inayotumika
kupanda ni kati ya sentimita.23-30 kwa 15-23 na kina cha sentimita.5-10 na mara
nyingi hupandwa katika matuta. Baadhi ya mazao huweza kupandwa katika shamba la
tangawizi ili kuweka kivuli chepesi ingawa si lazima kivuli kiwepo. Inashauriwa
kumwagilia maji endapo mvua inakosekana.
Wiki 1-2 kabla ya kupanda weka mbolea ya samadi au mboji kiasi cha tani 25-30
kwa hekta na kwa kukuzia weka kiasi cha NPK kwa uwiano wa kilo 36:36:80.
Tandaza nyasi shambani kuhifadhi unyevunyevu hasa pale kivuli kinapokosekana.
Palizi hufanywa mara magugu yanapoota, dawa ya kuua magugu, kama simazine au
round up hutumika.
magonjwa na wadudu yanayoathiri mmea huuu.
1. Madoa ya majani yanayosababishwa na viini vya magonjwa viitwavyo
Colletotrichum zingiberis na Phyllosticta zingiberi.
2. Kuoza kwa tunguu;
kunasababishwa na viini viitwavyo Pithium spp
3. Mizizi fundo;
inasababishwa na Meloidegyne spp.
Uvunaji.
Tangawizi huweza kuwa tayari kwa kuvuna kati ya miezi 9-10 baada ya
kupanda, wakati majani yake yanapogeuka rangi kuwa njano na mashina kusinyaa.
Tangawizi inayohitajika kwa kuhifadhi kwenye kemikali (preserved ginger in
brine) huvunwa kabla haijakomaa kabisa, wakati ile iliyokomaa kabisa huwa kali
zaidi na huwa na nyuzi hivyo hufaa kwa kukausha na kusaga. Mavuno hutofautiana
kulinganana na huduma ya zao, mavuno yanaweza kuwa kiasi cha tani 20-30 cha
tangawizi mbichi huweza kupatikana.
Usindikaji.
Tangawizi ikisindikwa utapata unga, mafuta maalum (essential oils) n.k.
Tangawizi iliyovunwa huweza kumenywa, kukatwa na kukaushwa juani au mara
nyingine huchovywa katika maji yaliyochemka kwanza na ndipo kukaushwa au
hukamuliwa mafuta. Pia tangawizi husindikwa na kuhifadhiwa kwenye chupa zikiwa
zimechanganywa na sukari na/au chumvi au bila kuweka kitu chochote. Hata hivyo
tangawizi ina Kiasi cha mafuta cha 16.0-18.0%.
Soko la tangawizi.
Soko laz tangawizi lipo ndani na nje ya nchi, kiasi
kikubwa kinauzwa nchini. Bei yake ni kati sh. 300-1,500/- kutegemeana na msimu.
GHARAMA ZA UZALISHAJI NA MAPATO
GHARAMA YA HEKTA MOJA:
Mbegu Tshs. 240,000/-
Vibarua 250,000/-
Mbolea(mboji/samadi) 150,000/-
Jumla 640,000/-
MAPATO:
Kilo 20,000 X300 =6,000,000/-
KILIMO BORA CHA TANGAWIZI.
Reviewed by BENSON
on
July 15, 2017
Rating:
No comments