KILIMO BORA CHA MATIKITI MAJI


UTANGULIZI
Tikiti maji ni zao linalolimwa kibiashara.hufahamika kama Watermelon, na kwa jina la kibotania (Botanical name) hujulikana kama Citrullus lanatus. Ni moja ya mazao yanayotoka kwenye familia ya mimea ya Cucurbitaceae, mazao mengine ynayotoka family hiyo mojana tikiti maji, ni matango (Cucumber), maboga (pumpkin), musk melon, squash n.k. Inaaminika kwamba asili ya tikiti maji ni huko jangwa la Kalari ambako lilikua linapendwa sana kwa sababu lilitumika kupooza koo au kukata kiu kwa watu wanaoishi karibu na Jangwa la Kalahari hii ni kwasababu tikiti maji ni tunda lenye maji mengi. Inakadiriwa zaidi ya asilimia 90 ya runda la tikiti ni maji, ndio maana huitwa tikiti maji. Hata hapa Tanzania Tikiti maji soko lake zuri ni kipindi cha joto ambako walaji wengi hutumia kwa ajili ya kukata kiu kutokana na joto. Wauzaji wa matikiti katika masoko mabalimbali wanasema biashara ya tikiti ni nzuri sana wakati wa kiangazi/joto na wakati wa baridi biashara hiyo inadorora.  Taarifa kama hizo ni nzuri sana kwa mkulima mjasiriamali anayelenga uhitaji wa soko.


MAANDALIZI YA SHAMBA:
Shamba la kupanda matikiti maji linapaswa liandaliwe vizuri, udongo ulainike vizuri usiwe na mabonge ya udongo kwa maana mbegu za tikiti zinapdwa moja kwa moja shambani  (direct seeding) na mbegu hizo zina umbo dogo, hivyo zinahitaji udongo uliolainika vizuri ili kuweza kuota. Shamba linapaswa kua sehemu ambayo hakuna miti, maana kivuli cha miti kinaweza kusababisha matikiti yasitoe matunda.

Vifuatavyo ni Vigezo vya kuzingatia wakati wa kutafuta shamba/eneo la kupanda matikiti maji.


1. Aina ya Udongo
Tikiti maji linaweza kulimwa katika aina nyingi za Udongo, lakini yanafanya vizuri zaidi kwenye udongo kichanga (fine sand), tifutifu na tifutifu kichanga. Aina ya udongo itaadhiri uzalishaji wa tikiti kutegemeana na hali ya hewa. Kwa mfano unapolima tikiti kwenye udongo wa mfinyazi wakati kuna  mvua nyingi, mimea ya matikiti haitaweza kustawi, kwa sababu udongo wa mfinyazi utatuamisha maji kwasababu ya mvua na hivyo mimea itakufa. Vilevile unapootesha matikiti kwenye udongo wa kichanga, halafu pawe hakuna maji ya kutosha mimea itakufa kwa kukosa maji. Pia kumbuka udongo wa kichanga unapoteza maji kwa haraka, hivyo unapolima kwenye udongo wa aina hiyo hakikisha una maji ya kutosha na umwagiliaji uwe wa mara kwa mara.

2. Utoaji wa maji shambani (Drainage).
Kigezo kingine ambacho mkulima anapaswa kuzingatia wakati wa kutafuta eneo la kupanda matikiti ni Udongo wenye uwezo wa kutoa maji, yaani udongo usiotuamisha maji. Unaweza kutengeneza mifereji itakayoasaidia kuondoa maji yanayozidi shambani.
3. Mteremko wa Ardhi (Topography)
Ni ile hali shamba linapokua limeinuka upande mmoja na upande mwingine kuna mteremko au unaweza kuiita slope. Shamba lenye mteremko au slope ni rahisi sana kukumbwa na mmomonyoko wa udongo ambao utaharibu mimea yako. Hakikisha unapoachagua shamba, basi unaepuka maeneo ya mtindo huo.

