MAMBO YA MSINGI YA KUZINGATIA ILI KUPUNGUZA MAGONJWA YA KUKU
Mlipuko wa magonjwa ni moja ya sababu za hasara kubwa kwa
wafugaji na vifo vinavyotokea kwa wakati mmoja. Pindi mfugaji
anapokumbwa na janga la vifo vya ndege, kabla ya kufikia mwisho wa
mzunguko wa uzalishaji hivyo basi asitarajie kupata faida nzuri mara
baada ya mauzo.
Hasara itokanayo na vifo inaweza kuepukika au kupunguzwa na kutokea kwa kiasi kidogo.
Hili linawezekana, ifuatayo ni namna ya kufanikisha hilo;-
1. Osha vyombo vya maji kila wakati na mwaga maji yaliyobaki.
Hakikisha unamwaga maji yaliyosalia mbali na kuosha chombo
na sabuni kila siku, weka maji safi yasiyo na dawa na wala usitumie maji
ya mto au yale usiyoyajua chanzo chake. Kama utaweka maji dawa basi
tumia ‘vitamini’ muhimu kama ‘vitalyte’ ambazo zinasaidia kuua vijidudu.
2. Wape maji kabla ya chakula.
Ndege wapo tofauti na binadamu au wanyama wengine.
Hakikisha unawapa maji kabla ya chakula hasa kama unatumia maranda, hii
ni kuhakikisha hawakanyagani wanapogombania chakula sehemu moja.
3. Usiwape chakula chenye uvundo.
Ni hatari sana kuwapa ndege/kuku wako chakula chenye
ukungu, ni kama kuwalisha sumu. Ukungu au uvundo huwafanya kuku waugue
kirahisi sana au kuwasababishia madhara mengine kiafya.
4. Fuatilia kwa makini ratiba za chanjo na tiba.
Mfugaji unatakiwa kupata tiba na chanjo sahihi kwa ndege
unaowafuga. Kuchanja ndege kutasaidia sana kuimarisha kinga yao dhidi ya
magonjwa hatari kama kideri, ndui, gumboro na mareksi. Dawa kama vile
za minyoo na antibayotiki ni muhimu sana kwenye afya ya kuku na ndege
wengine.
5. Nunua na fuga vifaranga wenye afya njema.
Matatizo mengi ya afya ya ndege au kuku ni matokeo ya
maisha duni ya awali ya kuku hao au huwa wanarithi. Itambulike hivi,
baadhi ya ndege/kuku hurithi afya mbovu kutoka kwa wazazi wao. Hata
hivyo baadhi ya watotoleshaji pia wanafuga kuku ambao wana afya mbovu na
hivyo huuza vifaranga au mayai dhaifu na waathirika na hivyo mnunuzi
anajikuta ananunua matatizo.
6. Zuia mkusanyiko wa hewa ya ammonia.
Maranda yakikaa muda mrefu bandani, hufanya hewa ya ammonia
kuzalishwa kwa wingi, hewa hii hufanya ndege wapaliwe hadi kufa. Kila
mara ondoa maranda mabichi au yaliyovunda na weka mengine haraka
iwezekanavyo ili kuepuka vifo vitokanavyo na kupaliwa au magonjwa ya
mfumo wa hewa.
7. Zuia panya na vicheche.
Banda la ndege linatakiwa lisiruhusu panya au wanyama
wadogo jamii ya kicheche kuingia ndani, na ndege wa mwituni kwa kuweka
nyavu au kupulizia dawa, ikiwa watapata upenyo wataua na kula ndege/kuku
wako na kuacha vimelea vya magonjwa wanapokula vyakula au kunywa maji
ya ndege wako.
8. Zingatia usafi na usalama.
Kipengele hiki cha usafi na usalama ni kipana ila
unachotakiwa kufanya ni kuzingatia usafi nje na ndani ya banda.
Unatakiwa ukamilishe usalama wa afya ya ndege/kuku wako kila wakati,
jambo ambalo wafugaji wengi hutekeleza pindi wanapo shitukizwa na
mlipuko wa magonjwa.
9. Wape chakula cha kutosha.
Ndege kama walivyo wanyama wengine, hawawezi kukua na
kuzalisha vizuri endapo wanapewa chakula duni na kidogo. Chakula bora ni
msingi imara na ni kinga kwani chakula duni hupelekea uzito kupungua
na kinga kuwa chini na hivyo hufa mapema. Jitahidi wape kuku chakula cha
kutosha ila usiwazidishie.
10. Wakinge dhidi ya baridi kali.
Baridi kali ni adui kwa afya ya wanyama, ndege na binadamu.
Jaribu kila uwezavyo kuwakinga kuwakinga ndege wako na baridi kali
kwani inaua haraka sana kama sumu. Wawekee chanzo cha joto wakati wa
baridi au jenga banda ambalo halipitishi baridi kali.
Hizo ndizo njia muhimu ambazo ukiwa mfagaji unazoweza kuzitumia ili kukinga magonjwa yanatokanayo na kuku.
MAMBO YA MSINGI YA KUZINGATIA ILI KUPUNGUZA MAGONJWA YA KUKU
Reviewed by BENSON
on
February 14, 2018
Rating:
No comments