JINSI YA KUTATUA CHANGAMOTO YA SOKO KWENYE KILIMO CHA BIASHARA


Image result for KILIMO BIASHARA
Karibu kwenye makala yetu ya leo ya USHAURI WA CHANGAMOTO ambapo tunaangalia zile changamoto zinazotuzuia kufikia malengo yetu tuliyojiwekea kwenye maisha. Hakuna njia iliyonyooka, kila kitu kina changamoto zake, na wakati changamoto inakusumbua, siyo rahisi kuona njia mbadala za kupita ili kutoka kwenye changamoto hiyo. Hapa ndipo tunapofanyia kazi kupitia kipengele hiki, kuziangalia changamoto hizi na hatua bora kuchukua.
Katika makala ya leo tunakwenda kuangalia changamoto ya masoko kwenye kilimo cha kibiashara. Kabla hatujaingia na kuangalia changamoto hii, tuangalizie kwanza kilimo kwa siku za hivi karibuni. Kwa sasa kilimo kimekuwa tu siyo kilimo, bali kimekuwa ujasiriamali na hata biashara kwa wengi ambao wanataka kujikwamua kiuchumi. Kadiri hali ya uchumi inavyokuwa ngumu, kukosekana kwa ajira na hata kutoridhishwa na kipato kwa wale walioajiriwa, watu wengi wamelazimika kuingia kwenye kilimo.

Kilimo kinaonesha dalili nzuri za kuweza kumtoa mtu yeyote anayekifanya vizuri na kwa ubunifu. Hii ni kwa sababu bado uhitaji wa mazao ya kilimo ni mkubwa ndani na nje ya nchi. Lakini pamoja na uwezo huu wa kilimo kuwatoa watu kifedha, bado changamoto ni nyingi. Changamoto zinaanzia kwenye upatikanaji wa shamba bora, upatikanaji wa maji ya umwagiliaji kwa sababu mvua sio za uhakika. Upatikanaji wa mbegu bora pia ni changamoto kubwa, wasaidizi kwenye shughuli hizi za kilimo nao wamekuwa changamoto, siyo watu wote wapo tayari kujitoa. 

Ukiweza kuvuka changamoto zote hizo, za kuanzia shamba mpaka kuvuna, kuna changamoto kubwa inayokuwa mbele yako mkulima, changamoto hii ni soko. Kumekuwa na watu wa katikati ya mkulima na mlaji, watu hawa wanajulikana kama madalali. Hawa wamekuwa wakipata faida mara dufu kuliko hata mkulima aliyeteseka shambani kwa muda mrefu. Je unawezaje kutatua changamoto hii ya soko kwenye kilimo cha kibiashara? 

Hapa tutakwenda kushirikishana mbinu za kufanya hivyo. Lakini kabla hatujaingia kwenye ushauri wenyewe, tusome maoni ya mwenzetu aliyetuandikia kuomba ushauri juu ya hili; 

Nina malengo ya kulima kilimo cha biashara cha matikiti maji, lakini changamoto kubwa ninayoiona ni soko, wakulima tunalanguliwa sana hasa mashambani na ukizingatia mimi ni mkulima ninayetaka kuanza, naomba msaada katika hili. Naishi dar maeneo ya kigamboni, Ahsante. David Haule. 

Kwa mwenzetu David pamoja na wengine wote ambao mnapitia changamoto ya masoko kwenye kilimo, hapa kuna mambo muhimu sana kuzingatia ili kuondokana na changamoto hii ya masoko. 

KWANZA; Angalia aina ya kilimo unachofanya au kutaka kufanya. 
Kumekuwa na wimbi la watu kukimbilia kilimo cha zao fulani, kwa sababu tu kuna watu wachache waliofanya kilimo hiko na wakafanikiwa. Mfano mzuri ni kilimo cha matikiti maji. Zao hili ndiyo limekuwa kimbilio kwa kila anayefikiria kuingia kwenye kilimo. Hii ni kutokana na ufupi wa msimu wake na usambazaji wake kuwa mkubwa. 

Kuna sheria moja ya uchumi inasema kwamba kadiri kitu kinavyopatikana kwa wingi, bei yake inakuwa ndogo. Na hili ndilo limekuwa linatokea kwa wakulima wanaolima mazao yanayoliwa na wengi. Unapofika msimu wa mavuno, bei inakwenda chini kwa sababu kila mtu anauza. Na hapa ndipo madalali wanaponufaika sana kwa kununua kwa bei ya chini sana na kwenda kuuza kwa bei ambayo wao watapata faida. Hawajali kama bei wanayonunua kwako mkulima itarudisha gharama zao, wanachoangalia ni kama wao wanapata faida. 

Hatua ya kuchukua hapa ni epuka kulima mazao ambayo kila mtu anakimbilia kulima, na ikiwa ndiyo chaguo lako basi una vitu viwili vya kufanya, cha kwanza ni kulima tofauti na msimu, yaani ujipange ili unapovuna upatikanaji usiwe mkubwa. Cha pili soma namba mbili hapo chini. 