4. Mwanga wa jua (Sunshine).
 Katika upandaji wa zao lolote mwanga wa jua ni muhimu sana kwasababu husaidia kwenye utengenezaji wa chakula cha mmea (Photosynthesis). Kwa upande wa matikiti, mwanga wa jua una athari kubwa sana kwenye mazao, aidha kupungua au kuongezeka. Mmea wa Tikiti  unahitaji angalau masaa 6 ya mwanga wa jua. Hii inasaidia sana katika utengenezaji wa sukari kwenye tikiti. Pia mwanga wa jua husaidia ukuaji wenye afya wa mmea wa tikiti. Hivyo kwa ukuaji mzuri, unapochagua eneo la kulima tikiti chagua eneo ambalo Mimea itapata mwanga wa jua wa moja kwa moja (direct sunlight) kwa angalau masaa 6 hadi 8 kwa siku. Hii ikimaanisha kwamba eneo liwe mbali na majenngo au miti mikubwa inayoweza kuleta kivuli kwenye shamba.

Madhara ya Kukosa Mwanga wa Kutosha
  • Matikiti yaliyopo eneo lenye mawingu ya mara kwa mara au eneo mbalo halipati mwanga wa jua wa kutosha, huzaa matunda yenye ladha mbaya.
  • Mimea ikikosa mwanga, hunyauka na kufa.
  • Uchavushaji (pollination) kwenye Mimea ya Matikiti hufanywa na wadudu kama nyuki, Shughuli za nyuki zinapungua wakati wa baridi au wakati wa mvua kwa sababu vipindi hivyo hakuna mwanga wa jua wakutosha. Hii ina maana kwamba hata eneo lenye kivuli sio rafiki kwa shughuli za uchavushaji
  • Matikiti yanahitaji joto ili kuzalisha matunda matamu. Hii ikimaanisha kama eneo litakua lina kivuli halitakua na joto hivyo matunda yatakosa sukari

5. Maji
Upatikanaji wa maji katika eneo la kuzalishia matikiti ni kigezo kingine muhimu cha kuzingatia wakati wa kuchagua eneo. Ili kufanya kilimo chenye uhakika, jitahidi eneo lako liwe karibu na chanzo cha maji cha uhakika, kwa ajili yakufanya umwagiliaji.

6. Kufikika.
Eneo liwe sehemu kunakofikika hususani  kwa miundombinu ya barabara. Eneo liwe mahali ambapo gari kubwa inaweza kufika, ili kusaidia usafirishaji wakati wa kuvuna.

AINA ZA MBEGU NA UCHAGUZI WA MBEGU NZURI
Uchaguzi wa aina ya mbegu (variety) ni kitu cha msingi sana katika kilimo cha tikiti ambapo shughuli zote zinajengwa kwenye msingi huo. Hii kimaanisha kama ukikosea kuchagua aina ya mbegu nzuri hata ukijitahidi mbinu nyingine, hazitakua na tija.  Kuchagua mbegu nzuri na zenye ubora sio kazi nyepesi, ni ngumu kweli kweli, kwa bahati mbaya wakulima wengi hukimbilia zile mbegu maarufu ambazo zinatangazwa zaidi, ambapo mara nyingi wanapokwenda kwenye uhalisia kwa kulima mbegu hizo hukumbana na hali tofauti na waliyoisikia kwenye matangazo.

Vigezo vya muhumu kuzingatia wakati wa Kuchagua Aina ya Mbegu:
Kabala mkulima hajafanya maamuzi ya mbegu ipi alime,

ni vyema akazingatia vigezo vifuatavyo:

Ni aina ipi ambayo ina soko? Kama unalima kibiashara, hichi ni kigezo cha kwanza kuzingatia, tambua kwanza soko unalolenga linapendelea aina ipi ya matikiti. Kwa mfano kwa kanda ya ziwa, matikiti yenye mistari ya Zebra, hayana mpenyo kwenye soko la kanda ya ziwa, walaji wengi bado wanapendelea yale matikiti ya kijani au wengine wanayaita meusi, yasiyokua na mistari au mabakamabaka. Sasa kwa kusikia maeneo mengine kama Arusha na kwingine  kwamba watu wanalima matikiti ya mistari ya zebra na Wewe uko kanda ya ziwa , halafu  ukaingia kulima hayo ya Zebra wakati soko lako unalolenga ni Mwanza, lazima wakati wa kuuza utalalamika hakuna soko. Hivyo ni muhimu  kufahamu  soko lako kwanza, jua linahitaji aina ipi kisha ndio ufanye uamuzi wa kulima aina ipi.

Uwezo wa kumudu au kukubali mazingira utakayolimia (adaptability). Sio aina zote za matikiti zinakubali kila aina ya mazingira, kuna maeneo  ambayo aina fulani inakubali, na ila aina nyingine ikagoma. Hivyo fahamu uwezo wa aina hiyo ya tikiti kuota kwenye mazingira yako. Kama kuna majirani  wanaolima matikiti au watu wa maeneo ya karibu na mazingira yako wanalima tikiti, unaweza kufanya utafiti wako kwa kujua ni aina ipi inafanya vizuri kwa hao majirani zako.

