KILIMO BORA CHA NANASI
Nanasi ni tunda la kitropiki,
linalopendwa na walaji wengi kwa sababu ya ladha yake tamu na harufu yake
nzuri. Tunda hili laweza liwa mara tu baada ya kuvunwa, baada ya kulipika, au
kama juisi. Nanasi ni chanzo kizuri cha vitamin A na B, pia inakiwango kingi tu
cha vitamin C pamoja na madini kama vile: patasiam, magnesiam, kalsiam, na
madini chuma.
Asili ya nanasi inaaminika kuwa
ni Brazil na Paraguay huko Amerika ya Kusini. Hapa Tanzania, nanasi hulimwa
zaidi maeneo ya Bagamoyo, Kibaha (Pwani), Tanga, Mtwara, Lindi, Geita na
Mwanza. Lakini pia maeneo yote ya pwani ya Tanzania yanafaa kwa kilimo cha
nanasi.
Hali ya hewa inayofaa kwa
ukuaji wa nanasi
Kilimo cha nanasi kinapendelea
hali ya hewa ya joto na husitawi vema katika mwinuko kati ya mita 0-1750 kutoka
usawa wa bahari. Mwinuko wa mita 1300 hadi 1750. Mahitaji ya joto ni kati ya
nyuzi joto 18°C hadi 35°C.
Udongo unaofaa kwa kilimo cha
nanasi
Kwa kilimo cha nanasi chachu
(pH) ya udongo inayofaa ni 5.5 hadi 6.0, na hustawi vizuri zaidi katika udongo
tifutifu na udongo wenye kichanga usiotuamisha maji. Ingawa nanasi huweza
kustawi katika udongo wa aina yoyote ile, udongo wa mfinyanzi haufai kwa kilimo
cha nanasi.
Maandalizi ya shamba
Lima shamba kwa trekta, kwa
ng’ombe ama kwa jembe la mkono kwa kina cha sentimita 30 hadi 45. Shamba la
nanasi unaweza kulilima kwa sesa (flat-bed) au kwa matuta (furrows).
Kwa sesa: chimba mashimo kwa nafasi
ya sm.60 kati ya mistari, sm. 30 kati ya miche na sm. 80 kati ya kila mistari
miwili. Weka mbolea kianzio katika kila shimo na upande, hakikisha shamba lina
unyevu wa kutosha kabla ya kupanda. Weka tani 10 hadi 15 za mbolea ya kuku,
weka pia viganja 2 vya mbolea ya zizi katika kila shimo.
Upandaji wa mananasi
Zipo aina mbali mbali za
‘mbegu’ (machipukizi/maotea) lakini yale yanayochipua kutoka ardhini hufaa
zaidi na hukomaa mapema. Chagua machipukizi mazuri yenye umri mdogo na yenye
kulingana kwa ukubwa. Iweke miche kwenye kivuli kwa siku 3 kabla ya
kuipandikiza iweze kutoa mizizi haraka. Pandikiza mwanzoni mwa mvua za masika.
Nafasi iwe sm.60 kati ya mistari, sm. 30 kati ya miche na sm. 80 kati ya
mistari miwili. Pandikiza miche 50,000 katika hekta moja. Chovya miche kwenye
dawa ya Diazinon au Fention kwa muda wa dakika 25 kabla ya kuipandikiza ili
kuzuia mashambulizi ya wadudu.
Palizi
Palilia shamba mara kwa mara
ili kuhakikisha shamba halina magugu. Katika kilimo cha nanasi magugu
hudhibitiwa kwa palizi ya jembe, kung’oa kwa mkono ama matumizi ya viuagugu.
Matumizi ya viuagugu hurahisisha zaidi palizi ya nanasi ukizingatia kuwa nanasi
huwa na miiba katika ncha za majani yake ambazo huchubua ngozi endapo palizi za
jembe zitatumika. Njia nyingine ni matumizi ya matandazo (mulch) ya majani au
plastiki (plastic mulch) maalum kuzuia magugu.
Mahitaji ya mbolea ya mananasi
Weka mbolea ya NPK gramu 50
hadi 70 kwa kila mche wakati wa kupanda. Weka tena gramu 85 kwa kila mche baada
ya miezi 3 na pia miezi 3 baadae.
Wadudu na Magonjwa yanayosumbua
minanasi
Nanasi ni zao lisilosumbuliwa
na wadudu ama magonjwa mara nyingi. Hii ni faida kubwa sna kwa wakulima wa
nanasi! Hivyo endapo patatokea mashambulizi ya wadudu na magonjwa, ushauri
zaidi wa kitaalam utafutwe kukabiliana na tatizo husika. Hakikisha unakagua
shamba ili kuzuia wadudu kama wataonekana.
Uvunaji wa mananasi
Nanasi huanza kutoa maua miezi
12 hadi 15 baada ya kupanda kutegemeana na aina ya nanasi au maotea ya mbegu
yaliyotumika, muda wa kupanda na joto la mahali husika. Kwa kawaida nanasi
hukomaa miezi 5 baada ya kutoa maua, hivyo nanasi huchukua miezi 18 hadi 24
kukomaa/kuiva. Katika kilimo cha nanasi, mimea ikitoa maua kwa nyakati tofauti
tofauti itasababisha kuvuna kidogo kidogo na kwa muda mrefu. Kwa sababu hiyo
ndio maana ni muhimu kupanda kwa wakati mmoja mbegu zenye umri na ukubwa sawa.
Kwa wanaofanya kilimo cha
nanasi kibiashara (commercial pinapples production) hutumia kemikali aina ya
Ethrel (@ 100 ppm) mwezi mmoja kabla ya kuanza kutoa maua ili mimea mingi iweze
kutoa maua kwa wakaii mmoja, angalau 80% ya mimea yote.
Vuna wakati kikonyo cha nanasi
kimebadilika rangi kuwa njano ya dhahabu. Kata kikonyo cha nanasi chenye urefu
wa sm. 30 kikiwa kimeshikana na nanasi na upunguzie majani ya kichungi chake.
Utunzaji wa mananasi
Hifadhi nanasi katika eneo
lenye ubaridi huku kikonyo chake kikielekea juu. Hakikisha unauza nanasi mara
tu au siku 2 hadi 3 baada ya kuvuna ili kutunza ubora wake.
KILIMO BORA CHA NANASI
Reviewed by BENSON
on
August 10, 2017
Rating:
No comments