KANUNI SITA {6} ZA UFUGAJI BORA WA KUKU.
Kuku wa kienyeji ni wazuri kwa ufugaji kwa sababu: Wanavumilia sana magonjwa,
Ni rahisi kuwahudumia, Chakula chao ni cha bei ya chini, Wavumilivu wa hali
tofauti za hewa, Hawahitaji uangalizi wa karibu, na soko lake ni kubwa sana na
bei nzuri (Mayai trei moja SHs 10,000 mpaka 15,000, kuku wakubwa wanaanzia SHs
15,000 mpaka 30,000). Hii haimaanishi kwamba, uwaache kuku bila uangalizi,
kwani nao hupata magonjwa kama wasipo patiwa chanjo sahihi, hupungua uzito na
uzalishaji mayai hushuka kama wasipo patiwa chakula chenye virutubisho vyote.
Hapa naelezea vitu muhimu katika hii formula ya ufugaji kuku wa kienyeji kwa
mafanikio:
1. Aina ya kuku: Chagua aina ya kuku wenye uwezo wa kutaga mayai
mengi na wakati huohuo, kuzalisha nyama nyingi. Hii itakupa faida kote, kwenye
upande wa nyama na upande wa mayai. Kuku hawa wanajulikana kama Chotara,
wanatabia sawa na kuku wa kienyeji wenye asili ya Tanzania wanaopatikana maeneo
mengi nchini; kutokana na uvumilivu wao wa magonjwa na hali tofauti za
mazingira. Pia wanauwezo wa kutaga mayai mengi (Wastani wa mayai matano kwa
wiki) karibu sawa na kuku wa kizungu. Aina ya kuku hawa ni kama vile, Chotara
wekundu (Rhode Island Red), Black Australorp (Weusi/Malawi), Barred Plymouth
Rocks (Madoa), New Hamshire Red, Kuroila wanapatikana sana Uganda, na Kari
kutoka Kenya. Hizi ni aina ya kuku zinazo patikana Tanzania.
2. Chanjo: Kama nilivyosema mwanzo, kuku wa kienyeji ni
wavumilivu wa magonjwa lakini si kwamba hawayapati, kuna magonjwa ambayo ni
hatari pia kwa kuku wa kienyeji. Chanjo ni muhimu kuwaepusha na hatari ya
kuyapata magonjwa haya. Chanjo muhimu kwa kuku wa kienyeji ni; New Castle,
Gumboro, Marek’s na Ndui ya kuku. Fuata utaratibu wa chanjo kutokana na ushauri
wa daktari. Nitawaletea pia makala ya magonjwa na chanjo hivi karibuni.
3. Chakula: Kuku wa kienyeji pia wanahitaji mchanganyiko sahihi wa chakula,
ili waweze kukupatia mazao mengi na bora, na kuwaepusha na magonjwa. Zipo
fomula mbalimbali za chakula kutokana na umri wa kuku, na aina ya kuku. Kuku
wote wanahitaji chakula chenye mchanganyiko sahihi wa Madini, Vitamini,
Protini, Fats, Wanga, Vyakula vya kulinda mwili ili usipatwe na maradhi, na
Maji safi. Muhimu kuwapatia kuku majani kama ziada ya chakula, hii hupunguza
gharama za chakula na kuwafanya kuku waonekane wenye afya bora. Ni vizuri
kuwapatia vifaranga chakula spesheli cha dukani kama huna ujuzi wa kutengeneza
mwenyewe. Kwani vifaranga wengi hufa kutokana na kutokupata chakula chenye
mchanganyiko sahihi kwao. Kuku wa mayai pia wanahitaji mchanganyiko sahihi ili
waweze kutaga mayai kwa wingi.
4. Banda: Kuku wa kienyeji pia, wanahitaji banda au nyumba ya
kuku imara ili kuweza kuwakinga na baridi kali, wanyama hatari, na wizi. Banda
pia liwe na semu nzuri za kutagia na sehemu za kulala ziwe juu , kwani kuku
hupendelea kulala juu. Ni muhimu banda liwe katika hali ya usafi muda wote. Kwa
hivyo ni vizuri linyanyuliwe juu kidogo ili kuruhusu uchafu kuanguka chini na
lijengwe ka kutumia mbao, mabanzi, milunda, nyavu, na mabati. Vifaranga
wanahitaji kutenganishwa na kuku wakubwa. Banda si lazima liwe la gharama
kubwa, kwani mafanikio ya ufugaji wa kuku ni vile unavyo waangalia na si banda.
Mada inayohusu mabanda bora ya kuku itakuja hivi karibuni.
5. Majogoo kwa majike: Ili mayai mengi yaweze kutotolewa, ni vizuri
jogoo mmoja aweze kuwahudumia majike wasio zidi 7. Kwani kuku wanaweza kutaga
bila ya jogoo, lakini mayai hayatoweza kuleta kifaranga. Ili mayai yalete
vifaranga ni lazima yawe yamerutubishwa (Fertilized eggs) na jogoo. Kwa hivyo
ni vizuri kuweka Jogoo 1 kwa majike 7, hivyohivyo Jogoo 2 majike 14, Jogoo 3
majike 21, n.k. Pia hakikisha kuku wanao tumika kuendeleza kizazi ni wale wenye
afya bora.
6. Vyombo vya chakula: Hakikisha vyombo vya chakula ni visafi na
vinawatosheleza kuku wote. Vyombo hivi ni vizuri vifanyiwe usafi wa mara kwa
mara, ili kuwaepusha kuku na magonjwa. Maji machafu huwa ni chanzo kikuu cha
magonjwa hasa ya kuhara. Hakikisha kuku wako wanabadilishiwa maji angalau mara
mbili kwa siku.
KANUNI SITA {6} ZA UFUGAJI BORA WA KUKU.
Reviewed by BENSON
on
January 14, 2018
Rating:
No comments