Angalia gharama za kuhudumia/matunzo.Kuna aina za tikiti zinahitaji matunzo ya gharama kubwa kama vile mbolea za kutosha, madawa n.k. Hivyo ni muhimu kujua gharama zake kabla hujanunua, ili kama uwezo wako hautamudu, uchague aina nyingine, ili usije pata hasara kwa kuchukua aina yenye kuhitaji matunzo makubwa ukashindwa kuyahudumia.

UPANDAJI
Katika upandaji wa tikikiti zipo aina nyingi za upandaji, ila kwa hapa tutagusia aina mbili ambazo zina matokeo mazuri.

Upandaji wa Mstari mmoja (Single row system). Hapa tuta linakua na mstari mmoja tu wa tikiti. Nafasi ya mstari hadi mstari ni mita 2 au mita mbili na nusu (2 – 2.5m). Nafasi ya mche hadi mche ni sentimita 60.

Upandaji wa Mistari miwili (double row system).Hapa tuta linakua na mistari miwili ya tikiti. Nafasi ya mstari hadi mstari ni mita tatu na nusu hadi mita nne (3.5 – 4.0m). Nafasi ya mche hadi mche ni sentimita sitini (60cm).

Kwenye shimo moja zinapandwa mbegu mbili, kama zikiota zote mbili, basi moja unaing’oa na kuhamishia kwingine ambako kunaweza kua ni sehemu mpya kabisa au ni hapohapo shambani, kwenye shimo ambalo hazijatoata au ziliota zikafa.

UWEKAJI WA MBOLEA
Mbolea ya Samadi: Weka shamba lako mbolea ya samadi iliyokauka vizuri. Kiasi kinachotosha ni tani 5 had 8 kwa ekari moja.

Mbolea za kupandia: Mbolea ya kupandia unaweza kutumia DAP, Minjingu au mbolea yeyote yenye kirutubisho kikubwa cha Phosphorous. Mbolea ya Kupandia inawekwa wakati wa kupanda, kwenye shimo la kupandia, unatanguliza mbolea ya kupandia wastani wa gramu 5, kisha unafunika na udongo kidogo kisha ndio mbegu ya tikiti inafuata. Lengo hapa ni mbegu isigusane na mbolea ya kupandia.

Mbolea za Kukuzia: Mbolea za kukuzia ni zinazotumika sana kwenye kilimo cha tikiti ni kama NPK, na CAN.

Mbolea za Majani (foliar fertilizers). Hizi ni mbolea zinazowekwa  kwenye majani kama unavyopulizia dawa (spraying). Mbolea hizi hua ni zile zenye vile virutubisho vinavyohitajika kwa kiwango kidogo (micronutrients). Unapiga mara matikti yanapoota, kisha unapiga tena wakati wa utoaji wa maua, halafu unamalizia na wakati wa utengenezji wa matunda.

MAGUGU NA PALIZI
Magugu yana madhara kwa zao lolote, ila yana madhara makubwa zaidi kwa zao la tikiti maji. Lakini ni muhimu kufahamu kwamba Udhibiti wa magugu au palizi kwenye matikiti kunahitaji umakini sana kwa maana tikiti hazihitaji kubugudhiwa au kuguswaguswa/kutingishwatingishwa maana husababisha mmea mzima kupata stress kitu ambacho kitaathiri mpangilio wa uzalishaji. Palizi pia inaweza kuharibu maua au matunda yale madogo yaliyoanza kutengenezwa.

ATHARI ZA MAGUGU KWENYE UZALISHAJI WA MATIKITI MAJI
Magugu yanashindania virutubisho na mazao (compete with plant for nutrients). Na magugu yana uwezo mkubwa wa kutumia virutubisho kuliko mazao, ndio maana magugu yanakua kwa haraka kuliko mazao yaliyopo shambani. Hii hupelekea uzalishaji wa tikiti kupungua.

Magugu yanashindania maji na mazao ya tikiti, na kupelekea tikiti kukauka. Kama ilivyo kwa virutubisho hivyohivyo magugu yana uwezo wa kutumia maji haraka kuliko mazao.
Magugu yanapunguza utoaji wa maua kwenye tikiti kutokana na kupungua kwa mwanga wa jua. Magugu husababisha kivuli kwa matikiti hivyo kukosa mwanga wa kutosha ambao husaidia mimea kutoa maua.

