FAIDIKA KWA KULIMA KILIMO BORA CHA MCHICHA

Mchicha ni mboga za majani pia maua yake hutumika katika kutengeneza mchuzi rojorojo. Mbegu za mchicha ni chakula safi kwa watoto wachanga. Mbegu husagwa na kutengenezwa uji na zaidi ya hayo pia mchicha huweza kumwongezea mkulima kipato hasa pale mkulima huyo akijikita katika kilimo hiki.

MAHITAJI YA HALI YA HEWA KWAAJILI YA KULIMA MCHICHA.
Mchicha unahitaji maji ya kutosha katika kipindi chake chote cha ukuaji hadi kuvuna. Vilevile mchicha huhitaji udongo wenye rutuba ya kutosha na wenye kuhifadhi maji.


UTAYARISHAJI WA SHAMBA
Tengeneza shamba la mchicha kwa kutifua ardhi na kulainisha udongo wenye kina cha sentimeta thelathini. Weka mbolea ya samadi debe moja katika kila mita moja ya mraba. Panda mchicha katika matuta yenye upana wa 90cm-100cm.


AINA ZA MBEGU ZIFAAZO KWA KILIMO HIKI CHA MCHICHA
1.    Amaranthus hybridus huu ni mchicha wenye majani mekundu na mbegu zake ni nyeusi.
2.    Amarantus africana ni mchicha wenye majani ya kijani na mbegu zake ni ni nyeusi.
3.    Amaranthus hypochondriacus ni mchicha wenye majani ya kijani na mbegu zake ni njano hasa mbegu zake hutumika kutengeneza uji wa watoto wachanga
4.    Amaranthus dubius ni mchicha wa kienyeji na Aspinosus ni mchicha wenye miba mingi.

UPANDAJI
·         Changanya mbegu za mchicha na mchanga kwa uwiano wa 1:3, 1:4, 1:5 au 1:6 ili kurahisisha upandaji.
·          Mchicha upandwe katika tuta kwa mistari yenye nafasi ya sentimita thelathini.
·         Funika mbegu kwa kutumia udongo uliolaini na tandaza nyasi kavu baada ya kupanda ili kutunza unyevunyevu na toa matandazo baada ya siku tatu hadi tano tangu siku ya kupanda.
·         Pandikiza mchicha kwa nafasi ya sentimeta kumi na tano kwa ishirini.
·         Mwagilia maji ya kutosha.

KUKUZIA
Tumia mbolea ya samadi iliyolowekwa kwenye maji kwa muda wa masaa ishirini na nne kumwagilia mchicha wako ili kupata mavuno mengi zaidi. Tumia kiasi cha debe moja kwa kila mita moja ya mraba.


NAMNA YA KUDHITI WADUDU WAHARIBIFU
Adui mkubwa wa mchicha ni wadudu aina ya mafuta au kitaalamu zaidi huitwa spinach aphids ambao hufyonza utomvu wa mchicha na kusababisha majani kujikunja , mchicha kusinyaa na kunyauka. Kudhibiti wadudu hawa mwagilia mchicha wako kutumia chombo kinachotoa maji mithili ya mvua kitaalamu kinaitwa "watering can" ili kuwadondosha wadudu hao.
Wadudu wengine ni kitambazi ambacho hula majani ndani kwa ndani hivyo tumia mwarobani kunyunyuzia majani ili kuwaua wadudu hao waharibifu.

MAVUNO
Mchicha huwa tayari kuvunwa baada ya majuma 3 hadi 6 tangu kupandwa au kupandikizwa. Uvunaji huweza kuendelea kwa muda wa miezi 2 hadi 3 kutegemeana na namna utakavyoamua kuuvuna mchicha wako.

KIASI CHA MAVUNO
Kila mita moja ya mraba huzalisha kiasi cha 4kg hadi 5kg za mchicha. Hii inamaanisha kuwa utapata kiasi cha tani 20 hadi 40 kwa hekta moja ya mchicha.

NAMNA YA KUHIFADHI MCHICHA KWA SIKU NYINGI ZAIDI
Baada ya kuvuna funga mashina ya mchicha na weka katika chombo chenye maji kwa kufanya hivyo unaweza kuhifadhi mchicha kwa muda wa masaa 24 yaani siku moja.

Ili kuhifadhi mchicha kwa zaidi ya miezi 4 fanya kama ifuatavyo:-
1.    Vuna mchicha wako kisha usafishe vizuri
2.     Funga katika mafungu.
3.    Chemsha maji mpaka yachemke.
4.     Tumbukiza mafungu ya mchicha katika maji yanayochemka kwa muda wa dakika 1 hadi 2.
5.    Kausha vizuri chini ya kivuli na utunze mchicha wako katika sehemu isiyo na unyevunyevu.
6.    Hapo utakuwa na uhakika wa kuuza mchicha wako supermarket na kuusafirisha hata nje ya nchi.


FAIDIKA KWA KULIMA KILIMO BORA CHA MCHICHA FAIDIKA KWA KULIMA  KILIMO BORA CHA MCHICHA Reviewed by BENSON on September 05, 2017 Rating: 5

No comments