UFUGAJI BORA WA NGURUWE.
Ufugaji wa Nguruwe ni lazima uwe wa kisasa ili
kupata kile kilichokuwa bora. Jamii nyingi hapa Tanzania huchukulia nguruwe
kama mnyama mchafu na asiyefaa kuwa karibu naye na hata kwa matumizi. Lakini ukweli
ni kwamba ukiamua kufuga nguruwe ni mradi ambao unafaida lukuki. Unaweza
kuanzisha mradi wa nguruwe kwa gharama ndogo lakini baada ya kipindi cha miezi
tisa tu ukaanza kujipatia kipato kutokana na ufugaji huo.
Ufugaji
Kwa kawaida nguruwe wanafugwa na watu wa kada zote, wafugaji wadogo wadogo na
hata wakubwa. Aina hii ya ufugaji huweza kumpatia mkulima kipato pamoja na
lishe kwa familia, na hauhitaji gharama kubwa.
Banda
Nguruwe wanahitaji kuwa na banda lililojengwa kwa vifaa nafuu. Unaweza kutumia
mchanga na simenti kuweka sakafu, ama ukatumia udongo wa mfinyanzi kwa ajili ya
kuweka sakafu. Ukubwa wa banda unategemeana na idadi ya nguruwe unaotaka
kufuga. Mita 3 kwa mita 2.5 zitawaweka guruwe 8-10 wanaonenepeshwa kwa soko au
nguruwe jike mmoja na nguruwe dume mmoja.
Malisho
Ulishaji wa nguruwe ni rahisi kwa kuwa wanakula aina mbalimbali za vyakula
kulingana na mazingira wanayofugwa. Unaweza kuwalisha kwa kutumia majani laini
ya aina mbalimbali, na pia hulishwa kwa kutumia masalia ya nafaka (pumba).
Unaweza kuwalisha kwa kutumia mashudu au pumba aina ya Wheat Poland. Pia
unaweza kuwalisha kwa kutumia mabaki ya jikoni.
Kuzaliana
Nguruwe hubeba mimba kwa kipindi cha siku 114, ambazo hugawanyika kwa miezi
3, wiki 3 na siku 3. Nguruwe mmoja ana uwezo wa kuzaa watoto 6 hadi 14 kwa mara
moja. Watoto wa nguruwe (piglets) huanza kula chakula cha kawaida wanapofika
umri wa mwezi mmoja na nusu mpaka miezi miwili. Endapo nguruwe watapata matunzo
mazuri, baada ya miezi 8 wanakuwa na uzito kati ya kilo 50-70 na wanaweza
kuuzwa.
Matunzo
Baada ya nguruwe kuzaa anatakiwa kupatiwa chakula cha kutosha na cha kutia
nguvu ili kupata maziwa ya kutosha kwa ajili ya watoto wake. Watoto wa nguruwe
wachomwe sindano ya madini ya chuma (Iron injection) baada ya siku moja au
mbili toka kuzaliwa. Hii ni muhimu sana vinginevyo wanaweza kufa wote. Kata
meno (tooth clipping) baada ya miezi mitatu. Unaweza kuhasi madume (castration)
baada ya miezi miwili.
Magonjwa yanayoathiri nguruwe
Kuna aina nyingi za magonjwa yanayoshambulia nguruwe, lakini yapo yale
yaliyozoeleka ambapo ni lazima kukabiliana nayo ili kuwa na ufugaji wenye tija.
Ugonjwa wa miguu na midomo
Ugonjwa huu huathiri nguruwe sehemu za miguu na midomo. Ni ugonjwa ambao
hushambulia nguruwe mara kwa mara hasa wasipokuwa na matunzo mazuri. Ugonjwa wa
miguu na midomo, hudhoofisha nguruwe kwa haraka sana, ikiwa ni pamoja na
kupungua uzito.
Chanjo: Chanjo kwa ajili ya ugonjwa wa midomo na miguu (FMD
vaccine) hutolewa kila baada ya mwaka mmoja. Hii inasaidia kuwaweka nguruwe
wako katika hali nzuri zaidi bila kushambuliwa na magonjwa hayo.
Tiba: Ugonjwa huu hauna tiba halisi. Inapotokea nguruwe wakawa
wameshambuliwa kinachofanyika ni kutibu magonjwa nyemelezi kwa kutumia
antibiotics.
Homa ya Nguruwe (Swine fever)
Virusi vinavyosababisha ugonjwa wa homa ya nguruwe
huenea kwa haraka sana miongoni mwa makundi ya nguruwe,
na huua kwa haraka sana, lakini hauna madhara kwa binadamu na
hauambukizwi kwa binadamu. Nguruwe walioambukizwa waanshikwa na
vindonda ama mapunye kwenye ngozi. Pia masikio na ngozi huwa
mekundu.
Chanjo: Ugonjwa huu hauna chanjo wala tiba. Kinachofanyika mlipuko
unapotokea ili kuwa salama ni kuwateketeza nguruwe wote walioathirika na kuanza
upya. Unaweza kuteketeza kwa kuwachoma moto.
Muhimu: Baada ya kuwateketeza nguruwe wagonjwa,
safisha banda kisha nyunyiza dawa aiana ya Acon au Ectomin, na uache banda wazi
kwa kipindi cha wiki moja kabla ya kuweka nguruwe wengine.
Ugonjwa wa mapafu (Pneumonia)
Huu ni ugonjwa unaoshambulia sehemu za koo na mapafu ya nguruwe, ambapo
husababisha kukohoa na kupumua kwa shida. Ugonjwa huu husababishwa na bacteria
(Secondary bacterial), joto kupita kiasi, vumbi na gesi inayotokana na madawa
makali.
Tiba: Homa ya mapafu kwa nguruwe inatibika kwa kutumia antibiotics.
Pamoja na kuwaweka wanyama sehemu safi, isiyo na baridi kali au joto la
kupitiliza kiwango.
Kimeta (Anthrax)
Huu ni ugonjwa unaosababishwa na bakteria wanaojulikana kama Bacillus
anthracis, wadudu hawa wanabaki kuwa hai kwa muda mrefu na wanaweza kuwa kwenye
udongo wakiwa hai kwa kipindi cha miaka mingi.
Chanjo: Chanja nguruwe wako dhidi ya kimeta kama
utakavyoelekezwa na wataalamu wa mifugo walio karibu nawe.
Tiba: Unaweza kutibu nguruwe wako kwa kutumia dawa aina ya
Penisilin au Oxytetracycline.
UFUGAJI BORA WA NGURUWE.
Reviewed by BENSON
on
August 13, 2017
Rating:
No comments