Magugu pia yanapunguza utoaji wa matunda kwenye mmea. Maua yakiwa machache hasa maua ya kike ina maana matunda yatakayotengnezwa yatakua machache zaidi.

Magugu yanazuia shughuli ya uchavushaji (pollination) shaghuli ambayo ni muhimu sana kwenye kilimo cha matikiti. Hii ina maana wadudu wanaofanya ushavushaji kama Nyuki, watakimbilia kwenye maua ya magugu na kuacha kushughulika na maua yamatikiti.
Magugu pia yanavutia wadudu na magonjwa kwenye mazao

UTHIBITI WA MAGUGU
Mpaka wa sasa hakuna madawa chaguzi (selective herbicides) ya kufanya palizi kwenye tikiti.  Madawa chaguzi, ni yale madawa ambayo unapiga shambani alafu yanaua magugu lakini hayana madhara kwa mazao. Mfano dawa yenye kiambato (active ingredient) cha Oxyfluorfen  ya kupiga kwenye vitunguu, inapopigwa kwenye shamba la vitunguu, inaangamiza magugu lakini vitunguu vinabaki salama. Kwa upande wa zao la tikiti bado hakuna dawa za namna hiyo.

Hivyo magugu kwenye tikiti yanahitahitji kufanyiwa palizi kwa mkono au jembe wakati mimea ikiwa midogo. Epuka kufanya palizi wakati tikiti limeshaanza kutoa maua.

Kama umefanya palizi mapema na bado kipindi cha utoaji maua pakawa na mgugu basi subiri kidogo, kipindi cha utoaji maua kikiisha tu, basi ng’oa hayo magugu kwa mkono, huku ukiepuka kugusagusa mimea ya tikiti.

Uwekaji wa Matandazo (Mulching)
Njianyingine ya kudhibiti magugu ni njia ya kuweka matandazo (mulching). Kuna ana mbili za matandazo, ambayo ni matandazo ya Asili (orgnic Mulch) na Matandazo yasiyo ya asili (inorganic mulch).

Uwekaji wa matandazo ya asili (Organic mulching)
Njia hii inatumia nyasi/majani yaliyokauka, vumbi la miti (saw dust) au wengine wanayaita maranda. Maranda (Saw dust) ni yale masalia yatokanayo na upasuaji wa miti au mbao. Nyasi au maranda hayo yanatandazwa shambani. Ukipata maranda ni nzuri zaidi, maana baadaye yataoza haraka shambani na kuwa mbolea.

Uwekaji wa matandazo yasiyo ya asili (Inorganic mulching)
Njia hii ni utmiaji wa matandazo ya karatasi za plastic (plastic mulching) kudhibti magugu. Hapa karasi nyeusi (black polythene) ndiyo inatumika maana hairuhusu magugu kuota. Pia inasaidia kuhifadhi unyevunyevu kwenye udongo kwa maana zinapunguza upoteaji wa maji (evaporation). Faida yake nyingine ya njia hii ni kwamba inadumu muda mrefu zaidi ya matandazo ya asili. Matandazo haya (karatasi ya plastic)  yanaweza kutumika hata kwa misimu zaidi ya mine bila kubadilisha.

UMWAGILIAJI WA MATIKITI
Matikiti maji aslimia 90 yake ni maji, hivyo yanahitaji maji ili kukua. Mizizi ya mmea wa tikiti huenda chini sana kutafuta maji kwa ajili ya kusaidia matunda yenye njaa ya maji. Mwagilia mimea maji ya kutosha, ili angalau maji yaingie inchi 6 kwenda chini. Hii itafaa zaidi kama unatumia mifumo ya umwagiliaji wa matone (drip irrigation system).

Matikiti maji yanahitaji maji kipindi chote cha ukuaji, ila kipindi cha muhimu zaidi ni wakati yanapotengeneza matunda na wakati wa ukuaji wa matunda. Kama maji yasipotosha kipindi hichi, tunda halitaweza kukua kufikia uwezo wake wa mwisho (full potential), na inaweza kusababisha tunda kudumaa au kusababisha kudondoka. Kipindi hichi ni cha kuhakikisha mimea inapata maji kwa gharama yoyote.

