NJIA 10 ZA KUPUNGUZA MAGONJWA YA MLIPUKO WA KUKU.
Mlipuko
wa magonjwa ni moja ya sababu za hasara kubwa kwa wafugaji na vifo
vinavyotokea kwa wakati mmoja. Pindi mfugaji anapokumbwa na janga la
vifo vya ndege, kabla ya kufikia mwisho wa mzunguko wa uzalishaji hivyo
basi asitarajie kupata faida nzuri mara baada ya mauzo.
Hasara itokanayo na vifo inaweza kuepukika au kupunguzwa na kutokea kwa kiasi kidogo.
Hili linawezekana, ifuatayo ni namna ya kufanikisha hilo;-
1. Osha vyombo vya maji kila wakati na mwaga maji yaliyobaki.
Hakikisha
unamwaga maji yaliyosalia mbali na kuosha chombo na sabuni kila siku,
weka maji safi yasiyo na dawa na wala usitumie maji ya mto au yale
usiyoyajua chanzo chake. Kama utaweka maji dawa basi tumia ‘vitamini’
muhimu kama ‘vitalyte’ ambazo zinasaidia kuua vijidudu.
2. Wape maji kabla ya chakula.
Ndege
wapo tofauti na binadamu au wanyama wengine. Hakikisha unawapa maji
kabla ya chakula hasa kama unatumia maranda, hii ni kuhakikisha
hawakanyagani wanapogombania chakula sehemu moja.
3. Usiwape chakula chenye uvundo.
Ni
hatari sana kuwapa ndege/kuku wako chakula chenye ukungu, ni kama
kuwalisha sumu. Ukungu au uvundo huwafanya kuku waugue kirahisi sana au
kuwasababishia madhara mengine kiafya.
4. Fuatilia kwa makini ratiba za chanjo na tiba.
Mfugaji
unatakiwa kupata tiba na chanjo sahihi kwa ndege unaowafuga. Kuchanja
ndege kutasaidia sana kuimarisha kinga yao dhidi ya magonjwa hatari kama
kideri, ndui, gumboro na mareksi. Dawa kama vile za minyoo na
antibayotiki ni muhimu sana kwenye afya ya kuku na ndege wengine.
5. Nunua na fuga vifaranga wenye afya njema.
Matatizo
mengi ya afya ya ndege au kuku ni matokeo ya maisha duni ya awali ya
kuku hao au huwa wanarithi. Itambulike hivi, baadhi ya ndege/kuku
hurithi afya mbovu kutoka kwa wazazi wao. Hata hivyo baadhi ya
watotoleshaji pia wanafuga kuku ambao wana afya mbovu na hivyo huuza
vifaranga au mayai dhaifu na waathirika na hivyo mnunuzi anajikuta
ananunua matatizo.
6. Zuia mkusanyiko wa hewa ya ammonia.
Maranda
yakikaa muda mrefu bandani, hufanya hewa ya ammonia kuzalishwa kwa
wingi, hewa hii hufanya ndege wapaliwe hadi kufa. Kila mara ondoa
maranda mabichi au yaliyovunda na weka mengine haraka iwezekanavyo ili
kuepuka vifo vitokanavyo na kupaliwa au magonjwa ya mfumo wa hewa.
7. Zuia panya na vicheche.
Banda
la ndege linatakiwa lisiruhusu panya au wanyama wadogo jamii ya
kicheche kuingia ndani, na ndege wa mwituni kwa kuweka nyavu au
kupulizia dawa, ikiwa watapata upenyo wataua na kula ndege/kuku wako na
kuacha vimelea vya magonjwa wanapokula vyakula au kunywa maji ya ndege
wako.
8. Zingatia usafi na usalama.
Kipengele
hiki cha usafi na usalama ni kipana ila unachotakiwa kufanya ni
kuzingatia usafi nje na ndani ya banda. Unatakiwa ukamilishe usalama wa
afya ya ndege/kuku wako kila wakati, jambo ambalo wafugaji wengi
hutekeleza pindi wanapo shitukizwa na mlipuko wa magonjwa.
9. Wape chakula cha kutosha.
Ndege
kama walivyo wanyama wengine, hawawezi kukua na kuzalisha vizuri endapo
wanapewa chakula duni na kidogo. Chakula bora ni msingi imara na ni
kinga kwani chakula duni hupelekea uzito kupungua na kinga kuwa chini na
hivyo hufa mapema. Jitahidi wape kuku chakula cha kutosha ila
usiwazidishie.
10. Wakinge dhidi ya baridi kali.
Baridi
kali ni adui kwa afya ya wanyama, ndege na binadamu. Jaribu kila
uwezavyo kuwakinga kuwakinga ndege wako na baridi kali kwani inaua
haraka sana kama sumu. Wawekee chanzo cha joto wakati wa baridi au jenga
banda ambalo halipitishi baridi kali.
Hizo ndizo njia muhimu ambazo ukiwa mfagaji unazoweza kuzitumia ili kukinga magonjwa yanatokanayo na kuku.
NJIA 10 ZA KUPUNGUZA MAGONJWA YA MLIPUKO WA KUKU.
Reviewed by BENSON
on
February 08, 2018
Rating:
No comments