MAMBO YA MSINGI YA KUZINGATIA KABLA YA KUFANYA CHANJO KATIKA UFUGAJI KUKU.
Watu wengi wamekuwa wakianzisha miradi ya ufugaji wa kuku bila
kuzingatia kanuni bora za utekelezaji wa mradi huo. Moja ya mambo ambayo
wafugaji mara nyingi husahau kuzingatia ni utoaji wa chanjo sahihi na kwa muda
muafaka.
Ni muhimu kufahamu mambo unayotakiwa kuzingatia katika kuwapatia
kuku chanjo. Wakati wa kutayarisha mpango wa kuchanja kuku kwa ajili ya kinga
dhidi y magonjwa, kuna vipengele vikuu sita ambavyo unatakiwa uvifahamu na
kuvizingatia kama ifuatavyo:
1. Vifaranga vinavyoanguliwa kwa pamoja: Iwapo una
kundi zaidi ya moja la vifaranga wanaoanguliwa, weka utaratibu wa chanjo ambao
utapunguza uwezekano wa magonjwa kuenea shambani.
2. Umri wa kuchanja kuku: Kwa kuku ambao wanatarajiwa
kutaga mayai au kuwa kuku wazazi, chanjo nyingi hutolewa si zaidi ya mwezi
mmoja kabla ya kuku kuanza kutaga.
3. Magonjwa makuu katika eneo husika: Ni muhimu
sana kuelewa magonjwa ya kuku yaliyopo katika eneo lako kabla ya kuandaa
program ya uchanjaji, kwa magonjwa ambayo chanjo zenye vimelea hai hutumika.
4. Hali ya kiafya ya kuku watakaochanjwa: Usiwape
chanjo kuku ambao wanaonesha dalili za kuathirika kwa mfumo wa hewa au
wanaonesha kuwa na minyoo au wadudu wengine. Kwa kuku walio na dalili hizi
chanjo zinaweza kuleta madhara.
5. Aina ya kuku watakaochanjwa: Kuku wanaofugwa kwa ajili ya
nyama wanahitaji kinga ya muda mfupi, hivyo basi chanjo moja inaweza kutosha.
Lakini kuku wa mayai na kuku wazazi wanahitaji mpango wa chanjo ambayo
itawakinga na magonjwa kwa kipindi chote wanapokua na kutaga.
6. Historia ya magonjwa katika shamba: Kabla ya
kuandaa mpango wa chanjo, lazima ufahamu ni magonjwa gani yaliyoenea katika
shamba.
• Kama unataka kuingiza kuku wapya kutoka mahali ambako ugonjwa
umeshawahi kutokea, kuku hao wachanjwe wiki 3 kabla ya kuwaingiza shambani.
• Iwapo utatumia chanjo yenye vimelea hai, hakikisha kwamba
magonjwa hayo yameshawahi kutokea katika shamba husika. Usitumie chanjo hizi
katika shamba ambalo ugonjwa huo haujawahi kutokea au kutambuliwa.
• Wasiliana na mashamba jirani kufahamu iwapo wanatumia chanjo
zenye vimelea hai.
Mambo muhimu ya kuzingatia
• Hakikisha unazingatia kwa makini masharti ya mtengenezaji wa
chanjo: Jinsi ya kuhifadhi, kutayarisha na njia inayotumika kumchanja kuku.
Wakati wote zingatia masharti ya mtengenezaji kuhusu uhifadhi wa chanjo ili
isipoteze nguvu.
• Fuata ushauri wa daktari wa mifugo unapoandaa mpango wa chanjo
• Watumie wataalamu waliopatiwa mafunzo ya utoaji chanjo
• Chagua aina ya chanjo kulingana na umri na hali ya kiafya ya
kuku
• Fanya usafi wa mara kwa mara katika mabanda ili kupunguza
wingi wa vimelea kwenye mazingira
• Tumia maji ambayo hayajawekwa dawa au kemikali kwa ajili ya
kuchanganyia chanjo, kwa mfano maji ya kisima, mvua na kadhalika. Maji ya
kuchanganyia chanjo yawe na ubaridi, yasiwe moto.
• Changanya chanjo kabla ya kutumia na iwekwe mbali na kuku.
• Pata ushauri wa daktari wa mifugo kabla ya kuchanja kuku
wagonjwa au wale ambao hawako katika muonekano mzuri.
• Siku ya chanjo, usiwape kuku maji kwa masaa 3 – 4 ili waweze
kunywa maji yaliyowekwa chanjo kwa haraka.
• Zoezi la uchanjaji lifanyike haraka ili kupunguza usumbufu kwa
kuku.
• Tenganisha kuku waliochanjwa na wale ambao hawajachanjwa.
• Baada ya kuchanjwa, kuku wawekwe kwenye banda linalopitisha
hewa vizuri.
• Baada ya kila zoezi la kuchanja, wafanyakazi wabadilishe
mavazi, viatu/buti zisafishwe na kuwekwa dawa, na vifaa vilivyotumika viwekwe
dawa ya kuua vimelea.
• Fuata utaratibu uliowekwa wa kuharibu/kusafisha vifaa
vilivyotumika kuchanja.
• Weka kumbukumbu za uchanjaji.
MAMBO YA MSINGI YA KUZINGATIA KABLA YA KUFANYA CHANJO KATIKA UFUGAJI KUKU.
Reviewed by BENSON
on
October 12, 2017
Rating:
No comments