Maji pia yanaweza kuharibu ubora wa matikiti endapo yatawekwa wakati ambao sio na kwa kiwango kisicho sahihi. Ikiwa na maana kwamba kipindi maji yanapohitajikwa kwa wingi, basi yawekwe kwa wingi, kipindi yanapohitajika kwa uchache basi yawekwe kwa uchache.

Maji ya umwagiliaji yanapaswa kudhibitiwa wiki mbili baada ya kutengeneza matunda, ili sukari iweze kutengenezwa vizuri. Usipodhibti maji kipindi hichi, maji yakizidi hupelekea matunda kukosa sukari na hivyo kukosa ladha, na kukosa ladha ni kupunguza ubora tikiti. Epuka uwekaji wa maji kipindi cha uvunaji kwa maana matunda yatapasuka na kusababisha kuoza.

UVUNAJI WA MATIKITI MAJI:
Hii ndiyo shughuli pkee katika uzalishaji wa matikiti isiyohitaji fedha zaidi bali ujuzi. Wakati huu kila mkulima ana shauku ya kuonja bidhaa yake ili kuona ina ladha gani. Tatizo sasa linakuja pale ukiambiwa utenganishe matikiti yaliyoiva na yale ambayo hayajaiva. Kama huna ujuzi utajikuta unaharibu matikiti mengi kwa kuyaonja ili kujua kama yameiva.

Jinsi ya Kutambua matikiti yaliyoiva (Baadhi ya dalili za Matunda yaliyoiva):
Kutambua matikiti yaliyoiva ni kazi rahisi sana, lakini kama huna maarifa utajikuta unavuna matunda ambayo hayajaiva kitu ambacho kitapunguza ubora wa matunda yako.

Tikiti lililoiva linatambuliwa kama ifuatavyo:
1. Tazama tumbo lake. Tumbo la tikiti ni ile sehemu ya upande wa chini wa titkiti iliyogusana na ardhi. Kwa tikiti lililoiva sehemu hii inayogusana na ardhi hua ya njano na sio nyeupe kama inavyokua kwenye matikiti ambayo hayajaiva.

2. Lipige kwa kidole au mkono. Tumia kidole chako kwa upande wa kucha au kiganja chako, kupiga tunda la tikiti pale katikati ya tunda kwa ubavuni. Tunda lililoiva litakua na sauti ya kama kuna uwazi kwa ndani unapoligonga. Au sauti ya ngoma.

Tikiti maji hutumia siku 60 hadi 120 toka kupanda hadi kukomaa, inaegemea zaidi na aina ya tikiti. Mfano zipo aina nyingine zinatotumia siku 60 hadi 80 kama sugar baby, MSHINDI F1, ANDAMAN F1, ADITI F1, zinatotumia siku 80 hadi 90 kama Sukari F1, Zebra F1, ANDAMAN F1, na zipo zile zinazochukua siku 100 hadi 120 kama Pata Negra F1. Mavuno ya tikiti hutegemea sana aina ya tikiti na matunzo. Unaweza kupanda aina zenye mavuno makubwa lakini matunzo yakawa duni, usitegemee kupata mavuno makubwa. Aina nyingi za chotara (Hybrid) zinauzao wa tani 15 hadi 25 kwa ekari (15 – 25 tones/acre)

Stori ya Mkulima aliyetengeneza million 30:
Mwezi huu mwanzoni, nilikua kwenye shughuli za kuwatembelea baadhi ya wakulima katika wilaya ya Sengerema, nilipata wasaa wakufika kwenye mashamba ya baadhi ya wakulima. Nikiwa kwenye shambala la mkulima mmoja katika kata ya Kasenyi, hapo shambani kulikua na wakulima kama 3 wengine, katika mazungumzo, ikaibuka stori ya kilimo cha matikiti kwamba ni dili sana kwa siku za leo. Kuuliza kwanini wakasema kuna mkulima mmoja hapo kijijini amekua ndio stori ya mjini kwa huko kwao, maana msimu uliopita alipata Milioni 30, (30,000,000) kwenye Kilimo cha tikiti. Nilipata hamasa ya kutaka kufahamu zaidi kuhusu huyo mkulima, na namna alivyoweza kupata kicheko kikubwa hivyo. Katika kuendelea kudadisi kwa kuuliza maswali, nikagundua kwamba mkulima huyo Alilima zaidi ya ekari 10, yaani hiyo milioni 30 aliipata kwenye hizo ekari zaidi ya 10. Kufanya mahesabu sawasawa, nikagundua kwamba kila ekari alipata milioni 2 na laki kadhaa tu. Kwa mkulima ambaye hayuko kimahesabu akiisikia hiyo milioni 30 anaweza kuona kama ni faida kubwa sana, lakini sio kubwa kivile kama walivyokua wanamwaga sifa. Kwa idadi ya ekari alizolima mkulima huyu, alipaswa akianguka sana basi ni milioni 40. Nilichogundua ni kwamba wakulima wengi wao wanaangalia zaidi Mapato Ghafi (Gross income) yaani yale mapato anyaoyapata baada ya kuuza mazao yake, bila hata ya kutoa gharama alizotumia kuzalishia  wakidhani ndio faida. Moja ya ujuzi au uwezo anaopaswa kua nao mjasriamali yeyote ni Uwezo wa kufanya mambo kimahesabu. Kabla ya kuanza kilimo fahamu gharama unazohitaji kuwekeza kwenye hicho kilimo,  halafu weka kumbumbukumbu ya gharama halisi unazotumia, ili badaye uweze kufahmu umepata faida kubwa, ndogo au umepata hasara.

