KILIMO BORA CHA NYANYA CHUNGU.
Zao hili pia hujulikana kwa jina la Mshumaa, "Nyanya Chungu",
"Ngogwe" au "Ntongo". Huu ni mmea wa kitropiki, na kustawi
kwake karibu ni sawa na bilinganya.
Mmea hukua na kufikia urefu wa meta moja hadi moja na unusu na matawi
na majani yake hufanya kichaka. Nyanya mshumaa zinaweza kuwekwa katika makundi
mawili: yaani aina itoayo matunda madogo madogo na machungu sana na aina itoayo
matunda makubwa na machungu kidogo.
Rangi ya matunda huwa kijani kibichi au kijani-njano, au njano-nyeupe,
na yakipevuka kabisa hugeuka mekundu. Matunda yafikia hatua ya kupevuka huwa
hayafai tena kuliwa, ila kwa kutoa mbegu za kupanda. Matunda hupikwa au
kukaangwa na kufanywa mchuzi, au huchanganywa na mboga zingine. Pia hupikwa
pamoja na ndizi.
Kupanda:
Miche huoteshwa kwa kupanda mbegu ambayo husiwa kwenye kitalu na
kutunzwa kama mazao mengine. Miche ifikiapo kimo cha sentimeta 10 hadi 15
hupandikizwa bustanini, kwa umbali wa sentimeta 90 kwa 90, hadi 120 kwa 120;
hii kutegemeana na ukubwa wa kichaka chake. Mimea ya "Ngogwe"
hutunzwa kama bilinganya, huhitaji ardhi yenye rutuba na unyevu wa kutosha.
Mazao huanza kuvunwa miezi miwili baada ya kupandikizwa, na uvunaji huendelea
kwa muda mrefu kidogo.
Magonjwa.
Nyanya Mshumaa ni mmea mgumu, kwani unaweza kustahimili upungufu wa
maji kuliko aina nyingine za Mboga. Vile vile haushambuliwi sana na baadhi ya
Magonjwa yasababishwayo na mvua au uchepechepe mkubwa. Ingawa yako magonjwa na
wadudu ambao hushambulia zao hili, madhara ya si makubwa sana kiasi cha kutisha
au kumkatisha tamaa mkulima. Usafi wa bustani na kubadilisha mpando wa mazao,
vinaweza kuondoa tishio hilo.
Kuvuna
Mboga huvunwa wakati zikiwa bado mbichi. Ili ziweze kukaa kwa muda
mrefu (hata majuma mawili) bila kuharibika, inapendekezwa kuzichuma pamoja na
sehemu ya vikonyo vyake. Vikonyo hivyo hukobolewa wakati wa kuzitayarisha
kupikwa. Kwa hiyo, zao hili linaweza kusafirishwa hadi masoko ya mbali bila
kuharibika.
Mkulima ongeza uzalishaji katika mazao ya mboga mboga ukuze uchumi
wako.
KILIMO BORA CHA NYANYA CHUNGU.
Reviewed by BENSON
on
September 27, 2017
Rating:
No comments