PILI; Hakikisha unatoa mazao bora sana. 
Watu wengi wanapokutana na changamoto hiyo hapo juu, pale madalali wanapotaka kununua mazao yao kwa bei ya chini, hukataa na kuamua kupeleka mazao yao sokoni wao wenyewe. Na hapa ndipo wanapokutana na ukweli mchungu, wakifika sokoni, watu wanachagua ubora. Kwa zao kama tikiti maji, watu wanaangalia mbegu na ukubwa wa tunda. Ukipeleka matunda madogo utajikuta unapata hasara kubwa kuliko hata ungemuuzia dalali shambani. 

Hivyo hakikisha kwa kilimo chochote unachochagua kufanya, mazao unayotoa ni bora sana. Unapokuwa na mazao bora, hata dalali akifika shambani, hatakuwa na nguvu ya kukuburuza, na akitaka kufanya hivyo unaweza kuamua kuyapeleka sokoni wewe mwenyewe. Kwa zao la tikiti, unapokuwa na matunda makubwa, mnahesabiana na dalali na kuuziana kwa bei fulani kwa kila tunda, lakini ukiwa na matunda madogo ananunua kama mzigo hivyo anakadiria tu bei. 
Kilimo chochote unachochagua kufanya, hakikisha unatoa mazao bora sana. Weka juhudi kubwa, fuatilia kwa karibu kuhakikisha unatoa mazao ambayo unaweza kuyauza popote pale. 

TATU; Tafuta njia mbadala za kusambaza mazao yako. 
Kama umechagua kufanya kilimo cha kibiashara, basi unahitaji kutafuta njia mbadala ya kusambaza mazao yako. Unaweza kuyasambaza kwa kupeleka sokoni na kuuza kwa jumla, au unaweza kuyasambaza kwa kuuza kwa rejareja. Unachohitaji ni kuangalia wapi ambapo mazao yako yanaweza kuhitajika kisha tengeneza mtandao wako wa masoko. Kwa mazao ya nafaka unaweza kuuza moja kwa moja kwa walaji kama mahoteli, shule na hata taasisi nyingine zinazotumia nafaka katika vyakula. 

Ili kuweza kusambaza mazao yako mwenyewe, unahitaji kuwa na mazao bora, ambayo yatawafanya watu wayafurahie. 

NNE; Ongeza thamani ya mazao yako. 
Tatizo kubwa ambalo wakulima wengi wanapitia ni kukosa taarifa za kutosha, na hivyo wenye taarifa wanazitumia kufaidika zaidi. Kwa mfano mtu analima mpunga na kuuza ukiwa kama mpunga. Mtu mwingine anaununua na kukoboa, anapata mchele na kuupanga katika viwango tofauti. Anatafuta vifungashio na kufunga mchele huo na kuuza kwenye maeneo mbalimbali, ikiwepo kusambaza nje ya nchi. Kwa mkulima wa kawaida anaweza kuona hili ni jambo kubwa sana ambalo yeye hawezi kufanya. Lakini kwa kupata taarifa sahihi mkulima yeyote anaweza kuongeza thamani kwenye mazao yake. 

Kwenye zao lolote unalolima, jiulize ni kwa namna gani unaweza kuongeza thamani ili usiuze likiwa ghafi. Bei ya kitu ghafi na kilichoongezwa thamani ni tofauti kubwa sana. Fikiria ni namba gani unaweza kuongeza thamani kwenye zao unalolima. 

TANO; Pata taarifa, jielimishe kuhusu kile unachozalisha na kilimo kwa ujumla. 
Kuna taarifa nyingi sana kuhusu kilimo lakini wakulima wanazo chache mno. Wakulima wengi wamekuwa wavivu kujifunza vitu vipya kuhusu kilimo. Wengi wamekuwa wakilima kwa mazoea, wengine wamekuwa na imani zisizo sahihi kwenye kilimo kuhusu matumizi ya mbegu za kisasa na mbolea za viwandani. Jielimishe kuhusu kile kilimo unachofanya, jua wengine wanaolima na wakafanikiwa ni mbinu gani wanatumia. Jua mbegu bora zaidi ni zipi na zinahitaji mazingira gani. 

Unapoamua kufanya kilimo sehemu yako ya kujiingizia kipato, chukulia ile ndiyo kazi yako, na mara zote angalia fursa ya kujifunza kupitia kilimo unachofanya. Unapolima na kupata mazao ambayo siyo viwango ulivyotarajia, jiulize ni wapi ulikosea na wakati mwingine usirudie kosa hili. 

Kilimo siyo rahisi hata kidogo, unahitaji kuweka juhudi kubwa kwenye kulima, kujifunza na hata kusambaza mazao yako. unahitaji kuweka juhudi kubwa ili kuweza kufikia malengo yako ya kifedha kupitia kilimo. Jambo zuri ni kwamba inawezekana, kwa sababu wapo wengi walioweza. 

JINSI YA KUTATUA CHANGAMOTO YA SOKO KWENYE KILIMO CHA BIASHARA JINSI YA KUTATUA CHANGAMOTO YA SOKO KWENYE KILIMO CHA BIASHARA Reviewed by BENSON on March 09, 2018 Rating: 5

No comments