Tunazo Huduma ambazo zinaweza Kukupa faida kubwa kwenye kilimo cha tikiti kuliko huyu mlima wa million 30.

Huduma ya Kwanza: Uchambuzi wa Gharama na Faida (Cost benefit Analysis – CBA)  wa Zao lolote utakalotaka kulima Kibiashara.

Kwanini CBA? Baadhi ya Manufaa ya kuanza na CBA ni:
CBA itakusaidia kujua Rasilimali na gharama zinazohitajika kwenye uwekezaji wa kilimo unachotaka kufanya. Hii itakusaidia kufanya maamuzi ya kuendelea na wazo la kulima zao hilo au itakubidi ufanye zao lingine.

CBA itakusaidia kujua makadirio ya mapato faida utakayopata. Hakuna mtu anayependa kufanya kitu bila kujua manufaa ya kile anachokifanya. Hivyo CBA itakupa picha ya kile utakachokipata.

CBA itakusaidia kujua mgawanyiko wa gharama zinazohitajika. Mfano kama kilimo cha tikiti kinahitaji mtaji wa milioni 2. Haina maana kwamba lazima uwe na hizo milioni mbili ndio uanze kilimo cha tikiti. Inaweza kua inahitajika laki 5, halafu baada ya mwezi ikahitajika milioni moja, halafu mwishowe ikahitajika laki 5. Sasa bila kujua mgawanyiko huo unaweza kudhani ni ngumu kufanya kilimo cha tikiti kwasababu ya mtaji mkubwa unaohitajika, kumbe unaweza kuanza na kiasi fulani. CBA itakupa picha kamili kwenye hilo.

Huduma hii pia inaambatana na ushauri wa mbegu nzuri kulingana na soko unalolilenga na ukuaji wake kwenye eneo unalotaka kulima. Pia namna ya kuipata mbegu Halisi (maana moja ya changamoto kwenye zao la tikiti ni kwamba baadhi ya mbegu ni feki, unaweza kununua mbegu ghali na mwishowe kumbe umechukua feki)

Huduma hii inapatikana kwa gharama ndogo ya 20,000/= (Elfu Ishirini tu).
Huduma ya Pili: Master Plan. Huu ni Muongozo au Mpango kazi wa Kilimo cha zao la Tikiti.
Mpangilio huu unakuonyesha shughuli zote za Shambani na muda wake wa kufanyika. Hii itawasaidia sana wale ambao wanataka kufanya kilimo lakini hawajui kipi kianze na kipi kifuate. Pia utawasaidia kuongeza faida wale ambao wamewahi kulima kilimo cha tikiti lakini hawakupata faida waliyotegemea. Muongozo huu utakuonyesha aina ya mbolea na kiasi kinachohitajika, aina za madawa ya magonjwa na wadudu na kiasi gani cha uchanganyaji wa dawa hizo, Umwagiliaji,  na mambo mengine mengi.

Gharama ya kutengnenezewa Mungozo (Master Plan) ni 20,000/= (Elfu Ishirini tu).
Kwa watakaohitaji Huduma zote mbili watafanyiwa kwa 30,000/= (Elfu thelathini tu)

KILIMO BORA CHA MATIKITI MAJI KILIMO BORA CHA MATIKITI MAJI Reviewed by Muungwana Blog on May 15, 2017 Rating: 5

No comments